Mbunge
wa Viti Maalum (Chadema), Rose Kamili, aliyedai ametekwa na kuteswa
wakati wa uchaguzi mdogo mkoani Iringa, amemtuhumu Mwenyekiti wa CCM
mkoani humo, Jessica Msambatavangu kuwa anahusika na mashambulizi dhidi
yake.
Kamili alidai alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga uliofanyika mapema mwezi huu.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari mjini Dodoma, siku moja baada ya kula kiapo cha kuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba, alisema akiwa vijijini alikokwenda kusambaza mawakala wa kusimamia uchaguzi wa Kalenga, alitekwa na watu asiowafahamu ambao walimwingiza kwenye gari na hadi ofisi za CCM mkoani Iringa.
“Nilipofikishwa katika ofisi hizo nilianza kushushiwa kipigo kikali hata kabla sijashushwa kwenye gari. Nilipelekwa katika moja ya ofisi na kukutana Mwenyekiti wa CCM Msambatavangu na kumtambua,”alisema.
Alieleza kusikitishwa na hatua ya mwanamke mwenzake akimfanyia visa hivyo.
Alisema kuwa Msambatavangu aliamuru aletwe baunsa ambaye ndiye aliyeanza kumpa kipigo kikali huku kiongozi huyo akisisitiza apigwe zaidi.
Alisema baada ya kupigwa kwa zaidi ya dakika 20, lilikuja gari la polisi na wakamweleza kuwa wamefika mahali hapo kwa ajili ya kumwokoa na kumchukua kumpeleka kituoni.
Kamili alisema alipofikishwa polisi hali yake ilianza kuwa mbaya ndipo walipomwandikia fomu namba tatu (PF3) na kumkimbiza kwenye matibabu.
Alisema anasikitishwa kuwa hata baada ya kumtaja mbaya wake polisi, mwenyekiti huyo hajakamatwa na badala yake yupo ndani ya bunge la katiba huku kukiwa hakuna hata jalada alilofunguliwa dhidi ya kiongozi huyo.
Aidha Kamili alilituhumu Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa upendeleo wa dhahiri na kutojali madhila yaliyompata.
“Tangu nijeruhiwe hakuna tamko lolote lililotolewa na uongozi wa Bunge kuhusiana tatizo lililonikuta, licha ya kuwa Spika ni mwanamke.”
Alisema mbali na kutoa tamko, hakuna msaada wowote wa kitabibu alioupata kutoka bungeni, lakini wabunge wa CCM wanapougua bunge linakuwa mstari wa mbele kutoa huduma.
Umoja wa wabunge wanawake wa vyama vya Upinzani wametoa tamko la kulaani kitendo hicho na kuitaka Serikali ichukue hatua haraka kushungulikia tatizo hilo.
Akitoa tamko hilo mbele ya wandishi wa Habari, Mwenyekiti wa wabunge hao, Suzan Lyimo alisema kuwa kitendo alichofanyiwa mwanamke mwenzao ni kibaya kinachowakatisha wanawake tamaa.
0 comments:
Post a Comment