Thursday, 18 May 2023

WAZIRI MCHENGERWA AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUTOA MSAADA WA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI KUIMARISHA USALAMA KWA WATALII JIJINI ARUSHA

...

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa (wa pili kushoto) akiwa katika pikipiki zilizokabidhiwa na Benki ya CRDB kwa Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia jijini Arusha kwa ajili ya kusaidia katika doria na kuimarisha ulinzi na usalama kwa watalii. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya Arusha, Felician Mtahengerwa (wa kwanza kulia), na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo.

======== ======== =========


Arusha Tarehe 18 Mei 2023 - Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa msaada wa pikipiki 15 kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha ili kuimarisha doria zitakazoongeza usalama kwa watalii wanaokuja nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Utalii na Maliasili, Mohamed Mchengerwa alipopokea pikipiki hizo zenye thamani ya TZS 40 milioni kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia kilichopo jijini hapa.
Waziri amesema sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika uchumi na maendeleo ya wananchi nchini kwani ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, ikiwa ya pili kwa kuchangia kwenye Pato la Taifa (GDP), na ya tatu kwa kutoa ajira.


“Ripoti za Benki Kuu Tanzania (BOT) zinaonyesha sekta ya utalii inaendelea kuimarika baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19. Mapato yatokanayo na utalii kwa Machi yalifikia Dola za Marekani bilioni 2.787 ikilinganishwa na dola milioni 885 kipindi kama hicho mwaka 2021. Katika mwezi huo, jumla ya watalii 1,574,630 waliingia nchini,” amesema Mchengerwa na kuongeza huku akipongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour.


“Kipeeke kabisa naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa msaada huu wa pikipiki 15 ambao Benki yetu ya CRDB imeutoa kwa kituo chetu hichi. Pikipiki hizi zitawawezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Askari watakabiliana haraka na dharula jambo litakalosaidia kuimarisha usalama kwa watalii na kuifanya nchi yetu kuwa kivutio kikubwa hivyo wageni wengi kuja kuitembelea.”
Mwaka 2020, sekta ya utalii ilichangia asilimia 10.6 kwenye pato la taifa ila kiasi hichi kilishuka hadi asilimia 5.7 mwaka 2021 kutokana na athari za UVIKO-19 hivyo kuilazimu Serikali kuchuku ahatua za makusudi kuifufua kwa kufuata taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanya matangazo kimataifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe kurekodi filamu ya ‘The Royal Tour.’


Ili kuhakikisha usalama wa watalii wanaokuja nchini, Serikali ilianzisha kitengo maalum cha utalii na diplomasia kwa ajili ya kuwahudumia watalii na wanadiplomasia wanaofika nchini kutalii ama kuwekeza kwa haraka.


Kwa kuwa jiji la Arusha ndio kitovu cha utalii nchini, kituo hicho kimejengwa huko na askari wake walipewa mafunzo ya ziada ndani na nje ya nchi juu ya namna bora ya kuhudumia watalii. Vituo vingine vidogo vimefunguliwa katika wilaya za Arumeru, Karatu, Monduli na Longido.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa amani, utulivu na usalama katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo ni jukumu la jamii nzima kushiriki kuuimarisha.


“Pamoja na kuwepo hali ya amani na utulivu nchini, bado baadhi ya matukio ya uhalifu hujitokeza kama vile vile uporaji wanaofanyiwa raia hata watalii wanaokuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Ili Jeshi la Polisi litekeleze majukumu yake kwa ufanisi linahitaji vitendea kazi vya kutosha,” amesema Nsekela.


Mkurugenzi huyo amesema wanayo furaha kubwa kukabidhi pikipiki hizo ili kuwasaidia askari kukimbizana na wahalifu wanaowapora watalii au kusafirisha mihadarati hivyo kuharibu sifa njema za jiji hili la kitalii.
“Tunaamini matumizi sahihi ya pikipiki hizi yatasaidia kudhibiti uhalifu jijini hapa na tunaahidi tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kupunguza baadhi ya changamoto zinazokwamisha ufanisi wake ili nchi yetu iendelee kuwa salama kwa biashara na uwekezaji,” amesema Nsekela.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Edith Swebe, amesema jitihada zinazoendelea kuutanga utalii wa Tanzania umelifanya Jiji la Arusha kupokea wageni wengi wanaoongeza haja ya askari polisi kuwapo katika kila eneo.
“Tunachokifanya sasa hivi ni kusimamia mradi wa utalii salama ambao unahitaji askari kuwapo kila walipo wageni. Pikipiki hizi tunazozipokea zitasaidia kuwafikisha askari kwenye maeneo ambako magari hayawezi kufika kwa urahisi zikiwamo barabara nyembamba. Jeshi la Polisi linaaminimazingira salama ni kivutio cha utalii,” amesema Edith ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa kamanda wa Mkoa wa Simiyu.


Hata hivyo, ameiomba Serikali na wadau wengine wa utalii kuliwezesha jeshi hilo kupata pikipiki nyingine 10 zitakazofanya kata zote 25 za Jiji la Arusha kuwa na pikipiki moja ya doria itakayosaidia utekelezaji wa mradi wa utalii salama.









Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger