Tuesday 19 April 2016

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Yamuonya Uhuru Kenyatta

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetishia kuichukulia Kenya hatua kali isiposalimisha kwa mahakama hiyo washukiwa watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya kutatiza mashahidi.

Msemaji wa ICC Fadi el Abdallah alisema mahakama hiyo itairipoti Kenya kwa Baraza la Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Roma (ASP)  kama itaendelea  kushikilia msimamo wa kutowawasilisha Wakenya hao watatu mbele ya mahakama hiyo mjini Hague, Uholanzi.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Bi Fatou Bensouda, amepata kibali cha kuwakamata aliyekuwa mwanahabari Walter Osapiri Barasa, wakili Paul Gicheru na Philip Bett kwa madai ya kutatiza mashahidi katika kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang.

Agizo la kukamatwa kwa Bw Barasa lilitolewa Oktoba 2013 ilhali lile la kukamatwa kwa Philip Bett na Paul Gicheru lilitolewa Septemba 2015 kwa madai kuwa walihonga mashahidi.

Kesi dhidi ya Bw Ruto na Sang ilitupiliwa mbali mapema mwezi huu kwa misingi kuwa ilikosa ushahidi wa kutosha kutokana na mashahidi kutatizwa.

Akihutubia hafla ya maombi mjini Nakuru mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta alitangaza kuwa hakuna Mkenya mwingine atakayefikishwa katika mahakama ya ICC kujibu mashtaka.

Alisema kusitishwa kwa kesi hizo ndio mwisho wa ushirikiano baina ya Kenya na mahakama hiyo ya kimataifa.

“Ukurasa huo tayari tumefunga na hatutakubali Mkenya kurudi katika mahakama ya ICC. Tuna mahakama zetu za kutatua matatizo yetu,” akasema rais katika uwanja wa michezo wa Afraha.

“Kenya ikipuuza agizo la kuwasilisha washukiwa hao, majaji watawasilisha ripoti yao mbele ya Baraza la Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Roma ambalo litachukua hatua zinazostahili,” akasema Bw Fadi.

Kifungu cha 87(7) cha Mkataba wa Roma kinasema: “Nchi mwanachama ikikataa kushirikiana na ICC na kutatiza utendakazi wake, mahakama inaweza kuwasilisha malalamishi kwa baraza la ASP.”

Wiki iliyopita, Bi Bensouda alisema kusambaratika kwa kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang kulichangiwa kwa kiwango kikubwa na kutatizwa kwa mashahidi na akataka washukiwa hao watatu wapelekwe ICC.

Alisema mashahidi 17 ambao walikuwa wameandaliwa na upande wa mashtaka walijiondoa baada ya kutishwa na kutengwa.

Hapo jana, Fadi alisema ICC inajua kuhusu tangazo la Rais Kenyatta wa Kenya kutosalimisha washukiwa hao na kuwa inafuatilia hatua hiyo kwa karibu.

“ICC haijapokea pingamizi zozote rasmi kutoka Kenya kuhusu mashtaka ya Wakenya watatu wanaoshukiwa kutatiza mashahidi wa kesi za ghasia  baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007,” alisema Bw Fadi
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger