Friday 24 February 2017

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Chaipinga TCU.,Chasema Hakijawahi Dahili Wanafunzi Vilaza

...
Siku moja baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutangaza utata wa udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu, wadau wakubwa wa elimu, wamejitokeza kupinga hatua hiyo. Wadau hao ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) .

UDSM kimeeleza kwamba hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyedahiliwa chuoni hapo, ambaye hana sifa za kujiunga na chuo hicho.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Florens Luoga alisema jana kuwa chuo hicho kimeweka utaratibu ambao unaweza mwanafunzi yeyote anayedahiliwa chuoni hapo, awe na sifa zinazohitajika kwa kuwa hawafanyi biashara.

“Sisi hapa ni wakali kuhusu jambo hilo, tukibaini kuwepo kwa mwanafunzi ambaye hana sifa tunamfukuza. Hatusubiri TCU iseme...hata tukibaini kuwa mtu alifanya udanganyifu na alishamaliza chuo, lakini hakuwa na sifa, tunamnyang’anya digrii tuliyompa,” alisema Profesa Luoga na kuongeza:

“Hiki ni chuo, hatufanyi biashara, sisi kazi yetu hapa ni kuandaa wataalamu na ndio maana tunakuwa wakali na makini kuhakikisha wanafunzi tunaowachukua, wote wanakuwa na sifa stahiki”, alisema

 Profesa Luoga alisema uhakiki ambao umefanywa na TCU na kutoa idadi ya wanafunzi 224 wanaosoma chuoni hapo, kuhakikisha wanawasilisha ushahidi wa nyaraka zao, wanaufanyia kazi, kwani kuna uwezekano tume hiyo haina taarifa kuhusu programu zinazoendeshwa na chuo hicho.

Alifafanua kuwa kuna baadhi ya programu maalumu, ambazo Serikali ya Tanzania imeingia na nchi nyingine kwa ajili ya kuendesha programu maalum.

Alisema kozi hizo zimekuwepo chuoni hapo kwa muda wa miaka 40 sasa na zinafanywa kutokana na makubalino ya Serikali ya Tanzania na nchi husika.

Alisema chuo hicho kikongwe Tanzania, kutokana na kuwepo makubaliano hayo kimekuwa kinapokea baadhi ya wanafunzi ambao wanatoka nje ya nchi na akasisitiza kuwa yawezekana ndio hao ambao TCU imeshindwa kupata nyaraka zao.

“Yawezekana kuna taarifa ambazo hazijakaa sawa, tumepokea taarifa ya TCU sisi kama chuo ni jukumu letu kuitekeleza,” alieleza Profesa Luoga.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger