Monday 6 February 2017

Mbowe awakutanisha mameya sakata la UDA

...


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekutana kwa dharura na mameya, manaibu meya na viongozi waandamizi kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili suala la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Hivi karibuni, Rais John Magufuli wakati akizindua Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (DART) alitoa siku tano kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha Sh bilioni 5.8 zilizolipwa na Kampuni ya Simon Group zinapangiwa matumizi baada ya kuuzwa hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa kampuni hiyo.
Jiji la Dar es Salaam kwa sasa linaongozwa na Ukawa chini ya Meya kutoka Chadema, Isaya Mwita. Katika kikao cha baraza Halmashauri ya Jiji hilo chini ya Meya Mwita kilichofanyika wiki iliyopita, kilishindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kutokana na madai ya wajumbe wa baraza hilo kuwa kitendo hicho ni kubariki ufisadi wa kuuza hisa kwa Simon Group.
Kikao hicho cha Baraza kilifanyika ili kuitikia agizo hilo la Rais Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa mradi wa Dart.
Hata hivyo, pamoja na siku tano alizotoa kuisha bado halijapatiwa ufumbuzi. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alipozungumzia suala hilo nje ya ukumbi wa Bunge, alikiri kuwaita viongozi hao wa jiji la Dar es Salaam ili kuzungumzia suala hilo la UDA.
“Nimewaita ili tuzungumze sintofahamu ya suala hili ili tupate msimamo wa pamoja.Tunahitaji kupata suluhisho la suala hili ili wakazi wa Dar es Salaam wanufaike na Uda,” alisisitiza.
Katika jiji la Dar es Salaam lenye halmashauri sita, Ukawa ilishinda halmashauri tatu ikiwemo halmashauri ya jiji hilo inayoongozwa na Mwita, Ubungo ikiongozwa na Boniface Jacob na Ilala chini ya Charles Kuyeko.
Baadhi ya viongozi hao wa Ukawa wa Dar es Salaam walionekana wakirandaranda katika viwanja vya Bunge jana na baadhi yao walikiri kuitwa na mwenyekiti huyo wa Chadema huku wakidai kuwa hawafahamu wameitiwa nini.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene akizungumzia kushindwa kugawanywa kwa fedha hizo alitaka watendaji wa jiji hilo wapewe muda ili waweze kuja na suluhisho la suala hilo.
Alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia maagizo ya Rais Magufuli kuhusu matumizi ya fedha hizo, lakini endapo atapewa maelekezo kuhusu fedha atayatekeleza.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger