Na Elisante Kindulu - Chalinze
CHAMA Cha walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya BAGAMOYO kimeendelea kutoa misaada mbalimbali mashuleni ikiwa ni pamoja na kusaidia vifaa vya ujenzi.
Hatua ya kusaidia vifaa vya ujenzi imekuja baada ya shule ya Sekondari ya Dunda kuezuliwa na upepo kwa choo cha wanafunzi wa kike na hivyo kufanya vijana hao kupata changamoto kupata huduma hiyo muhimu.
Vifaa hivyo vilikadhidhiwa na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Bagamoyo, Mwl. Hamisi Kimeza pamoja na Katibu wake Mwl. Shaaban Tessua katika viwanja vya shule hiyo hivi karibuni.
Katibu Tessua alisema kwamba vifaa hivyo vya upauaji ni hatua ya mwanzo tu ya msaada wao huku vifaa vingine vikiwemo mifuko ya saruji kupitia CWT mkoa wa Pwani kitengo cha walimu wanawake nayo itafuata.
Katika hatua nyingine CWT Wilaya ya Bagamoyo imeendelea kutoa majiko ya gesi kwa ajili ya walimu mashuleni ikiwa ni sehemu ya Mchango wake ili walimu waweze kupata huduma ya pamoja ya chakula wawapo mahala pa kazi.
Akikabidhi majiko hayo akiwa na baadhi ya wajumbe wa CWT wa kamati ya utendaji ya Wilaya, Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Bagamoyo Mwl. Hamisi Kimeza alisema, lengo la kutoa majiko hayo ni kuongeza mshikamano na upendo kwa walimu wawapo mahala pa kazi, kwani chakula ni eneo mojawapo la kuwakutanisha wote kwa wakati mmoja.
Lakini Mwenyekiti huyo aliwaeleza walimu kuwa chama Wilaya hakitakuwa na fedha za kujaza gesi baada ya ile ya awali kumalizika , badala yake akawashauri watafute namna ya kupata fedha hata kuchangia fedha zinazorejeshwa mashuleni kwa ajili ya posho ya vikao vya kichama mahala pa kazi.
Naye Katibu wa Chama hicho Wilaya ya Bagamoyo, alisema kuwa wamefanya zoezi Hilo katika awamu mbili kwa baadhi ya shule ,lakini lengo Ni kuzifikia shule zote za halmashauri ya Chalinze pamoja na Bagamoyo zilizopo wilayani Bagamoyo.
Mwenyekiti wa CWT ,Wilaya ya Bagamoyo Hamisi Kimeza(kushoto) na Katibu wa Chama hicho wa Wilaya, Shaaban Tessua(kulia) wakikadhi mbao kwa walimu wa shule ya Sekondari Dunda ili kusaidia matengenezo ya choo kilizoezuliwa na upepo shuleni hapo.
0 comments:
Post a Comment