Na Mwandishi wetu,Iramba-Singida.
Wilaya ya Iramba mkoani Singida imejipanga kuanza mashindano ya mpira wa miguu ili kuwakutanisha vijana pamoja na kuimarisha afya zao, kutambua vipaji vyao na kuviendeleza.
Mashindano hayo yanaratibiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda huku yakiwa yanatarajiwa kuanza mapema mara baada ya msimu wa kilimo kumalizika.
Mwenda amebainisha hayo jana tarehe 13 Januari 2023 wakati akizingumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya WazoHuru Media Group Limited Mathias Canal aliyemtembelea ofisini kwake Mjini Kiomboi,Singida.
Amesema kuwa Ligi ya mpira wa miguu ambayo ina lengo la kuimarisha sekta ya michezo Wilayani hapo na kuwakutanisha vijana itasaidia kutengeneza mahusiano imara na madhubuti katika msingi wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Wilaya kwa ujumla wake.
"Nawasihi wananchi na wadhamini mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha dhamira hii katika kuimarisha sekta ya michezo na kufanikisha kuanza na kumalizika kwa mashindano hayo,michezo ni furaha,amani na upendo,"amesisitiza.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya WazoHuru Media Group Limited Mathias Canal amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kujipanga kuanzisha mashindano hayo ambayo yatakuwa chachu ya kuitangaza Wilaya ya Iramba na sekta ya uwekezaji.
Amesema kuwa Wilaya ya Iramba ina maeneo mengi mazuri na ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya Kilimo, Elimu, Mifugo na Uvuvi ikiwa ni pamoja na sekta ya Viwanda.
0 comments:
Post a Comment