Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa rasmi mradi unaoshughulikia masuala ya afya ya uzazi kwa vijana na wanawake unaojulikana kama Reproductive Equity Strategy in Tanzania (REST) unaoendeshwa na shirika lisilo la Kiserikali la Deutsche Stiftung Weltbevolkerung (DSW) - Tanzania ambao utafanya kazi kwenye Wilaya tatu za Mkoa ikiwa ni pamoja na Dodoma mjini, Bahi na Mpwapwa.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki katika uzinduzi wa mradi unaoshughulikia masuala ya afya ya uzazi kwa vijana na wanawake. Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
****************************
Mkoa wa Dodoma umezindua rasmi mradi unaoshughulikia masuala ya afya ya uzazi kwa vijana na wanawake unaojulikana kama Reproductive Equity Strategy in Tanzania (REST) unaoendeshwa na shirika lisilo la Kiserikali la Deutsche Stiftung Weltbevolkerung (DSW) - Tanzania ambao utafanya kazi kwenye Wilaya tatu za Mkoa ikiwa ni pamoja na Dodoma mjini, Bahi na Mpwapwa.
Akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kipaumbele katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu yake ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora ya afya.
“Matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yanaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya hospitali 676, vituo vya afya 1,466 na zahanati 7, 965. Tanzania Bara pekee ina hospitali 662, vituo vya afya 1,430 na zahanati 7,680 na mkoa wetu wa Dodoma una vituo vya afya 69 na zahanati 402. Hivyo ni muhimu sana kuendelea kuhamasisha wananchi hususan wakina mama wajawazito kutumia vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma, mpango wa Serikali ni kutokomeza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ifikapo mwaka 2025” Amesema Mhe. Senyamule.
“Nitoe rai, mkafanye kazi kwa ufanisi mkubwa maana tunataka kila unachokifanya Dodoma, kifanyike kwa ufanisi kwani tunakwenda kuifaharisha Dodoma kwa mradi huu” Ameongeza Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la DSW Bw. Peter Owaga, amesema “Mradi huu unatekelezwa kwenye mikoa minne ya Tanzania ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza kwa kushirikiana na mashirika 11 yasiyo ya Kiserikali. Kwa mkoa wa Dodoma unatekelezwa katika Wilaya tatu ikiwemo Dodoma mjini, Bahi na Mpwapwa chini ya mashirika ya Dodoma Youth Development Organization (DOYODO), Women Wake Up (WOWAP) na Family Engage for Action Foundation (FAEAF) wakiongozwa na Shirika la DSW Tanzania.
Lengo la mradi huu ni kusaidia wanawake na wasichana kupata na kutumia huduma za afya ikiwemo afya ya uzazi ili kuleta ustawi wao na kuweza kutimiza matarajio na malengo ya maisha yao. Mradi huu pia utasaidia utekelezaji wa sera na miongozo mbalimbali ya afya ya uzazi ikiwemo kupinga unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Baadhi ya kazi za Mradi huu ni pamoja na kutoa mafunzo kwa Watoa Huduma wa Afya kuhusu masuala ya Afya ya Uzazi ikiwamo utoaji wa huduma rafiki kwa Vijana na Jinsia, utoaji wa Mafunzo ya Afya ya Uzazi na Stadi za Maisha kwa Vijana Balehe katika Shule za Sekondari, Vyuo na walioko nje ya mfumo rasmi wa shule, kutoa mafunzo kwa Vyombo vya Habari kuhusiana na Masuala ya Afya ya uzazi na Jinsia katika kusaidia kutoa elimu kwa jamii, kutumia njia za ubunifu ikiwamo michezo, Sanaa na vikaragosi katika kuelimisha jamii.
0 comments:
Post a Comment