Polisi wa Kenya wanamshikilia mtu mmoja mjini Bungoma baada ya kuning’inia kwenye helikopta iliyoubeba mwili wa aliyekuwa mfanyabiashara Jacob Juma.
Mtu huyo, Saleh Wanjala ambaye
hakutoa sababu za kufanya hivyo, alishikiliwa na polisi huku akipata
matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa Bungoma.
Wanjala alionekana
akining’inia kwenye helikopta iliyobeba mwili wa mfanyabiashara huyo
wakati ikipaa kutoka kwenye Uwanja wa Posta mjini Bungoma baada ya
wananchi kutoa heshima za mwisho.
Wanjala aliamua kuidandia helikopta hiyo wakati ikiondoka kupeleka mwili wa Juma nyumbani kwake katika Kijiji cha Mungore.
Akisimulia
mkasa huo, Wanjala alisema alikuwa karibu na helikopta hiyo wakati
ikianza kupaa na kwamba aliumia baada ya mguu wake kukwama.
“Nilikuwa
nimeketi chini ya helikopta na wakati ilipokuwa inaanza kupaa, mguu
wangu ulikwama hapo ikabidi nijishikilie vizuri ili nisianguke,” alisema
Wanjala.
Rubani wa helikopta hiyo alilazimika kumpeleka hadi
uwanja wa ndege wa Bungoma mita 700 kutoka kwenye uwanja huo lakini
Wanjala aliamua kuruka na kuumia vibaya miguu na mikono. Muuguzi wa
Hospitali ya Bungoma, Leah Atsewa alisema bado wanamfanyia uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment