Friday, 12 May 2023

KATAMBI:TUTAENDELEA KUWACHUKULIA HATUA WAAJIRI WASIOWAPA MIKATABA WAFANYAKAZI

...

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akijibu swali Bungeni leo Mei 12, 2023, jijini Dodoma.




Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akijadili jambo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei, 2023.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeanza kufanya ukaguzi na kuwachukulia hatua waajiri wanaokwepa kuwapa mikataba wafanyakazi kwa kuwatumia kama vibarua ili kunyonya haki zao.

Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo bungeni leo Mei 12, 2023 alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Mhe. Sophia Mwakagenda. Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji serikali inatoa kauli gani kwa baadhi ya viwanda kwenye Mkoa wa Pwani maeneo ya Mbagala na Mkuranga vinavyowatumikisha wafanyakazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni na kuwaa ujira wa Sh.4,000 kwa siku.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Katambi amesema serikali imebaini wapo waajiri wanakwepa kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi ili kuendelea kuwaita vibarua na kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu ni unyonyaji mkubwa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kuchukua hatua na tunafanya kaguzi kujua historia ya wafanyakazi wamefanya kazi kwa kipindi gani na aina ya kazi anayoifanya ili kuwaingiza kwenye mifumo ya kuwa na mikataba ya kazi ili haki zao zilindwe kwa mujibu wa sheria,”amesema.

Naibu Waziri huyo amesema katika sheria ya ajira na mahusiano kazini inaeleza moja ya mambo ni kukubaliana yawe kimkataba na yaandikwe na kuwekwa wazi na kitendo cha waajiri kutolipa mishahara au masilahi yao ni kuvunja sheria hiyo.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo amehoji lini Serikali itahakikisha watanzania wanaofanya kazi kwenye kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi ili kulinda haki za wafanyakazi kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara katika Sekta Binafsi imefanya utafiti na kuboresha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi na tayari viwango vimetangazwa.

Amelihakikishia bunge kuwa ofisi hiyo itahakikisha waajiri wanatekeleza ipasavyo viwango vya mishahara vilivyotangazwa kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya kazi na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili kujenga uelewa wao katika kutekeleza Sheria za kazi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger