Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kutembelea mradi wa kusimika kamera za usalama (CCTV) katika jiji la Dodoma, mradi unaolenga kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, mali zao pamoja na miundombinu ya umma.
Mradi huo unahusisha njia kuu nne zinazoingia na kutoka jijini pamoja na baadhi ya maeneo ya ndani ya jiji yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, miundombinu ya serikali na maeneo yenye historia ya matukio ya kihalifu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, amesema mradi huo unahusisha ufungaji wa nguzo 50 zitakazobeba jumla ya kamera 106 ambazo zina uwezo wa kusoma namba za magari, sura za watu, kuhesabu vyombo vya usafiri na watu, pamoja na kubaini matukio mbalimbali ikiwemo magari yaliyopaki sehemu zisizoruhusiwa .
Amesema Mradi huo utakapo kamilika utasaidia kudhibiti makosa ya barabarani, vitendo vya jinai na uharibifu wa miundombinu, huku ukitoa uhakika wa usalama kwa wadau wa maendeleo na wawekezaji.
Ameeleza kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 473 ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
"Halmashauri imeingia mkataba na Kampuni ya Wisjane Smart System, iliyopokea kazi rasmi tarehe 1 Juni mwaka huu, na inatarajiwa kukamilisha ndani ya siku 90 tangu kuanza kwake, " ameeleza Shekimweri.
Kwa upande wa Mtaalam wa mradi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wisjane Smart System, Wisley Ussiri, amesema Kamera zilizofungwa ni za aina tatu .
Amezitaja kuwa ni kamera zinazoweza kusoma namba za magari, kamera zenye uwezo wa kufuatilia matukio kwa umbali mrefu wa viwanja 45 vya mpira sawa na kilomita 4.5, na kamera za kufuatilia mienendo ya watu na kwamba Maeneo ya vipaumbele ya ufungaji ni Nala, Machinga Complex na maeneo ya katikati ya jiji la Dodoma.
Ussiri ameongeza kuwa Mfumo huu, unaoendeshwa kwa teknolojia ya kisasa, unatarajiwa kusaidia vyombo vya usalama kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa changamoto ya uhaba wa nguvu kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema utekelezaji wa mradi huu utakuwa chachu ya kuongeza usalama na kudhibiti uhalifu jijini Dodoma, kwani kamera zitakuwa zikirekodi na kubaini matukio mbalimbali kwa haraka.
Amesisitiza kuwa uwepo wa Kamera hizo pia utaleta heshima kwa jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi.
Senyamule amezitaka Taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwekeza katika mifumo ya ulinzi wa kisasa itakayosaidia kulinda rasilimali zao.
Aidha, ameahidi kuendelea kusimamia suala la amani na utulivu hususan katika kipindi cha uchaguzi, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanatimiza haki zao bila kuvunja sheria.








0 comments:
Post a Comment