
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waandishi wa habari za mazingira nchini wametakiwa kuandika kwa kina habari za uchunguzi kuhusu shughuli na matukio mbalimbali yanayochangia kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa lengo la kuisaidia jamii kuchukua hatua na kulinda mazingira.
Wito huo umetolewa na Mhariri Mwandamizi wa Habari za Mazingira, Deodatus Mfugale, wakati akitoa mada kuhusu uandishi wa habari za uchunguzi wa mazingira katika mafunzo ya wanahabari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Kati yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mfugale amesema maeneo mbalimbali nchini yanaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji miti, upanuzi wa mashamba katika maeneo yaliyohifadhiwa, uvamizi wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira, uvamizi wa maeneo ya malisho pamoja na shughuli za uchimbaji madini zisizozingatia kikamilifu masuala ya mazingira.
Amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuibua changamoto hizo na kusaidia jamii kuelewa madhara yake, huku akiwataka kutumia takwimu sahihi, sheria na vyanzo vya kuaminika ili kuibua masuala ya uwajibikaji.
“Waandishi, nendeni mkaandike habari za uchunguzi kusaidia jamii ili kuifanya dunia kuendelea kuwa salama. Lakini muandike kwa usahihi na mjumuisha sauti za wananchi wanaoathirika,” amesema Mfugale.
Amesema uandishi wa habari za mazingira haupaswi kuishia katika kuripoti matukio pekee, bali unapaswa kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza chanzo cha tatizo, wahusika, madhara yanayotokea na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Mussa Juma, amesema mwandishi wa habari za mazingira anapaswa kuandika kwa usahihi na uhuru, kuelewa kwa kina jambo analolifanyia kazi na kuhakikisha anashirikisha sauti za makundi mbalimbali katika jamii.
Juma amesema makundi hayo yanapaswa kujumuisha wanawake, vijana na jamii zinazoathirika moja kwa moja na changamoto za kimazingira, huku akisisitiza umuhimu wa uandishi unaochochea uwajibikaji na kulinda maslahi ya umma.
Amesema wanahabari wanapaswa kuongeza utafiti kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini, zikiwemo athari zinazohusiana na ongezeko la joto duniani, ukame, mafuriko, kupungua kwa uzalishaji wa chakula na uharibifu wa mifumo ya ikolojia.
Naye Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Halima Sonda, ametoa wito wa kuhakikisha wanahabari wanawake wanapewa fursa sawa na wenzao wanaume katika kufanya na kuchapisha habari za uchunguzi, hususan zinazohusu mazingira.
Wakili Sonda amesema bado kuna changamoto ya udhalilishaji wa wanawake kwenye mitandao ya kijamii pamoja na mifumo dume katika jamii, hali ambayo inaweza kuwazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika uandishi wa habari za uchunguzi.
Amesema changamoto hizo zinapaswa kupingwa huku wanahabari wanawake wakitakiwa kufahamu sheria na taratibu zinazolinda haki zao dhidi ya ukatili na udhalilishaji.
Mafunzo hayo yameandaliwa na THRDC kwa kushirikiana na MAIPAC, kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa lengo la kuwawezesha wanahabari kuimarisha ujuzi wa kuandika habari za mazingira, kuibua changamoto na kuchangia uwajibikaji katika usimamizi wa mazingira.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wanahabari kutoka Dodoma, Singida, Mbeya, Iringa na Morogoro, na ni sehemu ya mfululizo wa mafunzo yanayotolewa kwa wanahabari nchini kupitia mradi unaolenga kuwawezesha waandishi wa habari za mazingira kuimarisha uwezo wao na kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kabla ya mafunzo ya Kanda ya Kati, mafunzo kama hayo tayari yametolewa katika Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.






0 comments:
Post a Comment