Friday, 21 October 2016

Alichosema Rais Magufuli kuhusu mikopo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu

...

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 483 kwa mwaka huu kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ambapo wanafunzi zaidi ya 118,000 watanufaika.

Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi la hostel za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo, Rais Magufuli amesema miongoni mwa hao watakaonufaika, wanafunzi 93,000 ni wanaoendelea na masomo na wanafunzi takribani 25,000 ni watakaoanza masomo mwaka huu huku akiweka bayana kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia masikini.

Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na upangaji mbaya wa wanafunzi katika vyuo, kutoa mikopo kwa upendeleo, kutozingatia sifa za mkopaji, kutoa mikopo hewa na kufungua vyuo kabla ya mikopo ya wanafunzi kutolewa na pia amewaonya wanafunzi kujiepusha na vitendo visivyofaa wakati Serikali inarekebisha dosari hizo.

"Na ndio maana wakati mwingine na wabaya wanapitia humo humo, mara fanye hivi fanyeni vile, wakati wanajua kuwa mkifanya yasiyofaa Serikali itawafukuza tu ili mkafanyie mambo yenu huko.

"Kwa sababu huwezi kuwa unahangaika kutafuta fedha za kuwapa mikopo, wakati huo huo unahitaji kujenga reli, wakati huo huo unahitaji kujenga barabara, wakati huo huo unahitaji kulipa mishahara, wakati huo huo unahitaji kutoa elimu bure, wakati huo huo Karagwe kuna njaa, wakati huo huo watu wanahitaji dawa hospitali, halafu watu wengine wanataka kukuendesha kana kwamba hela unayokusanya ni kwa ajili yao tu, ni lazima tuelewane na mimi ninataka kuwaeleza kwa dhati lazima twende katika njia iliyonyooka, ni bora uwe Rais usiye maarufu lakini utimize uliyoyaahidi, asitokee mtu wa kukuendesha, ninajua mmenielewa" amesisitiza Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kujipanga vizuri kukusanya marejesho ya mikopo kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo ambapo mpaka sasa bodi inadai takribani Shilingi Trilioni 2.6.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger