Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mohamed Gaber Abulwafa.
Na Dotto Kwilasa, DODOMA
CHUO Kikuu cha Misri kimeeleza kusudio la kuanzisha tawi lake nchini Tanzania kwa ajili ya kuanza kutoa elimu katika fani mbalimbali.
Kutokana na hayo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemuelekeza Mkurugenzi anayeshughulikia Vyuo Vikuu katika Wizara hiyo Dkt.Kenedy Hosea kuhakikisha anaanza mazungumzo na vyuo vikuu nchini ili kuona ni chuo gani kipo tayari kuanza ushirikiano huo ili utekelezaji uanze mara moja .
Waziri Mkenda ameeleza hayo leo 16, Agosti 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mohamed Gaber Abulwafa katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jijini Dodoma.
Amemweleza Balozi huyo kuwa serikali ya Tanzania imetoa fursa ya wawekezaji kuja nchini kwa kufuata taratibu za kisheria na kuwekeza haraka iwezekanavyo.
Amesema wakati taratibu zingine zinaendelea za uwekezaji huo, Chuo kikuu hicho kinaweza kuunda ushirika na Chuo Kikuu chochote kilichopo nchini ili kuanza kutoa elimu kusudiwa kwa haraka.
Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini Tanzania Mohamed Gaber Abulwafa amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.
Katika mazungumzo hayo wamejadiliana pia namna ya kuanza utekelezaji wa haraka wa (MOU) zilizosainiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini Misri.
Pia Balozi Abulwafa amewasilisha mualiko wa Waziri wa Nishati wa Misri kumualika katika mkutano utakaokuwa unajadili masuala ya Atomiki pamoja na mwaliko wa Waziri wa elimu wa Misri ili kujadili kwa kina umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu.
0 comments:
Post a Comment