Friday 28 March 2014

Seif: Hatuko tayari kujadili serikali mbili

...

Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya Kikwete.

Amesema tayari amewaandikia barua Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa kuna njama za kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar ni nchi” na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa Wazanzibari kamwe hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka kwa Rais Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa Muungano kuwa wa serikali tatu.
Alisema Jaji Warioba aliweka kando itikadi yake ya CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti la Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza Muungano wenye mfumo wa serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili hauvumiliki na kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza kutumia sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara wanataka Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo hilo halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae,” alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba yake alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala yake akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na kutaja ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu ni wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga. Mambo yamebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na kubabaika,” alisisitiza Maalim Seif.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger