Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene amemaliza mgogoro wa Uraia wa Mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Denis ambaye awali aliwahi kucheza Klabu ya Mbeya City FC ya Mbeya kabla ya kutua kwa Wekundu wa Msimbazi Simba SC.
Hivi karibuni iliripotiwa kuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kim Paulsen ameshindwa kumjumuisha Kibu katika Kikosi chake kutokana na kushindwa kutambulika uraia wake rasmi.
Baada ya sakata hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imejitokeza na kutoa ufanunuzi ambapo sasa Kibu amepewa uraia wa Tanzania kama ilivyotambuliwa awali ambapo aliwahi pia kucheza Taifa Stars.
“Kufuatia Mamlaka aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililoletwa kwake na TFF, amempa URAIA wa Tanzania Mchezaji wa Mpira wa Miguu, Kibu Denis Prosper, Sept. 30, 2021”, Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kurasa zake rasmi za Mitandao ya Kijamii.
Mshambuliaji Kibu Denis alicheza mchezo wa kirafiki Julai 13, 2021 kati ya Taifa Stars dhidi ya Malawi ambapo Stars waliondoka na ushindi wa bao 2-0 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment