Diwani wa kata ya mjini Mathew Ngalimanayo akizungumza na wajumbe wa kamati ya Siasa wakati alipokua akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2025/2030Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma
Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/2030, Kata ya Mjini katika Manispaa ya Songea imeendelea kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo huku ikikabiliwa na changamoto zinazogusa miundombinu, elimu, mazingira, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na huduma za kijamii.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani hiyo kwa mwaka 2025/2026 katika mkutano uliofanyika Septemba 28, 2026 katika Ukumbi wa Kata ya Mjini, Diwani wa Kata hiyo, Mathew Ngalimanayo, amesema baadhi ya changamoto zimeanza kufanyiwa kazi huku nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali za kutatuliwa.
Miongoni mwa maeneo yaliyotekelezwa ni ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Majimaji kwa gharama ya Sh milioni 96, uchimbaji wa kisima katika Shule ya Msingi Mfaranyaki, uwekaji wa taa za barabarani, ujenzi wa mitaro na maboresho ya barabara, ikiwemo CCM/Mahenge.
Akieleza namna kata hiyo inavyopokea na kushughulikia changamoto za wananchi, Ngalimanayo amesema baadhi ya mahitaji yaliyowasilishwa ni ujenzi wa vivuko, ukamilishaji wa jengo la mabweni, ujenzi wa mitaro katika barabara ya SOUWASA/Mashujaa pamoja na mtaro imara katika eneo la Makumbusho/Mahenge.
Amesema barabara ya SOUWASA/Mashujaa imepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku hatua zikiendelea kuchukuliwa katika maeneo mengine.
Katika elimu, amesema uzio umejengwa katika Shule ya Wasichana Songea kwa Sh milioni 20.5 kupitia mapato ya ndani ya Manispaa ya Songea, huku fedha zikipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa matundu matatu ya vyoo vya wanafunzi wenye ulemavu.
Pia amesema kata inaendelea kuhamasisha mpango wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto unaogusa lishe, afya, ujifunzaji wa awali, malezi yenye mwitikio na nidhamu.
Mbali na miundombinu na elimu, Ngalimanayo amesema kata imeendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi, ambapo jumla ya vikundi 103 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vimesajiliwa na vikundi saba vimefanikiwa kupata fedha taslimu kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali.
Hata hivyo, changamoto ya urejeshaji wa mikopo imeendelea kujitokeza baada ya vikundi 42 kutorejesha fedha walizokopa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 82.
Mwenyekiti wa Kata ya Mjini, Lothal Nikata, amesisitiza umuhimu wa kurejesha fedha hizo ili wananchi wengine waweze kunufaika, akieleza pia kuwa baadhi ya akina mama na vijana waliopata mikopo ya pikipiki wamewahi kunyang’anywa pikipiki hizo kutokana na kushindwa kurejesha fedha kwa wakati.
Nikata amewataka pia wenyeviti wa mitaa kusoma taarifa za mapato na matumizi na kutimiza wajibu wao katika kusimamia maendeleo ya maeneo yao.
Katika eneo la michezo, sanaa na utamaduni, Ngalimanayo amesema kata imefanikiwa kuwezesha kufanyika kwa bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililogharimu Sh 520,000, ambapo mshindi wa kwanza alikabidhiwa zawadi ya mbuzi, huku washindi wa pili na wa tatu wakipata zawadi za fedha taslimu.
Amesema shughuli hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushiriki wa vijana katika michezo na kuendeleza mshikamano wa wananchi.
Aidha, katika kuimarisha chama na jumuiya zake, amesema wameendelea kujenga mahusiano na wanachama na kushirikiana nao katika kufanikisha mipango ya chama na jumuiya zake, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Akihitimisha taarifa hiyo, Ngalimanayo amesema anaendelea kuyabeba na kuyafanyia kazi maoni na changamoto zinazowasilishwa na wananchi, akiahidi kuwahudumia wananchi wote kwa usawa. “Naendelea kuyabeba yale yote mnayoniambia, nitawahudumia wananchi wote kwa usawa. Changamoto zozote za kata yetu mzilete kwenye mikutano ya hadhara,” amesema.
Pia amewaomba wajumbe wa kamati na wananchi kuendelea kumpa ushirikiano, huku akisisitiza kuwa changamoto za kimaadili na nidhamu zinahitaji ushirikiano wa familia na jamii. “Tukae na watoto wetu, tuwaelekeze nini maana ya elimu. Hatuwezi kuacha nguvu za wananchi zipotee,” amesema, akisisitiza kuwa maendeleo ya Kata ya Mjini yanahitaji ushiriki wa pamoja wa viongozi, wazazi, vijana, wanachama na wananchi wote.


0 comments:
Post a Comment