Wilaya ya Meatu imeanzisha Kiwanda cha Kusindika Maziwa, huku Maswa ikianzisha Kiwanda cha Uzalishaji Chaki vyote vikishirikisha makundi ya vijana.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema Bariadi inatarajiwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza sabuni; Busega kitajengwa kiwanda cha maji wakati mipango zaidi ikiendelea kuangalia kiwanda kinachofaa wilayani Itilima.
Mtaka alisema katika kutekeleza azma ya Tanzania ya viwanda, mkoa umekuwa ukifanya jitihada za kuwaunganisha vijana kwa kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
“Ni fedheha kuona hata bandeji za hospitalini zinatoka nje huku malighafi zake inapatikana nchini. Ni vyema kuzitumia fursa zilizopo na mikakati ya kuanzisha kiwanda cha bandeji na maji,” alisema Mtaka.
Katika kutekeleza kaulimbiu ya mkoa huo ya ‘One district one product’, wanatarajia kuwashirikisha vijana na kuwajengea uwezo ili wafanye kazi za kujiletea maendeleo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema wizara yake itaendelea kuwaunga mkono vijana wanaothubutu kwa kuwapa mikopo ili waazishe miradi.
Mhagama alisema vijana wa Simiyu wameonyesha njia kwa wenzao nchini na kuwaahidi kuwapa mkopo wa Sh30 kwa kuanzisha kiwanda cha chaki na maziwa.
Aliwataka vijana kuchangamkia fursa badala ya kukaa vijiweni na kulalamika kuwa hawana kazi.
0 comments:
Post a Comment