Wednesday 4 November 2015

TEMCO: Uchaguzi Ulikuwa HURU na wa HAKI

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

TIMU ya Waangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu (TEMCO), imesema kwamba tathmini yao kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, unastahili hati ya uchaguzi safi, huru na wa haki ambao umeangukia alama A. 

Aidha, Temco imesema kwamba hata hivyo ikizingatiwa hisia za kutoridhishwa na baadhi ya wadau wa uchaguzi kuhusu uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), sheria na kanuni pamoja na upungufu kadhaa, imeshindwa kuupa uchaguzi huo alama A na hivyo kutoa alama B kwamba ingawa uchaguzi ulikuwa wa huru na haki. 

Akitoa taarifa ya awali ya TEMCO kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kiongozi wa timu hiyo, Dk Benson Bana alisema upungufu mdogo hauepukiki hivyo timu yao kutoa alama 60-69 ambayo inaangukia kwenye alama B. 

“Waangalizi wa ndani tulipoangalia kutoka kwenye taarifa za waangalizi wetu waliokuwa wamesambaa nchi nzima, toka mwanzo wa uchaguzi huu yaani katika utengaji majimbo, uteuzi ndani ya vyama, kampeni na siku yenyewe ya kupiga kura uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania unaangukia alama A, lakini kutokana na dosari hizo tunatoa alama B,” alisema Dk Bana. 

Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na kutoruhusu Watanzania walioko nje ya nchi kupiga kura, kuwepo na mgombea binafsi na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa kwamba sio waajiriwa wa Tume. 

Aidha, Dk Bana aliyataja mapungufu mengine kuwa ni katika kampeni hizo wagombea walijinadi wao badala ya vyama vyao vilivyowasimamisha, jambo ambalo lilijitokeza hasa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

“Hili halikutufurahisha kabisa, mgombea kuwa mtu binafsi kuliko kunadi taasisi zao hilo halikuwa jambo jema katika kukuza demokrasia na hii imejitokeza hasa kwa CCM na Chadema,” alisema Dk Bana. Alisema kwa mujibu wao, kampeni za vyama kuna ambazo hazikuzingatia muda na pia maneno yasiyofaa kujitokeza katika kampeni hizo. 

Hata hivyo, alisema tathmini za Temco zilionesha siku ya kupiga kura, hakukuwa na mambo yoyote ya kusababisha uchaguzi usiwe wa huru na wa haki watu walipiga kura katika hali ya amani na pia kura zilihesabiwa katika hali hiyo bila kuwapo vurugu pamoja na matokeo kutangazwa. 

Dk Bana alisema tathmini yao inaonesha pia kuwa vyama vya CCM, Chadema na CUF vilitumia demokrasia vizuri katika kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya vyama na kwamba vyama vingine havikuwa na demokrasia hiyo na kwamba kulikuwa na matumizi makubwa ya fedha kwa CCM na Chadema. 

Kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, Dk Bana alisema Temco imepokea kwa mshituko uamuzi wa kufutwa matokeo ya uchaguzi uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar kwa madai kuwa haukuwa wa huru na haki. 

“Tulikuwa na watazamaji 22 wa muda mrefu na 704 wa muda mfupi wa Temco Zanzibar, ambao waliangalia mchakato mzima wa uchaguzi na taarifa zao za awali zinaonesha kuwa shughuli zote za kabla ya uchaguzi zilifanyika kwa amani na utulivu, inashangaza uamuzi wa kusitisha kura zikiendelea kuhesabiwa,” alisema Dk Bana. 

Alisema Temco inaishauri ZEC kufikiria upya uamuzi huo kwa lengo la kufikia uchaguzi huru na wa haki kuimarisha amani, huku ikiitaka Serikali kuingilia kati kuleta amani kwa Zanzibar ikishirikiana na wadau wengine wa amani.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger