Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika semina ya siku moja ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu akichangia hoja kwenye semina ya siku moja ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wale wanaotoka halmashauri ambazo Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaanza iliyofanyika mkoani Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Malisili na Utalii Ally Juma Makoa akisisitiza jambo wakati wa semina ya siku moja ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga Cosato Chumi akichangia hoja katika semina ya siku moja ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wale wanaotoka halmashauri zinazopitiwa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza semina ya siku moja ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wale wanaotoka halmashauri zinazopitiwa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Wabunge wakiwa kwenye semina ya siku moja kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Januari 2023.
Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Joseph Shewiyo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa LTIP kwa wabunge tarehe 21 Januari 2023 jijini Dodoma (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
**************************
Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) inatarajia kutoa Hati Milki za Ardhi milioni moja katika maeneo ya mijini pamoja na Hati Miliki za Kimila laki tano kwenye maeneo ya vijijini.
Aidha, kwa yale maeneo ambayo upangaji wake utaleta ugumu kutokana na ujenzi holela maeneo hayo utambuzi wake utachukuliwa kama ulivyo na Mradi wa LTIP utatoa Leseni za Makazi milioni moja.
Hayo yamebainishwa tarehe 21 Januari 2023 na Mratibu wa mradi wa LTIP Joseph Shewiyo wakati wa semina ya siku moja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi iliyofanyika jijini Dodoma.
Alisema, kazi ya utoaji hati miliki kwenye maeneo ya mijini itafanyika kwa kutumia watumishi wa serikali kwa asilimia 20 huku asilimia 80 iliyobaki ikifanywa na makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi ya kupanga na kupima.
‘’Kazi ya mfano (Pilot) imeanza jiji la Dodoma ambapo kata tatu za Mbabala (Bihawana), Nghong’ona (Mapinduzi) na kata ya Mpunguzi (Mkwawa) zimechaguliwa. Aidha, halmashauri nane za Dodoma Jiji, Chalinze, Mafinga, Rungwe, Nzega, Tarime, Korogwe na Kigoma Ujiji ndizo zitakazoanza kwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mradi’ alisema Shewiyo
Akielezea upande wa Hati Milki za Kimila, Mratibu huyo wa LTIP alisema, kazi hiyo itafanywa na watumishi wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali na kubainisha kuwa kazi itakayofanyika ni pamoja na kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 250 na utoaji hati milki laki tano za kimila.
Aliwaeleza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii iliyojumisha pia Wabunge wanaotoka halmashauri ambazo mradi huo utaanza kwa mwaka wa kwanza kuwa, mradi wa LTIP utekelezaji wake utakuwa na shughuli mbalimbali na kuzitaja kuwa ni pamoja na utoaji Hati, maandalizi ya ramani za msingi, uboreshaji mfumo wa ILMIS, Alama za msingi na mifumo ya uthamini sambamba na ujenzi wa ofisi za ardhi za mikoa 25.
‘’Kazi nyingine zitakazofanyika kupitia mradi wa LTIP ni ukarabati wa ofisi za ardhi kwenye halmashauri 41, uboreshaji ofisi za Mabaraza ya Ardhi katika halmashauri 41, ukarabati wa masijala za ardhi za vijiji 250, kuwajengea uwezo watumishi pamoja na uratibu wa masuala ya kijamii na mazingira’’. Alisema Shewiyo.
Kwa upande wao, Wabunge wametaka utekelezaji Mradi huo wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini uende sambamba na utoaji elimu kwa wananchi hasa wanawake pamoja na watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya mitaa ili kuleta ufanisi zaidi katika mradi.
Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini mkoani Iringa ameshauri utekelezaji mradi huo uangalie pia maeneo ya viwanda na kubainisha kuwa sekta hiyo ni muhimu na imeendelea kukua kwa kasi kwenye maeneo mbalimbali.
Mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi ulio chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na utekelezaji wake umeanza Mei, 2022 na unatarajia kukamilika May 2027 (Miaka 5).
Lengo la mradi wa LTIP ni kuboresha ufanisi katika utawala wa ardhi na kuongeza usalama wa milki kwenye maeneo ya mradi. Lengo hilo linaenda sambamba na kuongeza idadi ya miamala itokanayo na nyaraka za umiliki, kupunguza muda unaotumika kupata nyaraka za milki, kuongeza uelewa wa usalama wa milki kwa kuzingatia jinsia, kuongeza idadi ya watanzania wanaomiliki nyaraka za umiliki pamoja na kuongeza ufanisi utakaofanya wamiliki kuridhika na mchakato wa uandaaji nyaraka za umiliki.
0 comments:
Post a Comment