Afisa msaidizi wa mahusiano TANESCO Mkoa wa Ruvuma bi Emma Ulendo akiwa katika kijiji cha Liula kata ya Matimila wakati walipotembelea kijiji hicho kutoa elimu kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umeme na kujikinga na mvua kubwa ya El Niño 
Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limeendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Liula, Kata ya Matimila, Halmashauri ya Songea Vijijini, kuhusu namna ya kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa za El Niño, utunzaji wa miundombinu ya umeme, namna ya kulipia huduma hiyo, kupambana na wizi wa vifaa vya umeme pamoja na kuepuka uchomaji moto holela katika maeneo yenye nguzo za umeme.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo, Afisa Msaidizi wa mahusiano TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Emma Ulendo, amesema wananchi wanapaswa kuwa makini wakati wa mvua kubwa, hasa pale nguzo za umeme zinapoanguka kwenye maji, na kutoa taarifa haraka TANESCO badala ya kusogelea eneo hilo, kwa kuwa maji yanaweza kuwa na umeme na kusababisha madhara hata bila mtu kugusa waya au nguzo.
Ulendo amesema elimu hiyo pia imelenga kuwaelimisha wananchi kuhusu mradi wa umeme unaotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwemo mchakato wa kuchukua fomu hadi mteja anapopata huduma ya umeme.
Aidha, amesema TANESCO inawasisitiza wananchi kutunza miundombinu ya umeme iliyofikishwa katika maeneo yao, hususan kipindi cha kusafisha mashamba na kuchoma moto, kwa kuhakikisha moto haukaribii maeneo yenye nguzo za umeme.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kununua na kutumia vifaa bora vya umeme visivyo feki, pamoja na kuhakikisha wanafuata taratibu sahihi za matumizi na malipo ya huduma hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Matimila, Menace Cosmas Komba, amesema kata hiyo ina vijiji sita na vitongoji 37, huku akieleza kuwa mkutano huo umefanyika mahsusi kwa TANESCO kutoa elimu kuhusu matumizi bora na salama ya umeme.
Komba amesema utekelezaji wa ahadi za Serikali umewezesha takribani asilimia 98 ya vitongoji vya kata hiyo kupata umeme, huku vitongoji vinne vikibaki kukamilisha huduma hiyo, ambapo laini kubwa na ndogo tayari zimepita na transfoma tatu zimewashwa.
Amesema wananchi wanachosubiri ni kupata elimu ya matumizi na malipo ya umeme ili TANESCO iweze kuwasha huduma hiyo kwa ajili ya matumizi yao.
Aidha, amesema uwepo wa umeme umeleta shughuli mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo saluni, biashara na vijana kutumia mashine za kuchomelea kutengeneza magril na bidhaa nyingine kwa ajili ya kuuza.
Komba amesema pamoja na manufaa hayo, wananchi wamepewa wajibu wa kulinda miundombinu ya umeme, hasa katika kipindi cha kiangazi, ambapo wamekatazwa kuchoma moto ovyo kwa kuwa unaweza kuunguza nguzo na kusababisha ajali pamoja na kukatika kwa umeme.
Pia amewataka wananchi kushirikiana katika kuzuia wizi wa mafuta ya transfoma na nyaya za umeme.
Amesema wananchi wameanza kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa kutambua kuwa wanailinda huduma inayowanufaisha.
Akizungumzia maendeleo ya Kata ya Matimila, Komba amesema eneo hilo limebadilika ikilinganishwa na zamani, likiwa na zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya cha Matimila, ambacho kimepata vifaa tiba, huku wakisubiri madaktari kuanza kutoa huduma za upasuaji.
Pia amesema kituo hicho kina mashine ya dharura ya kuzalisha umeme endapo huduma ya umeme itakatika, huku akieleza kuwa barabara mbalimbali zimefunguliwa na madaraja kujengwa, ikiwemo barabara kutoka Mletele hadi Mkongo katika Halmashauri ya Namtumbo na kutoka Matimila B hadi Kikunja pamoja na barabara ya Matimila B kuelekea Namtumbo kupitia Limamu.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Liula, akiwemo Dickson Thadeo Komba, Hamis Abbas na Moses Luambano, wamewahimiza wananchi kuwa makini katika kulinda miradi na miundombinu ya umeme kwa kuwa ni mali inayowanufaisha wao wenyewe.
Wamesema Serikali imewapatia huduma hiyo na jukumu la wananchi ni kuhakikisha inalindwa ili iendelee kuwafikia wananchi wengine katika vijiji na mikoa mingine.
Wamesisitiza kuwa mtu yeyote anayeonekana katika maeneo yenye miundombinu ya umeme na kufanya shughuli zisizoeleweka anapaswa kuhojiwa na taarifa kutolewa kwa mamlaka husika.
Aidha, wananchi hao wameomba kufungiwa mashine zinazotumia umeme kwa ajili ya kusaga nafaka ili waweze kupata huduma hiyo katika kijiji chao na kuachana na matumizi ya mashine zinazotumia mafuta.


0 comments:
Post a Comment