Sunday 7 April 2024

WAKENYA WAIKUBALI NGURUWE PROJECT KATIKA KIJIJI CHA NGURUWE DODOMA

...
DODOMA;  Idadi ya wawekezaji wa Kigeni wenye dhamira ya kufanya uwekezaji katika kijiji cha Nguruwe imezidi kuongezeka katika kijiji cha Mayamaya wilayani Bahi Mkoani Dodoma baada ya wafugaji kutoka nchini Kenya wakiongozwa na Paulo Kimanya kufika kitongoji cha Zamahero kujifunza juu ya ufugaji wa kisasa wa Nguruwe na kisha kuonyesha nia ya kuwekeza katika mradi huo uliyochipuka kwa kasi miezi michache iliyopita.

Wakizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi na kisha kuridhishwa na mazingira ya utekelezaji wa Nguruwe Project wenye nguruwe zaidi ya 800 wawekezaji kutoka nchini Kenya akiwemo Kimanyi wamesema wana kila sababu ya kuwekeza katika kijiji cha Nguruwe kwasababu ufugaji wake umezingatia sheria za mazingira na haki za wanyama hivyo wana amini watakwenda kunufaika na kitakachowekezwa.

"Sisi tumekuja hapa kijiji cha Nguruwe kwasababu tumeona taarifa za mradi huu na kwakuwa ulaji wa nyama ya nguruwe unazidi kushika kasi na mikataba haina shida kwa wawekezaji hivyo tunakwenda kuandaa fungu ili kuja kufanya uwekezaji",alisema Paul Kimanyi.

Awali mwanzilishi wa Kijiji cha Nguruwe katika kitongoji cha Namahero ambaye pia ni mkurugenzi wa Kijiji cha Nguruwe Project Simon Mkondya amesema wazo la kuanzisha mradi huo lilikuja baada ya kuona uhitaji wa kitoweo hicho unaongezeka na kwamba hadi sasa kuna nguruwe zaidi ya 800 wakubwa na wadogo waliozaliwa siku chache zilizopita.

Mkondya amesema shauku yake kubwa ni kuona kijiji hicho kinakuja kuwa kusanyiko kubwa la Nguruwe dunia na kuchangia pato kubwa la taifa kupitia mauzo ya mifugo na tozo ya utalii ambapo mtalii wa ndani atapaswa kulipa dola moja na mtalii wa nje kulipa dola 10 kutembelea na kisha kujionea maajabu ya kijiji hicho hivyo kila uchwao wawekezaji wanaongezeka na kutengeneza fedha .

Hadi sasa kijiji cha Nguruwe kimepokea watalii zaidi ya 1400 wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Venezuela,Colombia,China,Ufaransa,Kenya na mataifa mengine mengi ambao wamekuwa chachu kubwa ya kuinua uchumi wa kijiji cha Mayamaya kupitia biashara ndogondogo zinazofanyika hapo.

"Tumetengeza mfumo wa Rent to Own ambao mtu anawekeza fedha yake,kwa mfano laki saba anapata faida mara tatu katika kipindi cha miezi sita na muwekezaji atakuwa analipwa kila siku hadi miezi sita kuisha",alisema Mkondya.

Akieleza aina za nguruwe wanaofugwa katika kijiji hicho Muwekezaji huyo amesema ni aina tatu akiwemo Large White mwenye mafuta Mengi ambae hunenepa sana na hupendwa sana akina dada, Duroc ambaye tabia yake ni kuwa na nyama nyingi na mafuta machache pamoja na Landrace.

Ukiachana na wakenya ,kijiji cha Nguruwe kimetembelewa pia na viongozi wa serikali za vijiji vya karibu na mradi huo akiwemo Joseph Mchami mwenyekiti wa mtaa wa Sekondari kata ya Makutupora ambaye anasema amelazimika kufika ili kujionea uwekezaji uliofanyika na kisha kumuomba muwekezaji kuona namna ya kwenda kuwekeza pia katika mtaa wao.

Wengine ni Fadhili Hawadhi Juma na Mohamed Choku maarufu Muarabu ambao baada ya kukagua mazingira ya mradi wameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wake huku pia wakisema faida kubwa ipo kwenye kutengeneza ajira za vijana na kuinua uchumi wa kijiji cha Namahero.

Katika hatua nyingine Mradi huo umetembelewa na watumishi wa umma akiwemo Atupele Mwakalinga ambae anasema wamejifunza hatua zote za ufugaji wa nguruwe,changamoto za ufugaji na Mazingira ya Mradi na kisha kuondoka na imani kubwa ya kuja kuwekeza katika kijiji cha Nguruwe.

"Tumekuja hapa kujifunza kila kitu kuhusu nguruwe hivyo wanaondoka wakiwa hawana shaka yoyote ya kuja kuwekeza hivyo wanakwenda kujipanga na kurudi Namahero" ,alisema Mwakalinga.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger