Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mwanasiasa na mtumishi wa watu, Anthony Mavunde, amezindua rasmi kampeni zake za kugombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa kishindo kikubwa, akiahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira katika jimbo hilo endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo leo Sept. 3,2025 Mavunde amesema kuwa anaomba ridhaa ya wananchi ili aendelee kuwatumikia kwa moyo mmoja, kwa kuwa amekuwa akiishi nao, anazifahamu changamoto zao, na ana nia ya dhati ya kuzitatua.
Mavunde ameeleza kwamba Serikali inawekeza zaidi ya shilingi bilioni 600 katika ujenzi wa mji mpya wa Serikali eneo la Mtumba, jambo ambalo ni fursa ya kipekee ya kufanya Jimbo hilo kuwa la kisasa, wa kuvutia na wenye huduma bora.
Amesisitiza kuwa uongozi wake utalenga kuhakikisha maendeleo hayo yanawanufaisha wananchi wa kawaida kwa kuwawekea miundombinu na huduma bora karibu yao.
Ameeleza kuwa tayari amejenga shule kadhaa zikiwemo Shule ya Msingi Chiwondo, Mkoyo, na Mahomanyika Sekondari ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Chahwa unaendelea.
Mavunde ameahidi kuwa kila kata au mtaa usio na shule, atahakikisha unapata shule ili kuondoa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.
Aidha, amesema atapambana kuhakikisha michango ya mitihani ya Jumamosi inaondolewa ili kuwapunguzia mzigo wazazi.
Katika kuboresha miundombinu, Mavunde ameeleza kuwa atahakikisha barabara ya Hombolo – Mayamaya pamoja na barabara nyingine za ndani zinazopitika kwa shida zinajengwa kwa kiwango bora.
Ameahidi kununua greda maalum litakalotumika kwa matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hizo ndani ya jimbo.
Kwa upande wa huduma ya maji, Mavunde amesema kuwa uwezo wa kuzalisha maji jijini Dodoma kwa sasa umefikia lita milioni 47 kwa siku na lengo lake ni kuhakikisha kila kata ikiwemo Hombolo, Ihumwa, na Mahomanyika inapata maji safi na salama kwa urahisi.
Amesema baadhi ya maeneo yenye uhitaji mkubwa huduma hiyo itatolewa bure, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo muhimu.
Mavunde amesema kuwa ili yote hayo yatimizwe anahitaji ushindi ili aendelee kuwa mtumishi wa kweli wa watu wa Mtumba huku akiahidi utumishi wa haki, uwazi, na maendeleo kwa vitendo kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi wake.




0 comments:
Post a Comment