Mwanachuo aliyejiteka
Kennedy Nyangige mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha udaktari Bugando anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kujiteka na kisha kutuma meseji kwa wazazi, ndugu na viongozi wake wa chuo akidai ametekwa na inatakiwa milioni 3.5 ili aachiwe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa daktari wa hospitali ya rufaa ya kanda Bugando aitwaye Matiko Sirari jeshi la polisi lilianza kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kubaini kwamba kijana huyo alikuwa anadanganya ametekwa na wakati alijiteka mwenyewe ili pate hiyo hela.
Aidha Kamanda Mutafungwa amesema wakati anatuma ujumbe huo alikuwa kwenye nyumba ya kulala wageni huku anakunywa bia ndipo askari polisi walipomtia mbaroni na kwamba atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika
"Sasa baada ya tukio hilo na maelezo hayo huyo mtuhumiwa alikamatwa na kuletwa katika kituo cha polisi kwa mahojiano na tumeweza kuokoa fedha alizokuwa akizitaka kwa njia ya kitapeli kwamba ametekwa kumbe amejiteka mwenyewe, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa vijana ambao familia zao zimewaamini na kuwapeleka kwenye vyuo vya gharama kubwa kuacha janjajanja kuacha utapeli kwa kujipatia kipati kwa njia isiyo halali," amesema Kamanda Mutafungwa.
CHANZO -EATV
0 comments:
Post a Comment