Siku chache baada ya Kituo cha Sheria na
Msaada wa Haki za Binadamu (LHRC) kuhimiza na kutoa rai kwa Watanzania
kufanya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, mwitikio bado umekuwa
mdogo baada ya Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kumshikilia Mwanafunzi wa
Mwaka wa Tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Harold Mmbando
(23) mkazi wa Arusha kwa kosa la kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa Majeshi Tanzania Davis
Mwamunyange.
Kijana huyo kupitia Mtandao wa Kijamii
wa Facebook alisambaza ujumbe wenye maneno makali juu ya viongozi hao na
kutoa taarifa za uchochezi akimtaka Mkuu wa Majeshi kupindua nchi
kutokana na viongozi wote wa juu kuwa nje ya nchi huku kukisalia pasipo
kiongozi wa kukaimu nafasi hiyo.
“Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti” hayo
ni maneno yake mtuhumiwa yaliyonukuliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Charles Mkumbo na kuongeza kuwa mtuhumiwa alitoa maneno makali
pia kwa Dk. Shein kwa kusema “Dk.
Shein akiuawa kama Karume sitashangaa wala kustuka naomba Mungu mauaji
ya kisiasa yaliyotokea Zanzibar yawe kwa viongozi wa kisasa hasa
watawala na sio wananchi wa kawaida”.
Mkumbo
amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi upelelezi
utakapokamilika, huku akitoa rai kwa watu wote wanaotumia mitandao ya
kijamii kutumia pasipo kukiuka sheria na taratibu za kisheria .
Hili sio kosa la kwanza kuripotiwa juu
ya matumizi mabaya ya Mitandao ya Kijamii kwani Isaac Abakuk (40) mkazi
wa Olasiti jijini Arusha pia alipandishwa kizimbani Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha baada ya kumtukana Rais Dk. Magufuli katika ukurasa wake wa
Facebook ambapo ushahidi umekamilika na kesi yake itaanza kusiklizwa
mfululizo kuanzia June 5 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment