Saturday 15 May 2021

NAMUNGO FC WAITUNISHIA MISULI YANGA SC ...MASHABIKI WAONDOKA KWA HASIRA BAO KUKATALIWA

Vigogo Yanga SC wamelazimishwa sare ya bila mabao na wenyeji Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Hata hivyo mashabiki wa Yanga waliondoka na hasira uwanjani kufuatia refa Hance Mabena wa Tanga kukataa bao lao lililofungwa na mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Sogne kwa kichwa akimalizia mpira wa kona kipindi cha pili.

Kwa sare hiyo, Yanga SC inafikisha pointi 58 baada ya kucheza mechi 28 na inabaki nafasi ya pili, sasa ikizidiwa pointi tatu na mabingwa watetezi, Simba SC ambao pia wa mechi tatu mkononi, wakati Namungo FC yenyewe inafikisha pointi 36 baada ya mechi 26 nayo pia inabaki nafasi ya 10.

Via Binzubeiry blog
Share:

AZAM, SIMBA NA YANGA ZOTE ZATINGA ROBO FAINALI LIGI KUU YA TAIFA YA VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 20


TIMU za Simba, Yanga na Azam FC zimefuzu Robo Fainali ya Ligi Kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya kumaliza katika nafasi mbili za mwanzo katika makundi yao.

Pamoja na Simba walioshika nafasi ya pili Kundi B, Yanga walioongoza Kundi A na Azam FC waliomaliza nafasi ya pili Kundi A, timu nyingine ni Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mwadui, Tanzania Prisons na JKT Tanzania.

Prisons na JKT wamefuzu kama ‘best losers’ baada ya kukusanya pointi nyingi kwenye nafasi ya tatu katika makundi yao ikilinganishwa na Ruvu Shooting.
Share:

RAIS SAMIA AMTEUA MGOMBEA URAIS TANZANIA 2020 QUEEN SENDINGA KUWA RC IRINGA

Queen Cuthbert Sendinga
Queen Cuthbert Sendinga

Na Damian Masyenene - Shinyanga
Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Queen Sendiga ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa mkoa wa Iringa.

Queen Sendiga ambaye alikuwa mgombea wa urais mwanamke kivutio kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ameteuliwa leo akichukua nafasi ya Ali SalimHapi ambaye amehamishiwa mkoa wa Tabora.

Uteuzi huo unakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuahidi kuwa siku za usoni atateua viongozi mbalimbali katika nafasi za uongozi bila kujali itikadi zao za kisiasa bali ataangalia uwezo wao wa kuliletea taifa maendeleo na sifa zao safi.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Mei 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam ambapo alieleza kuwa lengo ni kuwa na umoja wa kitaifa.

"Huko mbele wakati nikiendelea kusuka serikali sitaangalia itikadi ya mtu kisiasa. mtu yeyote nitakayeona ana uwezo wa kusaidia taifa letu na kuleta tija katika eneo fulani, nitamteua afanye kazi bila kujali anatoka chama gani. ilimradi tu awe hana dosari ya kiusalama, wala dosari ya kimaadili," alinukuliwa Rais Samia Mei 7, 2020.

Uteuzi wa Queen Sendinga unaleta sura sawa na ule wa Anna Mgwira ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2017 akichukua nafasi ya Said Meck Sadiki, ambapo Anna alikuwa mgombea urais wa Tanzania mwaka 2015 kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.


Mwaka 2015 Queen aliwania ubunge katika jimbo la Kawe lakini hakufanikiwa kushinda ubunge ambapo jimbo la Kawe lilichukuliwa na Halima Mdee ambaye aliwania ubunge kwa tiketi ya chama cha Chadema.
Queen Sendiga akikabidhiwa fomu ya kugombea urais wa Tanzania mwaka 2020


Share:

RAIS SAMIA AMTEUA MWAKITALU KUWA MKURUGENZI WA MASHTAKA 'DPP'... DK. MHEDE MABASI YA MWENDOKASI 'UDART'

Sylivester Mwakitalu
**
Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi za Serikali akiwemo  Sylvester Mwakitalu kuwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuchukua nafasi ya Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu.

Taarifa ya uteuzi wa wakuu hao wa taasisi pamoja na wakuu wa mikoa ulioanza leo Jumamosi Mei 15, 2021 imetolewa leo na Mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa, ikieleza kuwa wataapishwa Mei 18, 2021 Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Inaeleza kuwa Rais Samia amemteua Neema Mwakalyelye kuwa Naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Joseph Pande kuwa naibu mkurugenzi wa mashtaka (DDDP).

Rais Samia pia amemteua Dk Edwin Mhede kuwa mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuchukua nafasi ya Ronald Lwakatale ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Nenelwa Mwihambi ameteuliwa kuwa katibu wa Bunge kuchukua nafasi ya Dk Stephen Kagaigai ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Soma pia
Share:

HUYU NDIYE DK. PHILEMON SENGATI MKUU MPYA WA MKOA WA SHINYANGA...ZAINAB TELACK AHAMISHIWA LINDI

Dk. Philemon Sengati
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati

Na Damian Masyenene - Shinyanga
Leo Mei 15, 2021 mkoa wa Shinyanga umempata mkuu wa mkoa mpya, Dk. Philemeon Sengati baada ya kudumu kwa miaka mitano na Zainab Telack aliyeuongoza mkoa huo tangu mwaka 2016 akipandishwa cheo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema.

Dk. Sengati ameteuliwa leo na Rais Samia Suluhu katika mabadiliko ya safu ya viongozi wakuu wa mikoa.

Dk. Sengati kabla ya uteuzi wa leo alikuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambapo alirithi mikoba ya Aggrey Mwanri Julai 3, 2020 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli kuchukua mikoba ya Mwanri ambaye alistaafu.

Kabla ya uteuzi huo wa kuwa RC wa mkoa wa Tabora Julai 3, mwaka jana, Dk. Sengati alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Magu, Dk. Sengati alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma akiwa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma.

Leo ameteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga kuchukua mikoba ya Zainab Telack ambaye amehamishiwa mkoa wa Lindi, ikiwa ni miezi miezi 10 tu baada ya kuwa RC mkoani Tabora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa Taasisi Mbalimbali. Tazama majina yote hapa
Share:

RAIS SAMIA AMTEUA ACP SALUM RASHID HAMDUNI KUWA MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU....AMKUMBUKA MAKONGORO NYERERE


Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Rashid Hamduni
Makongoro Nyerere

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa na Watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali ambapo kati yao amemteua Bwana Makongoro Nyerere kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Rashid Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali John Mbungo ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Soma Majina ya Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa Taasisi Mbalimbali walioteuliwa leo.
Share:

Breaking News : RAIS SAMIA AMEFANYA UTEUZI WA WAKUU WA MIKOA NA WATENDAJI WA TAASISI..WENGINE WAHAMISHWA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa Taasisi Mbalimbali.
Share:

MREMBO AFUNGA VIRAGO NA KUMKIMBIA MME WAKE AKIDAI NI MLAFI SANA


Mrembo kutoka mtaani Githunguri, kaunti ya Kiambu nchini Kenya ameamua kufunga virago na kumkimbia mumewe akidai hangevumilia kamwe tabia yake ya ulafi.

 Penyenye zinasema kwamba barobaro alianza tabia hiyo miezi kadhaa iliyopita na haijulikani ni wapi haswa alikotoa tabia hiyo kwa mujibu wa Taifa Leo.

“Jamani, sijui mume wangu amekuwa jini au nini! Nikipakua chakula anakula chote hivi kwamba mimi na wanangu nyakati nyingi tunakosa chakula na kulala njaa," mama alilia. 

Mama huyo alidokeza kwamba hata baada yake kulalamika mara kwa mara mumewe alikuwa akijitia hamnazo na kuendelea kufagia tu chakula chote jikoni.

 “Anakula hadi anavua shati, anakula ovyo na kulala kwenye sofa,” mrembo alieleza kwa masikitiko makubwa.

 Siku ya kisanga inasemekana mama aliandaa chapati kwa kitoweo cha kuku na kwa kuwa alikuwa hodari sana kwa mapishi watoto walikuwa na furaha isiyo na kifani.

Inasemekana kabla ya mama kupakua mlo, jamaa aliingia kwa kishindo.

 “Hujapakua chakula? Wagonja nini wewe jamani?” baba wa nyumba aliuliza kwa hasira. Pindi tu mama alipoweka chapati kwenye sinia, jamaa aliwaashiria watu wote kuketi kando na kumgonja ashibe.

 Inasemekana bila hata kujali watoto, alianza kula chapati kwa kasi huku akizirarua mara mbili tu. Lofa alirarua chapati zote familia yake ikisalia kumtazama. Wanawe walilia wakijishika matumbo, shetani mtu asione hata aibu wala huruma.

Tabia ya jamaa ilimfika kwenye koo mama naye mara moja akaingia chumbani akakusanya virago akawachukua wanawe na kushika njia.

 “Twendeni wanagu hapa tutakufa njaa,” aliwaambia wanawe. “ Mnaenda wapi nyinyi?” lofa aliuliza huku chapati ya mwisho ikiwa kinywani. “Hukunitoa pangoni. Nina kwetu na ndiko ninakoenda,” mama alimjibu jamaa kwa ujeuri kisha akaondoka.

 “Watarudi tu. Lakini hii tabia yangu itakuja kuniua maskini mie. Nitaikomeshaje jamani? Najipata nala tu bila breki!” jamaa alimweleza rafiki yake siku iliyofuata. Hata hivyo haijulikani iwapo mke na mume walisuluhisha tofauti zao na kurejea nyumbani na watoto.

Share:

OFISI YA WAZIRI MKUU YASHEREKEA EID NA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe.Ummy Nderiananga akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Watu wenye Ulemavu Yombo, Jijini Dar es Salaam
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akitoa mkono wa Idd kwa baadhi ya wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo, alipoambataana na viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kwenda kushiriki chakula cha mchana na wanachuo hao katika kusherekea sikukuu ya Eid El Fitr
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu, wakiwasikiliza viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walikwenda chuoni hapo kwa lengo la kula nao chakula cha mchana katika kusherekea sikukuu ya Eid El Fitr.

*******

Na Mwandishi Wetu

Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitr.

Akimwakilisha Waziri Mkuu katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema lengo la kuandaa chakula hicho ni kuendeleza umoja na kutoa faraja kwa kundi hilo la watu wenye ulemavu.

Katika kusherekea sikukuu hii ya Idd El Fitir, Ofisi ya Waziri Mkuu iliona ni muhimu kuandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na vijana wetu wa chuo hiki cha watu wenye ulemavu hivyo Waziri Mkuu pamoja na Waziri wetu wa Nchi, Mhe. Jenista Mhagama wamenituma niwawakilishe katika tukio hili kwasababu wao wapo katika majukumu mengine ya kitaifa, amesema Ummy Nderiananga.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Prof. Jamal Katundu, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuyajali na kuyasaidia makundi mbali mbali ya watu wenye mahitaji maalum kikiwemo chuo hicho cha watu wenye ulemavu.

Hili jambo kubwa sana na ndio maana mimi kama Naibu Katibu Mkuu nimepewa jukuma la kuratibu suala hili na kama mlivyoona vijana wetu wamefurahishwa sana na tukio hili hivyo natumie fursa hii kutoa wito kwa watu wenye uwezo na taasisi mbali mbali zenye mafungu ya kusaidia jamii kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuja kuwasaidia vijana wetu, Prof. Jamal Katundu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, amesema menejimenti pamoja na wanachuo wamelipokea tukio hilo kwa furaha sana ambapo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa tukio hilo.

Aidha, baadhi ya wanachuo wakiwemo Joseph Baraza na Evodia Mwombeki wameelezwa kufurahishwa na tukio hilo na wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walijumuika nao katika chakula hicho.

Tumefurahi sana kwa namna moja ama nyingine kwasababu huwa tunajisikia furaha sana kujumuika na watu tofauti tofauti na kujiona kwamba hatujatengwatunawashukuru sana kwa tukio hili la leo na Mungu awabariki sana, amesema Evodia Mwombeki, Mwanafunzi katika fani ya Kilimo na Ufugaji.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Kwasasa kina jumla ya wanafunzi 76 na kinatoa kozi mbali mbali zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.

Share:

NEC YAVIONYA VYAMA VINAVYOSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MUHAMBWE, BUHIGWE NA KATA 5


Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, vina wajibu wa kuweka mawakala kwenye vituo vya kupigia na kujumlisha kura lakini mawakala hao na wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia Sheria za Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2021 na kushirikisha kata za Buziku (Halmashauri ya Wilaya ya Chato), Bugarama (Halmashauri ya Wilaya ya Geita), Igunga (Halmashauri ya Wilaya ya Igunga), Ligoma (Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru) na Kata ya Miuta iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.

Jaji Mst. Kaijage amesema Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.

Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na kata tano za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua wabunge na madiwani wanaowataka.

Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zinakamilika leo jioni saa 12:00 hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.

“Pili upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”alisema Jaji Mst. Kaijage na kuongeza:

“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye majimbo na kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Kifungu cha 62 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.”

“Mojawapo ya vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura anaweza kutumia ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika  ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupga kura. Aidha majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala”

Jaji Mst. Kaijage amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.

Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Amewakumbusha wapiga kura kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka jana yaliyokubaliwa na wahusika wote vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, itahusisha idadi ya wapiga kura watakaopiga kura 303,965  walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kupigia kura ni vituo 793.


Share:

VIDEO : Rayvanny Ft. Innoss’B – Kelebe

 VIDEO : Rayvanny Ft. Innoss’B – Kelebe



Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI MEI 15,2021












Share:

Friday 14 May 2021

Wadau Wa Mabwawa Watakiwa Kuzingatia Sheria

 


WADAU wa mabwawa wamesisitizwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo na kuhakikisha mabwawa yanasajiliwa kwenye Mamlaka husika ili yatambulike kisheria kwa lengo la kuepusha  madhara yanayoweza kujitokeza kwa jamii na mazingira kwa ujumla.

Wito huo umetolewa hivi karibuni Jijini Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo vya Maji kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa wakati wa kufunga warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.

“Zingatieni Miongozo ya Usalama wa Mabwawa, tunahitaji uwepo wa mabwawa yenye manufaa na ambayo ni salama kwa viumbe hai na mazingira na si vinginevyo,” alielekeza Rwebugisa.  

Rwebugisa alisisitiza umuhimu wa kutumia Watalam wa Mabwawa waliosajiliwa kuanzia hatua za awali za usanifu hadi hatua ya usimamizi wakati tayari yameanza kazi ili kuepukana na changamoto zinazoweza kusababisha madhara.

Alisema baaadhi ya mabwawa hukutana na changamoto kadhaa huku mengine yakishindwa kukidhi matakwa ya matumizi yaliyokusudiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoshirikisha wataalam.

“Kabla hamjaanza kuchimba ama kujenga mabwawa hakikisheni mnashirikisha wataalam ili wajiridhishe kulingana na utaalam wao kama bwawa linalotarajiwa kujengwa mahali hapo linastahili na pia namna gani lijengwe ili kuepukana na changamoto zinazozuilika,” alisisitiza Rwebugisa.

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza endapo bwawa litajengwa bila ushauri wa kitaalam ni pamoja na kuvuja, jambo ambalo alisisitiza kuwa ni hatari kwa afya na maisha ya viumbe wanaozunguka eneo husika.

Alisema jamii pia inapaswa kuelimishwa na kutambua umuhimu wa mabwawa hasa ikizingatiwa kwamba mabwawa yanazo faida lukuki ambazo baadhi yake alizitaja kuwa utunzaji wa mazingira kwa kuhifadhi taka hatarishi lakini pia ni chanzo cha mapato kutegemeana na aina ya bwawa.

“Mabwawa yana faida nyingi sana, ni muhimu jamii ikaelimishwa juu ya faida hizo lakini pia namna ya kuyalinda na kuyatunza ili kuepusha madhara,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu warsha, Rwebugisa alisema imejikita kujadili Miongozo ya Usalama wa Mabwawa na kwamba wadau walioshiriki wajitahidi kufuata miongozo walioijadili.

Alielekeza washiriki kuhakikisha wanaendelea kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha usalama wa mabwawa na kuendeleza mawasiliano ya karibu na ya kila mara na Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wake.

“Mapendekezo yenu tumeyachukua kwa maboresho kwani miongozo iliyopo sio misahafu hivyo tutakuwa tunaboresha kila tunapoona kwa pamoja umuhimu wa kufanya hivyo,” alisema.

Warsha hiyo imeshirikisha Viongozi kutoka Wizara ya Maji, Wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), Wizara na Taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.


Share:

Wizara ya Madini yaagiza ukaguzi leseni za Madini Njombe

 Na Asteria Muhozya, Njombe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe kufanya ukaguzi wa Leseni zote 245 za Uchimbaji Madini mkoani humo ili kujua maendeleo ya uendelezwaji wake.

Agizo hilo linafuatia ombi lililowasilishwa na wachimbaji wadogo wa Madini mkoa wa Njombe ambao wameiomba Wizara kuwapatia maeneo ya kuchimba kutokana na sehemu kubwa kushikiliwa na wawekezaji kwa kipindi kirefu pasipo kuyaendeleza.

 ” Nakuagiza RMO fanya uchambuzi wa Leseni zote kujua zina hali gani, ikiwa zinalipiwa, ni maendeleo gani  yamefanyika ili kuanzia hapo wizara ichukue hatua. Tunapotoa leseni tunataka watu waziendeleze na wachimbe siyo kuzifungia kabatini,’’amesisitiza Prof. Msanjila.

Prof. Msanjila ameongeza kuwa, moja ya vipaumbele vya Serikali na kama alivyoeleza Waziri wa Madini katika Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ni pamoja na kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo   ili wachimbe, hivyo, wizara itahakikisha inalifanyia kazi kwa karibu suala hilo.

Amefanunua kuwa, endapo mmliki wa leseni ana nia ya kuiuza leseni yake hakatazwi isipokuwa anapaswa kuiendeleza kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine. ‘’ Ukitaka kuuza leseni lazima useme uliifanyia nini kabla ya kuiuza. Huu ndiyo utaratibu wa Sheria,’’ amesema.

Akizungumzia mwenendo wa makusanyo katika mkoa huo amesema bado kiwango kiko chini ikilinganishwa na rasilimali madini zinazopatikana katika mkoa huo ikiwemo chuma na makaa ya mawe na kuongeza kwamba, hadi sasa Mkoa wa Njombe umekusanya kiasi cha shilingi milioni 240 kati ya shilingi bilioni 1 uliyopangiwa kukusanya huku akitaja moja ya sababu ikiwa ni wamiliki kutozifanyia kazi leseni zao.

Pia, ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachimbaji wadogo katika mkoa huo kwa kufanya shughuli zao huku wakishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Madini pamoja na ofisi ya Mkoa wa Njombe suala ambalo limepelekea kutokuwepo kwa migogoro inayozuia maendeleo ya Sekta.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Njombe Alfred Luvanda, amemhakikishia Prof. Msanjila kuwa, wachimbaji mkoani humo wako tayari kimitaji ikiwemo kulipa kodi za serikali pindi itakapowapatia leseni za kuchimba madini, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Madini.

‘’ Kwanza tunashukuru sana kwa ujio wako, tunaamini kilio chetu kimefika sehemu sahihi.  Tunakuahidi tutachimba, tutalipa kodi za serikali na tutaipa serikali heshima,’’ amesema Luvanda.

Naye, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe Henry Mditi amewaeleza wachimbaji hao kuwa ofisi ya madini mkoani humo haitomuonea mtu yoyote na hivyo akawataka wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria.

Prof. Msanjila amekutana na wachimbaji hao Mei 13, 2021, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wachimbaji pamoja na watumishi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.


Share:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aongoza swala ya Eid al-Fitr kitaifa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya waumini wa madhehebu ya Kiislamu katika swala ya Eid Al-Fitr iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Swala hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini akiwemo Mufti wa Tanzania, Sheikh Abiubakar bin Zuberi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na makamu wake, Dkt. Philip Mpango kwa waumini hao, waziri mkuu amesema viongozi hao wanawatakia Waislamu na Watanzania wote nchini sikukuu njema.

Ametumia jukwaa hilo kuwahisi Waislamu kusherehekea siku kuu ya Eid al-fitr kwa kuiishi miiko ya dini hiyo.

Awali, akihutubia maelfu ya Waislamu waliofika katika ibada hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesisitiza umuhimu wa amani, upendo na kutosherehekea katika mazingira ya kupata dhambi.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza Kuu la Waislamu leo alasiri.


Share:

SHEIKH MAKUSANYA : WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU TUWATII VIONGOZI WETU..UWE UNAWAPENDA AMA HUWAPENDI

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya akitoa hotuba kwenye Swala ya Eid El Fitri katika uwanja wa Sabasaba mjini Shinyanga
Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Shinyanga wakiwa kwenye Swala ya Eid
Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Shinyanga wakipiga picha ya kumbukumbu na Sheikh wa Mkoa Ismail Makusanya watatu katikati
 **
Na Marco Maduhu, Shinyanga
Waumini wa dini ya Kiislamu hapa nchini, wametakiwa kuwatiii na kuwaheshimu viongozi wa kiserikali, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 14,2021 na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya, wakati akitoa hotuba kwenye swala ya Eid El Fitr iliyofanyika katika viwanja vya sabasaba Mjini Shinyanga.

Alisema maagizo ya kutii viongozi yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo ni vyema waumini hao wakafuata maagizo hayo, na kuwatiii viongozi wa nchi na kuwaheshimu, ili kujiongezea thawabu.

"Nawaomba waumini wa dini ya Kiislamu tuwatii viongozi wetu wa Serikali, uwe unawakubali ama kuwakataa, na hata kama huwapendi ama unawapenda, akiwamo Mkuu wetu wa Mkoa hapa Shinyanga Zainab Telack na kiongozi wetu wa nchi "Rais Samia",alisema Makusanya.

Pia aliwataka Waislamu kusheherekea Sikukuu ya Eid kwa kutoa sadaka wa yatima, wafungwa, wajane, pamoja na kufurahia na familia zao nyumbani na siyo kwenda kufanya mambo ya anasa.

Nao baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu akiwamo Twaha Habibu, alisema katika kusheherekea siku kuu hiyo ni vyema kila Muislamu akajiepusha na masuala ya anasa ikiwamo kunywa Pombe, ili kuepuka kuharibu mfungo wao kwa kuchuma dhambi.
Share:

HILAL SOUD : WAISLAMU WOTE WANAPASWA KUISHI KWA KUFUATA DINI...TUNAENDELEA NA UJENZI WA MISIKITI

Mkurugenzi Mkuu wa Soud Group Company, Hilal Soud

Na Annastazia Paul - Shinyanga
Waumini wa dini ya Kiislamu Mkoani Shinyanga wametakiwa kuishi kwa kufuata misingi ya dini, kwani ni ufunguo wa kutafuta usalama, maisha na inaleta baraka katika maisha yao.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Mei 14 2021, na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Soud Group (Soud Company Group) Hilal Soud wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Shinyanga katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Fitr, ambapo amesema kuwa Waislamu wote wanapaswa kuishi kwa kufuata dini.

“Waislamu wote akina baba, akina mama na watoto, ninawaasa kila mmoja afuate dini, kwani dini ni ufunguo wa maisha yake, dini ni ufunguo wa kutafuta usalama, dini inaleta baraka na ndiyo maana unakuta dini imepewa kipaumbele na huwa haiingiliwi na msimamo wa dini unaleta kheri”,amesema.

Amewaomba watu wenye uwezo wa kusimamia mambo ya dini waendelee kujitoa ili yasonge mbele.

“Waliopewa na Mungu, kwa mkono wa kulia nao watoe ili mambo ya dini yasonge mbele .Kwa waumini nawataka waendelee ili waweze nao kuwa wengi, kadri tunavyowasogezea majengo ya dini basi waumini waweze kuendelea na watatupa uwezo wa kufikiria kuwa kuna usalama zaidi”,amesema Hilal.

Hilal Soud ambaye pia ni Mjumbe wa Taasisi ya Kiibadhi ya Istiqaama Muslim Community of Tanzania inayojihusisha na masuala mbalimbali ikiwemo uratibu wa miradi ya kusaidia uislamu, kutoa elimu ya dini ya kiislamu, kujenga na kusimamia madrasa,misikiti shule na vituo vya kulelea yatima, amesema wanaendelea na ujenzi wa misikiti katika maeneo ya Kenyata na Ushirika Mjini Shinyanga.

Amesema kuwa wana mpango wa kusaidia watu mbalimbali hasa waamini wa dini ya kiislamu kupitia miradi ambayo itakuwa ikifanyika katika misikiti hiyo.

“Kujengwa kwa msikiti katika eneo la Kenyatta tunataka tuunganishe na madarasa ya akina mama, kwa sababu kubwa nyingi, sababu ya kwanza akina mama ni watu ambao wakipata elimu maana yake watoto wamefikiwa, jambo la pili ni watu ambao wanazingatia dini sana na pia Shinyanga tumeona akina mama wengi bado hawajaelewa dini inavyotakiwa, Msikiti huo unajengwa na familia ya Hilal Soud ambayo imeamua kusaidia jambo hilo litakalowanufaisha Waislam hasa katika Mkoa wetu wa Shinyanga”, ameeleza Hilal Soud.

Amesema kuwa msikiti uliopo katika eneo la Ushirika mjini Shinyanga unajengwa kwa michango ya Waislam mbalimbali walioamua kujitoa kwa usimamizi wa taasisi Kongwe ya Istiqaama Muslim Community of Tanzania na kwamba kutakuwa na madarasa pamoja na kituo cha kulelea watoto yatima.

“Huo Msikiti wa Ushirika unajengwa lakini kuna ndugu zangu wengi ambao wanausimamia ambao wapo karibu na sisi na pili Jumuiya itakuwa nayo inachanga katika jengo hilo na pia msikiti huo unajengwa na wasali waumini wa kiislam kwa kiasi kinachowezekana, pia tunatajia kutakuwa na madarasa mchanganyiko na kituo cha kulelea watoto yatima”, ameongeza.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger