Mwanamke anayefahamika kwa jina la Scholastica Peter mwenye umri wa Miaka 28 mkazi wa mtaa wa Bugwandege kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, amewajeruhi watoto wake wawili kwa kuwachoma moto kwenye mikono kwa kile alichodai alikuwa akiwaonya baada ya kukomba mboga.
Waandishi wa habari wamefika eneo la tukio na kuzungumza na Mama huyo ambaye amekiri kuwachoma moto watoto hao, akisema alifanya hivyo kama hatua ya kuwaonya, kwa sababu wana tabia ya udokozi wa mboga.
“Hawa watoto wana tabia ya udokozi ile siku nilipika mboga tukala usiku tukaibakiza asubuhi nikatoka nikaenda kutembeza mboga nikakuta wameikomba mboga yote ilikuwa ni mboga ya dagaa nilichanganya na nyanya ntole/chungu sasa nilikuwaga nawakanya hawasikii hiyo siku nilishikwa na hasira mara ya kwanza niliwapiga na ya pili hii mara ya tatu kulikuwepo jiko lilikuwa na moto na kulikuwepo na jiko ambalo nilikuwaga natolea mkaa baada ya kuwapiga nikasogeza hilo jiko ndiyo nikawa nawababua na kijiko”,amesema Scholastica.
Akizungumzia tukio hilo mtendaji wa kata ya Ibinzamata Victor Kajuna amesema kuwa taarifa hizo amezipata leo kutoka kwa wananchi waliochukua jukumu la kuwabeba watoto na kuwapeleka katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata.
“Leo majira ya saa nne asubuhi niliwapokea wananchi kutoka mtaa wa Bugwandege walifika wakiwa wameongozana na mama mmoja pamoja na watoto wake wawili wakaeleza kuwa baada ya watoto hao kuwaona wanaendelea kuishi bila msaada”,amesema.
Diwani wa kata ya Ibinzamata Mheshimiwa Ezekiel Sabo amekemea kutokea kwa tukio hilo huku akiwaomba wananchi wa kata hiyo kuacha tabia ya kutoa adhabu kali kwa watoto wao,kwani kwa kufanya hivyo ni ukatili.
“Taarifa hii ya watoto kuchomwa moto nimeipokea kwa masikitiko makubwa sana lakini nakemea swala hili lisijitokeze tena katika kata ya Ibinzamata kwa sababu jamii ikifikia hapo basi tutakuwa tumefika pabaya sana na niviombe vyombo vya serikali vifuatilie ili ukatili huu usijirudie tena”, amesema Sabo.
Kwa upande wake Afisa elimu wa kata ya Ibinzamata Mackrine Shija amewaomba wazazi na walezi kuacha tabia ya kutoa adhabu kubwa kwa watoto.
Msaidizi wa kisheria kutoka Community Edification Organization kata ya Ibinzamata Robert Said amesema kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.
0 comments:
Post a Comment