Jeshi la Ulinzi nchini Uganda limemkamata pasta na maafisa watatu wa polisi kufuatia kisa cha mwanamke mmoja raia wa kigeni kudaiwa kubakwa na kutapeliwa pesa zake.
Kukamatwa kwa mchungaji huyo kunajiri baada ya kituo cha NTV-Uganda wikendi iliyopita kufanya mahojiano na mwathiriwa.
Katika mahojiano hayo, mwathiriwa kwa jina Anda alifichua uyahawani ambao alitendewa na nabii Joseph Collins Twahirwa muda mfupi baada ya kuwasili nchini Uganda mnamo Disemba 11, 2022. Twahirwa alikuwa amemwalika Anda kwenda nchini Uganda kwa likizo.
Punde alipowasili nyumbani kwa pasta huyo, inasemekana alimpokonya pasipoti yake na kumwibia KSh37, 203 na €400(KSh53,698) kabla ya kumbaka.
Raia huyo wa Latvia mwenye umri wa miaka 36, alisema Twahirwa alimwambia alitaka kupata mtoto na kisha alimsukuma kitandani na kumbaka usiku wa Disemba 11, 2022.
Anda pia alisimulia masaibu aliyopitia alipojaribu kwenda kupiga ripoti katika Kituo cha Polisi cha Jinja Road na, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID).
Katika Kituo cha Polisi cha Jinja Road, maafisa walimtaka mtalii huyo awanunulie mafuta ya gari lao au ashiriki ngono nao. Polisi hao pia waliungana na wafuasi wa Twahirwa kumtesa raia huyo wa kigeni.
Anda aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alipokonywa simu yake na mawasiliano yote aliyokuwa nayo na Twahirwa kwenye mitandao ya kijamii yalifutwa ili kujaribu kuharibu ushahidi wa uhusiano wao.
Maafisa wa kituo hicho pia walidaiwa kumvua viatu kwa nguvu miguuni na kumtandika kabla ya kumtupa ndani ya seli.
Baadaye aliachiliwa na kuamriwa kufuta kesi dhidi ya Twahirwa.
Alipokimbia kwa CID, maafisa hao walimwambia Anda kwamba anacheza na mwanaume mwenye uhusiano na watu wenye ushawishi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa CID alisema kuwa maafisa hao watatu walikamatwa Jumapili, Januari 15, na wanatazamiwa kufikishwa kortini.
Twahirwa ambaye alikuwa ameachiliwa kwa bondi wakati taarifa hiyo ilipeperushwa, pia anashikiliwa na polisi na atafikishwa kortini ndani ya saa 48.
Claire Nabakka, ambaye ni naibu msemaji wa polisi, alithibitisha kwamba dhamana ya Twahirwa ilifutwa na kwamba pasta huyo wa Epikaizo Ministries International yuko chini ya ulinzi wa Jeshi.
Polisi pia walitoa wito kwa waathiriwa wa pasta huyo pia kujitokeza na kuwasilisha ripoti kwa CID ili kusaidia katika uchunguzi zaidi.
Kisa cha Anda kimeharibu sifa ya maafisa wa polisi nchini humo pamoja na wachungaji wa kipentekoste.
Chanzo - TUKO NEWS
0 comments:
Post a Comment