NI
ujambazi wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kuibuka na
wizi unaofanywa na majambazi katika maeneo mbalimbali nchini.Hatua
hiyo inatokana na majambazi hao kuibuka na mbinu mpya kila kukicha
katika matukio mbalimbali ambayo sasa yamekuwa yakishika kasi.
Mbali na mbinu ya
kutumia pikipiki, majambazi hayo pia huvamia vibanda vya kutoa huduma za
fedha, kuiba magari na hata wakati mwingine kuua.
Katika hali iliyovuta
hisia za watu wengi, juzi usiku majambazi yalifunga mtaa kwa saa mbili
na kupora fedha kwa watoa huduma ya fedha kwa njia ya simu katika eneo
la Tabata jijini Dar es Salaam.
Mbali na maduka, watu
wengine waliokuwa nje nao pia waliporwa simu na fedha. Hata hivyo
thamani ya fedha na vitu vilivyoporwa havikujulikana mara moja.
Tukio hilo lililoshtua
wakazi wengi wa mitaa ya Kimanga na Kisukuru wilayani Ilala, Dar es
Salaam, ni la pili kutokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Awali mwezi uliopita,
majambazi wenye silaha walimuua kwa risasi askari wa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na baadaye kumpora fedha Sh milioni tano, nje ya geti
la nyumbani kwake Mtaa wa Kimanga, saa tano asubuhi.
Tukio la juzi lilitokea
katika moja ya maduka yaliyoko pembezoni mwa kituo cha daladala cha
Jiandae kilichopo Tabata Kimanga, ambako majambazi wanaokadiriwa kuwa
zaidi ya wanne yaliingia dukani na kuwaamuru wafanyakazi kutoa fedha
zote za mauzo ya siku, huku wakiwatishia kwa mapanga na bastola.
Mmoja wa wafanyakazi wa kike katika maduka hayo alipoteza fahamu baada ya tukio hilo na alikimbizwa hospitali kwa matibabu.
Licha ya idadi kubwa ya
watu katika eneo hilo lenye biashara mbalimbali wakati wa jioni,
majambazi hao hawakujali, walifanya uporaji huo na baadaye kutokomea kwa
kutumia pikipiki aina ya Boxer.
Mashuhuda wa tukio hilo
waliliambia MTANZANIA jana kuwa kwa muda wa dakika tano hakuna gari
iliyoruhusiwa kwenda au kutoka Kimanga.
“Majambazi waliwaamuru wenye magari kutokukatiza eneo hilo, huku waenda kwa miguu wakiamriwa kuondoka haraka.
“Katika hali ya kawaida
ni vigumu kuamini kama majambazi wanaweza kuvamia na kupora vitu katika
maduka matatu kwa mpigo halafu wakatoweka bila kukamatwa,” alisema
shuhuda huyo aliyekataa kutajwa jina.
Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Kimanga, Manase Mjema, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema
majambazi hao yalikuwa yamejiandaa na yalitumia silaha kubwa.
“Awali kabla ya kufyatua
risasi yaliwaamuru wafanyakazi wa maduka yanayofanya biashara kupitia
miamala ya simu kutoa fedha zote za mauzo, vijana walikuwa ngangari
kidogo, hivyo majambazi waliamua kupiga risasi tatu hewani ndipo
waliamua kutoa fedha walizokuwa nazo,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti
huyo alikiri kuwapo kwa ulinzi hafifu katika mtaa wake, huku pia
akishauri Jeshi la Polisi kuimarisha doria mitaani kwa kuongeza askari
wasiokuwa na sare ili wasitambulike kwa urahisi.
“Nikiri kwamba ulinzi
wetu wa mtaa wakati wa usiku bado ni mdogo, tunaomba polisi nao
waangalie mbinu mbadala za kukabiliana na uhalifu, na hasa ujambazi huu
wa kutumia silaha za moto. Eneo la Tabata hivi sasa limekumbwa na
matukio mengi ya ujambazi, kwa hiyo lazima mbinu nazo zibadilike,”
alisema Mjema ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kimanga (Chadema).
Kwa upande wake, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alikiri kupokea taarifa za
ujambazi na tayari askari wake wameanza uchunguzi ili kuwabaini wahalifu
hao.
“Nitoe ombi na
nisisitize wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili
kutokomeza vitendo vyote vya uhalifu. Viongozi wote wa mitaa watupatie
taarifa za watu wanaowatilia shaka, nasi tutazifanyia kazi,” alisema
Kamanda Mkondya.
Katika siku za hivi
karibu kumeibuka matukio ya ujambazi katika maeneo mbalimbali nchini
huku wakiibua mbinu mpya za kufanikisha wizi huo.
Kutokana na hali hiyo
majambazi hao wamekuwa wakitumia pikipiki kwa ajili ya kutekeleza
uvamizi kwenye matukio hayo na hata wakati mwingine kuua watu na
kujeruhi.
Katika mfululizo wa
matukio ya ujambazi jijini Dar es Salaam, Agosti 23, mwaka huu, askari
wanne wa Jeshi la Polisi waliuawa baada ya majambazi kuvamia Tawi la
Benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke.
Majambazi hao
wanaokadiriwa kufikia 14, wakati askari hao wakibadilishana lindo,
waliibuka ghafla na kuanza kurusha risasi na askari mmoja aliyekuwa
lindo alifanikiwa kukimbia.
Kutokana na foleni
katika barabara nyingi za Dar es Salaam pamoja na miundombinu ya makazi
yasiyokuwa rasmi, matukio mengi ya ujambazi yanayoripotiwa ni ya kutumia
pikipiki, hivyo kuwapa wakati mgumu polisi ambao mara nyingi wanatumia
magari ya doria.
Mapema mwaka huu Rais
Dk. John Magufuli aliliagiza Jeshi la Polisi kutumia mbinu za kisasa
katika kukabiliana na uhalifu na kuifanya nchi kuwa sehemu salama
nyakati zote.
Dk Magufuli alionesha
kushangazwa na askari wa Jeshi la Polisi kunyang’anywa silaha yake na
majambazi na wakati mwingine kuuliwa na majambazi, akihoji uwezo wa
majambazi kiasi cha kuwatesa polisi kiasi hicho.
Rais alikuwa akizindua
Mpango wa kuboresha usalama wa jamii na mali zao, ambao una dhamira ya
kupunguza uhalifu ambapo ameliagiza jeshi hilo kuwahi kushughulikia
majambazi kabla ya wenyewe kushughulikiwa na majambazi hayo.
Pamoja na hali hiyo
Jeshi la Polisi lilitangaza mikakati mbalimbali ikiwamo ukaguzi maalumu
wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu ili kufuatilia
matukio mbalimbali.
Majambazi hao ambao kwa
muda sasa wamekuwa wakiibuka na mbinu mpya ikiwamo ya kutumia bodaboda
kuvamia benki na wanaotoka benki na kuwapora fedha.
Licha ya polisi kuweka
ulinzi maalumu na waendesha bodaboda watakaoonekana kupakia kitu
chochote na kukiweka mbele (katika tenki la mafuta) au kiti cha nyuma,
ikiwemo kusimamishwa na kupekuliwa lakini bado mbinu hiyo imekuwa
ikifeli na watu wakijikuta wakidhurika.
Katika miaka ya hivi
karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuvamiwa na
kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzichukua benki huku
wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa taarifa za wateja.
Mara zote majambazi
hutumia bodaboda kufanikisha uhalifu huo, huku wakiwa na silaha ambazo
huzitumia kutishia, kujeruhi na wakati mwingine kuua.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment