Sunday 8 November 2015

Rais Magufuli: Manunuzi ya Serikali Kuondoka na Watu

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


RAIS John Magufuli, ametoa agizo mahususi katika usimamizi wa manunuzi ya Serikali, ambayo yamekuwa yakitumika vibaya kwa kugeuzwa mwanya wa kuiibia Serikali. 

Ametoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es Salaam jana katika kikao chake cha kwanza na watendaji wakuu wa Serikali; wakiwemo makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade. 

Katika kikao hicho, Rais Magufuli ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika vibaya kwa watendaji wabadhirifu kununua vitu vya Serikali kwa bei ya juu kuliko bei halisi iliyopo sokoni. 

“Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja,” ameonya Rais Magufuli na kusisitiza kwamba kuwajibishwa huko kutahusu yeyote atakayeongeza bei, hata kama bei iliyoongezwa ni ya vitu vya bei ndogo kabisa katika jamii. 

*Mkakati wa Magufuli 

Kauli za Rais Magufuli katika kikao hicho cha jana na cha juzi alipofanya ziara ya kushtukiza ya Wizara ya Fedha, zimedhihirisha mkakati wake wa kuongeza mapato ya Serikali, kwa kuwa katika vikao vyote hivyo, amesisitiza umuhimu wa kukusanya kodi kwa kila mfanyabiashara mkubwa bila woga. 

Mbali na dhamira hiyo ya kuongeza zaidi mapato, agizo la kuchunga manunuzi ya umma, imeonesha dhamira nyingine aliyonayo katika kubana matumizi, kwa kuwa eneo la manunuzi ya umma, ndilo linalochukua asilimia 70 ya matumizi ya Serikali. 

Mbali na eneo hilo kuchukua sehemu hiyo kubwa ya mapato ya Serikali, lakini eneo hilo pia limekuwa likiathiriwa zaidi na vitendo vya rushwa hasa katika utoaji wa zabuni za Serikali. 

Mkakati huo wa Rais Magufuli, umezidi kudhihirisha dhamira yake aliyotangaza wakati wa kampeni, ya kwenda kuziba mianya ya rushwa na uvujaji wa mapato, ili fedha za Serikali zikatekeleze ahadi zake na kutatua kero za Watanzania wa kipato cha chini.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger