Na Dotto Kwilasa,Dodoma
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewataka madereva wa Serikali kote nchini kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu ili kuhakikisha usalama wa maisha, mali na siri za Serikali.
Amesema madereva hao ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali na hivyo wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika mwenendo na maadili kazini.
Akizungumza leo Jumanne, Septemba 2, 2025, jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), Waziri Mkuu amesisitiza kuwa madereva wana wajibu wa kufanya ukaguzi wa magari kabla na baada ya safari kwa kuhakikisha wanajaza kikamilifu taarifa za safari na matengenezo.
"Mnatakiwa kutunza kumbukumbu hizo kwa uaminifu, acheni vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya watu, usalama wa mizigo na nyaraka za Serikali, au kuhatarisha hadhi ya utumishi wa umma, " Amesema na kuongeza;
Ni muhimu kuhakikisha mnavitumia vifaa vya kisasa vya usalama barabarani na kujiepusha na matumizi mabaya ya magari ya Serikali au kushiriki katika shughuli zinazoweza kuathiri ulinzi na usalama wa taifa,kumbukeni kuwa dereva ni muhimili wa usalama wa safari, abiria na nyaraka muhimu za Serikali,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amekipongeza Chama hicho cha Madereva wa Serikali kwa mchango wake katika kuboresha huduma za usafirishaji Serikalini na kuimarisha ustawi wa madereva. Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili madereva.
Amesema , Serikali inajipanga kuboresha mazingira ya kazi, upatikanaji wa mafunzo ya mara kwa mara na uboreshaji wa maslahi ya madereva.
“Changamoto mlizowasilisha ni kielelezo cha kazi kubwa iliyopo mbele yetu ,Kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, waajiri na chama chenu, tutaendelea kusonga mbele kwa hatua madhubuti,” ameongeza.
Pia ametoa maagizo kwa waajiri kuhakikisha kuwa stahiki za madereva zinalipwa kwa wakati, ajira zinatekelezwa kwa mujibu wa muundo rasmi wa utumishi wa umma, na madereva wanapewa fursa za motisha kama ilivyo kwa watumishi wengine.
Amewataka waajiri kuzingatia haki za msingi za madereva ikiwa ni pamoja na mazingira bora ya kazi na usalama kazini.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa madereva wa Serikali ni mhimili muhimu katika shughuli zote za kila siku Serikalini na kuwa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu wao vina mchango mkubwa katika mafanikio ya taasisi za umma.
“Tutahakikisha kuwa ustawi wa madereva unakuwa kipaumbele chetu. Dereva akifanya kazi katika mazingira bora na yenye heshima, atatoa huduma bora kwa wananchi na Serikali kwa ujumla,” amesema Waziri Ulega.
Naye Katibu Mkuu wa CMST, Castro Nyabange, ameitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua mbalimbali anazochukua kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, ikiwemo madereva wa Serikali.
Amesema upandishaji wa mishahara na maboresho ya mazingira ya kazi umewagusa madereva moja kwa moja na kuahidi kuwa chama chao kitaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na madereva Serikalini zinaendelea kuwa za kiwango cha juu na za kuaminika.
Mkutano huo uliobeba kaulimbiu isemayo “Dereva wa Serikali, Epuka Ajali, Linda Gari Lako na Watumiaji Wengine wa Barabara na Oktoba Shiriki Uchaguzi Mkuu”, umehudhuriwa na zaidi ya madereva 2,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Mkutano huo unalenga kujadili changamoto, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano kati ya madereva na Serikali katika kuboresha huduma kwa umma.






0 comments:
Post a Comment