Serikali
inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kwa wanafunzi waliobaki kutokana
na ufinyu wa nafasi za shule za kidato cha tano, baada ya kubaini uwepo wa
nafasi hizo; na baadhi ya wanafunzi wenye sifa watachaguliwa kwenda kusomea
ualimu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bwana
Jumanne Sagini alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam juu ya wanafunzi
waliofaulu masomo ya sayansi.
Serikali kwa kutambua
umuhimu wa masomo ya sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi
kusoma masomo hayo, imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha
za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa majengo ili wanafunzi wengi zaidi
waweze kusoma masomo ya sayansi.
Bwana
Sagini alisema wanafunzi ambao wamefaulu vizuri masomo ya sayansi na wanapenda
kusoma masomo hayo wanayo fursa ya kubadilisha tahasusi (Combination) endapo zinapatikana
kwenye shule walizopangwa kupitia kwa wakuu wao wa shule. Iwapo tahasusi wanazozitaka hazifundishwi kwenye
shule hizo wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa Maafisa Elimu Mikoa ambayo shule
hizo zipo kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa ili waweze kubadilishiwa
tahasusi za sayansi kwenye shule zilizopo kwenye Mikoa husika.
“Jamii
inaweza kuwasiliana na watendaji wa wizara na Mikoa kwa simu ambazo
zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya waziri Mkuu- TAMISEMI. Hivyo, naendelea
kuwasisitiza watendaji wote wa Elimu hususani Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu
Mikoa kusimamia utekelezaji wa suala hili. Lengo la Serikali ni kuwa na idadi
kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ili kuendana na Malengo ya Milenia
na kutekeleza Mpango wa BRN.”alisema Katibu Mkuu.
Serikali
inaendelea kusisitiza kila mwanafunzi kwenda kuripoti shule aliyopangiwa
kuanzia tarehe 10-30 Julai, 2014, orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga
na kidato cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti za www.pmoralg.go.tz
na www.moe.go.tz
Serikali
inafanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu
katika fani za sayansi kwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kila
Mwanafunzi aliyefaulu masomo ya sayansi anapangiwa tahasusi ya masomo ya
sayansi.
Katika
matokeo ya mtihani kwa mwaka 2014, inaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 22,685
kati yao wasichana 7,859 na wavulana 14,826, wamechaguliwa kusoma tahasusi za
sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746 kati yao wasichana 5,038 na
wavulana 13,708 kwa mwaka 2013.
Uchaguzi
wa wanafunzi kidato cha tano kwa mwaka 2014, ulifanyika mwezi mei, 2014 na
matokeo yake kutangazwa kupitia tovuti ya OWM-TAMISEMI mwezi Juni 2014.Tofauti
na miaka mingine iliyopita, Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika
madaraja ya I-III umeongezeka kutoka watahiniwa 35,357 mwaka 2012 hadi 71,527
mwaka huu. Ufaulu huu ni zaidi ya asilimia mia moja ya watahiniwa waliokuwa na
sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka 2013.
Matokeo
haya yanakaribia sana malengo ambayo
Serikali imejiwekea kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (yaani Big Results
Now-BRN) ambapo serikali ilijiwekea lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu
kwa asilimia 60 mwaka 2013. Matokeo halisi yanaonyesha kuwa ufaulu umepanda
kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.
0 comments:
Post a Comment