Na Mwandishi wetu, Rutamba-Lindi
Katika tukio lililojaza shamrashamra na hamasa kubwa ya kisiasa, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Salma Rashid Kikwete, ameongoza uzinduzi mkubwa wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Salma, ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amepokelewa kwa shangwe na mamia ya wananchi katika viwanja vya Mahakama, Kata ya Rutamba.
Uzinduzi huo ulipambwa na uwepo wa viongozi wakuu wa kitaifa, akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Pia, tukio hilo lilishuhudia uwepo wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, aliyehudhuria kutoa baraka zake kwa mgombea na kuhakikisha mshikamano ndani ya chama unaimarishwa katika kuelekea uchaguzi huo muhimu.
Katika hatua ya kilele ya uzinduzi huo, Mhe. Salma Kikwete alipokea rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 kutoka kwa Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, madiwani wote wa Jimbo la Mchinga walikabidhiwa nakala za Ilani hiyo huku wakihimizwa kuwa bega kwa bega na Mbunge ajaye katika utekelezaji wa miradi na sera zilizomo.
Akihutubia wananchi waliohudhuria, Waziri Mkuu Majaliwa aliwahakikishia kuwa Serikali ya CCM itaendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi wa Mchinga kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi inatekelezwa kwa ufanisi ili kuinua maisha yao na kuleta maendeleo endelevu kwa jimbo zima.
Uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa kampeni zenye mvuto, mshikamano na matumaini makubwa kwa wananchi wa Mchinga, huku wakionesha imani kubwa kwa CCM na wagombea wake.




0 comments:
Post a Comment