MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishauri serikali kuanzisha kanda maalum ya kilimo ili kuwezesha zao kulimwa kwenye mkoa husika unaostahmili zao hilo.
Akichangia bajeti ya wizara ya kilimo Mei 9,2023,Mtaturu amesema ikifanyika hilo usalama wa chakula utakuwepo na mwisho wa siku pato la Taifa litaongezeka kupitia sekta ya kilimo.
“Nikuombe sana nchi hii tumekuwa sasa kutoka Mtwara mpaka Kigoma watu wanataka wote walime zao moja linaitwa korosho haiwezekani mwenyekiti,hatuwezi kuwa na kilimo cha korosho nchi nzima hata mazingira au hali ya hewa hairuhusu maana yake hata concetration ya namna ya kusaidia kilimo haitakuwepo,
“Mtu atoke kule Tandahimba anataka kwenda mpaka kule Mwanza alime alizeti haiwezekani ,tufike mahali tuwe na kanda maalum kwamba hii kanda ni ya alizeti kama ni Singida tu constrate pale Singida na mikoa ambayo inaweza kutoa maeneo,”amesisitiza.
Amempongeza Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mkoa wa Singida Parseko Koni kwa ambaye alizuia mahindi kulimwa mkoani humo na badala yake akaelekeza watu walime mtama na matokeo yake ikazalishwa kwa wingi.
ENEO LA UMWAGILIAJI.
Akichangia eneo hilo Mtaturu ameishauri serikali kuzingatia kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Nina amini kabisa mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kilimo cha Tanzania na sio Tanzania pekee bali maeneo mengi ya Afrika, lakini kama tutaendelea na hali ya kusubiria huruma ya Mungu kwa ajili ya kuleta mvua peke yake hatutaweza kusogeza kilimo hiki na kila mwaka tutakuja na sababu kwamba mwaka jana hatukufikia lengo kwa sababu mvua haikunyesha za kutosha,”amesema.
Ametoa ombi kwa serikali kutenga bajeti ya kutosha kwenye eneo la skimu za umwagiliaji ,lakini tunaomba skimu hizi nani anaenda kuzitunza kule chini,tunaona skimu nyingi hazitoi matokeo na kuna baadhi ya maeneo hata watu hawajui maana ya skimu yenyewe,nikuombe Waziri tutafute Mechanism nzuri ya kusimamia hili,
Amesema kuna maeneo mengi ya mito ,kuna maji ambayo yanapita kila mahali lakini wasipozuia maji na kuyatumia vizuri maana yake kilimo hakitaweza kubadilika.
SKIMU YA UMWAGILIAJI YA MANG’ONYI.
“Tunajua kwenye wizara yako umeiangalia skimu ya Mang’onyi lakini nikuombe waziri wakati unahitimisha hoja uzingatie hili,watu wa Mang’onyi wanataka kusikia wizara inasemaje,mwaka huu wa fedha tujenge ile skimu na kuiboresha kwa kuwa sasa hivi kuna soko la mbogamboga katika mgodi wa Ashanta ambao upo pale Mang’onyi,”amesema.
Mtaturu amesema wakitaka mabadiliko kwenye sekta ya kilimo nchini yanahitajika mambo matatu ambayo ni utaalam kwa maana ya teknolojia au elimu,uwekezaji kwa maana ya fedha na pembejeo ambazo zinafaa katika maeneo ya nchi.
“Ukienda kwenye utaalam ni afisa ugani wangapi ambao wana uwezo wa kumsaidia mkulima pale kijijini,wengi wanazidiwa uwezo na wakulima hivyo kuna haja ya kuwasaidia kubadilisha mtazamo wa kazi wanazozifanya,”ameongeza.
Ameiomba serikali iongeze fedha za kutosha kwenye eneo la kilimo ili watu Milioni 40 wanaojishughulisha na kilimo waweze kubadilisha kilimo na uchumi wan chi.
“Eneo la mbolea,viuatilifu na mbegu ni eneo ambalo tukifnaya vizuri na kuongeza utafiti na mbegu za kutosha zinazofaa zitamfanya mkulima awe na matokeo makubwa kwenye eneo lake,”.
SHUKRANI KWA SERIKALI.
“Kwanza nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kukibadilisha kilimo cha Tanzania kwa kuamini kabisa tukiboresha kilimo maana yake unaboresha uchumi wao watanzania wengi ambao wanafanya kazi hii,
“Nimshukuru zaidi waziri Bashe kwa namna ambavyo sisi watu wa Ikungi tulivyokuwa na changamoto ya upungufu wa chakula lakini wakatuletea chakula cha bei nafuu kutoka NFRA ,chakula kilitusaidia na leo tunaenda kufanya mavuno,”ameeleza.
KILIMO KILIVYOSHABIHIANA NA ILANI YA CCM.
Mtaturu amesema kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),yam waka 2020/2025,imeahidi kusimamia vizuri eneo la matumizi endelevu ya maji ya ardhi na ardhi ya kilimo na kuongeza miundombinu ya umwagiliaji jambo ambalo kupitia bajeti iliyosomwa tunaona linaendelea kutekelezeka.
“Makadirio yaliyowekwa mpaka 2025,tunapaswa tufikie asilimia 28 ya Pato la Taifa,lakini ukiangalia kwenye wasilisho tumefikia asilimia 26.1 maana yake tunaenda vizuri,miaka miwili na nusu ijayo huwenda tutafikia asilimia 28 kama ilivyoahidiwa katika Ilani,”amebainisha.
0 comments:
Post a Comment