Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imetoa Shilingi Bilioni 17 kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, hali itakayosaidia kuondoa upungufu wa zaidi ya lita milioni 2.7 za maji unaojitokeza kila siku Wilayani hapo.
Kwa mujibu wa Meneja wa DUWASA Wilaya ya chamwino Gray Mbalikila
ameeleza kuwa kwa sasa mahitaji ya maji katika mji huo ni wastani wa lita milioni 7.5 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa lita milioni 4.8, hivyo kusababisha upungufu mkubwa kwa wananchi.
Akizungumza mapema leo Sept 15,2025 Mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule kutembelea Mradi huo,Meneja huyo amesema mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama, kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi, na kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama.
Amesema Mkataba wa mradi huo ulisainiwa tarehe 6 Juni 2022 na utekelezaji ulianza rasmi mwaka 2023 na kwamba Utekelezaji huo unatarajiwa kukamilika ifikapo 10 Desemba 2025, ambapo hadi sasa mradi umefikia asilimia 45.
Amefafanua kuwa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 500,000 Chamwino, tenki la lita 200,000 Msanga na tenki kubwa la lita milioni 2.5 Buigiri.
Vilevile, mradi unahusisha ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 47, ikiwemo km 31 za mabomba makuu na km 16 ya kusafirisha maji kuelekea Msanga na Buigiri.
Amesema Mradi huo utakapokamilika, zaidi ya wananchi 59,000 katika kata 4, vijiji 7 na vitongoji 48 watanufaika na huduma hiyo.
"Upatikanaji wa maji safi utaongezeka kutoka asilimia 91 ya sasa hadi kufikia asilimia 100, huku uzalishaji ukiongezeka hadi wastani wa lita milioni 12.32 kwa saa 22 za uzalishaji, " ameeleza
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata maji bora na salama kwa wakati, na kuwataka wakandarasi kukamilisha kazi kwa viwango na muda uliopangwa.
“Tunataka wananchi wa Chamwino wapate maji safi na salama yenye ubora unaohitajika, ni lazima mkandarasi ajipange ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati,” amesema Senyamule.
Ameongeza kuwa wakandarasi wanapaswa kuongeza idadi ya mafundi na kuondoa visingizio visivyo na msingi, huku akiwataka vijana wazawa wanaoshiriki kwenye ujenzi wa mradi huo kuwa walinzi wa ubora wa kazi inayoendelea.
Kutokana na hayo baadhi ya Wananchi wa Chamwino wameeleza matumaini yao kwa mradi huo ambapo Juma Shabani wa Buigiri amesema mgao wa maji ulikuwa kero kubwa, lakini sasa hali inabadilika.
Kwa upande wake Theresia Paulo wa Msanga ameeleza kuwa watoto walikuwa wanapoteza muda wa masomo kwa kufuata maji mbali, hali ambayo sasa itabaki historia.
Naye Richard Mawela wa Chamwino mjini amesema mradi huo utaleta mabadiliko makubwa na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kumtua mama ndoo kichwani.



0 comments:
Post a Comment