Monday 31 March 2014

YANAYOENDELEA BUNGE LA KATIBA DODOMA 31st MARCH 2014

...

Raza: Tuache utoto tujadili Katiba

Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza ametaka wajumbe wenzake kuheshimiana bila kujali wingi au uchache wa wajumbe kwenye makundi yao, kama kweli wana dhamira ya dhati ya kutunga Katiba.
Akizungumza na gazeti hili, Raza alisema mwenendo wa Bunge siyo mzuri na hauleti picha nzuri kwa mamia ya wananchi ambao wanategemea wapatiwe Katiba bora itakayoondoa tatizo yao.
“Tupo hapa tunalipwa kwa siku Sh.300,000 na tunajua huku nyuma kuna maelfu ya wananchi wetu hawana hata Sh.1000 ya chakula, halafu tunakaa hapa tunafanya vurugu na kuacha kusikilizana hata katika hoja za msingi? Nadhani hatuwatendei haki wananchi,” alisema Raza.
Alisema hakuna asiyejua matatizo ya wananchi. Kinachotakiwa sasa ni kukaa na kuanza kupitia Rasimu ya Katiba, hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kuiwasilisha bungeni.



Sarungi: Sikubaliani na rasimu mpya

Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Maria Sarungi amepinga utaratibu wa kuwasilishwa tena bungeni mabadiliko ya Kanuni ambayo yataibua upya vurugu na hivyo vikao vya Bunge kuendelea kuahirishwa.
Sarungi  kuwa kanuni ambazo zilipitishwa kwa Azimio la Bunge Machi 11, zilitokana na kazi kubwa iliyofanyika, ikiwepo vikao vya maridhiano.
“Tulikaa karibu mwezi mmoja kupitisha kanuni hizi tena kwa maridhiano. Watu walikaa bungeni hadi usiku. Iweje leo hata bado hatujaanza kuzitumia walete mabadiliko?” alihoji.
Alisema kitendo cha kurejesha mijadala ambayo tayari ilipitishwa na Bunge ni kutaka kuibaua tena vurugu bungeni na hivyo kupoteza fedha za umma.
“Nadhani Watanzania wanajionea watu ambao wanakwamisha Bunge. Hapa kuna matumizi mabaya ya fedha. Kama tulipitisha kila kitu wenyewe iweje leo walete tena mambo yale yale upya,” alisema Sarungi.


Mjumbe: Wanasiasa wamenisikitisha


Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Rispa Miguma kutoka kundi la wateule 201 wa Rais, amesema kwa anayoyaona bungeni, hawezi hata siku moja kutamani kuwa mwanasiasa.
Alisema anachojifunza kutoka kwa wanasiasa wanaoshiriki Bunge la Katiba kinamsikitisha kutokana na kugeuza chombo hicho kuwa uwanja wa siasa badala ya mahala pa kuzungumzia masilahi ya taifa.
“Badala ya kuangalia kitu ambacho wananchi walio nje ya Bunge wanataka, mnatumia jina la wananchi, Watanzania eti wamewatuma wakati hata kuzungumza nao wengine hamzungumzi nao,” alisema.
Miguma alitoa ujumbe wa maneno ya Mungu dhidi ya wanaotuhumiana kuhusika na vitendo vya rushwa katika shughuli hiyo akisema:
“Huu ni ujumbe kwa kundi la 201 hasa kwa wale ambao wanahusika. Ujumbe wenu kwanza ni huu hapa, kwanza kabisa usimshuhudie jirani yako uongo, pili inunue kweli na wala usiiuze, tatu afichaye kosa atafuta kupendwa.”



Bunge livunjwe tukawaombe radhi wananchi- Mjumbe

Dodoma. Mivutano katika Bunge la Katiba imemchukiza mmoja wa wajumbe wa chombo hicho, Michael Laizer ambaye amemshauri mwenyekiti wake, Samuel Sitta amwombe Rais kuvunja Bunge.
Laizer pia amewataka wajumbe wenzake kurudi katika maeneo yao ili wakaombe radhi kwa Watanzania kutokana na ufujaji wa fedha unaotokana na kuwepo kwao kwenye vikao vya Bunge.
“Mwenyekiti narudia tena kama watu hawataki uamuzi huu, nakushauri andika barua kwa Mheshimiwa Rais ili aje alivunje Bunge na twende makwetu,” alisema Laizer.
Laizer alilishutumu Bunge hilo kuendelea kutafuna fedha wakati watu wengine wanaishi maisha magumu zaidi kiasi cha kushindwa kupata hata mlo mmoja kwa siku.
Alipinga muda ambao wametumia wajumbe hao kwa ajili ya kujadili masuala ya kanuni pekee bila hata ya kufikia uamuzi, akisema ndoto yake ni kuwa hadi wiki hii waanze kuchambua vifungu vya katiba.
Aidha alisema watu wenye umri mkubwa kama yeye (Laizer) wanaogopa kuchangia hoja kutokana na tabia ya kuzomeana.


Vurugu zawa kero Dodoma

Dodoma. Kitendo cha kuahirishwa mara kwa mara kwa vikao vya Bunge la Katiba kimewakera baadhi ya wakazi wa Mji wa Dodoma ambao sasa wanapendekeza chombo hicho kivunjwe.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema kuwa vurugu za bungeni zimewachosha na kuwafanya wakose hamu ya kuangalia au kusikiliza mijadala.
Katibu wa uchumi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani Dodoma, Mary Chihoma alisema kwa hali ilivyo sasa, haya ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
“Hatuwezi kusema ni mtu mmoja ndiye ambaye anastahili kubeba lawama hizo. Hawa wote wanatakiwa kulaumiwa moja kwa moja kwani wanakula kwa wasichokifanyia kazi,” alisema Chihoma.
Mwanasiasa huyo alitoa wito kwa wajumbe hao kumwogopa Mungu na kurudi kwenye mjadala wa msingi wa kutunga Katiba.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger