Wednesday, 27 October 2021

GGML YAKABIDHI VIFAA, ZANA ZA THAMANI YA MILIONI 132 KWA VETA MOSHI

...

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai akikata utepe kuzindua zana zilizotolewa na Kampuni ya GGML kwa Chuo cha VETA Moshi kwa ajili ya mafunzo kwa wanafunzi wanaosomea kozi zinazohusu masuala ya madini.
Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo akihutubia wageni waliohudhuria hafla ya kukabidhi msaada wa zana mbalimbali zilizotolewa na kampuni hiyo kwa Chuo cha VETA Moshi kwa lengo la kuwafundishia wanafunzi wanaosomea masuala ya madini.


***

Na Mwandishi wetu

Kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu Geita (GGML) imekabidhi rasmi zana/vifaa mbalimbali kwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Moshi vitakavyowezesha kutekeleza Mradi wa Mafunzo Jumuishi ya Ujuzi kwa Ajili ya Sekta ya Madini (Integrated Mining Technical Training-IMTT) kikamilifu.

Mradi huo maalum wa mafunzo unaohusisha sekta na wadau mbalimbali zaidi ya makampuni ya madini, unaendeshwa kwa mfumo wa uanagenzi kupitia chuo cha VETA Moshi baada ya kuasisiwa mwaka 2008 na GGML pamoja na makampuni mengine ya uchimbaji madini kupitia Chemba ya Nishati na Madini Tanzania(TCME).

Akikabidhi vifaa hivyo, mwishoni mwa wiki mjini Moshi, Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo alisema vifaa hivyo vina thamani ya Shilingi milioni 132.

Aidha, alisema GGML pia ilianza kufadhili vijana wanaozunguka mgodi wake huko mkoani Geita kuhudhuria kozi za ufundi stadi kuhusu madini zinazotolewa na VETA Moshi.

“Juni 2014 GGML ilisitisha programu yake ya mafunzo ya kiufundi ya ndani, ambayo ilikuwa inaendeshwa kwa miaka kadhaa. Baada ya uamuzi huu zana zilizokuwa zikitumika kwa programu zilihifadhiwa.

“Aprili mwaka huu uongozi wa GGML uliamua kuchangia zana hizi kwa taasisi yoyote ambayo iko katika nafasi nzuri zaidi ili kunufaisha kundi kubwa la wanufaika, na VETA Moshi ilionekana kuwa mnufaika anayefaa zaidi.

“Hivyo sasa, GGML inafuraha kukabidhi rasmi zana/vifaa vitakavyoiwezesha VETA Moshi kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuendelea kuboresha ubora wa wanafunzi wanaohitimu hapa katika kozi mbalimbali zinazohusiana na tasnia ya uziduaji.

Alisema GGML inatarajia zana zilizotolewa kwa VETA Moshi zitawawezesha wanafunzi wengi kupata ujuzi ambao ni muhimu kwa ajili ya kujiajiri na kujikimu kimaisha.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu alisema msaada huo kiuhalisi ni mkubwa kuliko thamani ya fedha iliyoainishwa.

"Kwenye makaratasi huu msaada unaonekana ni wa Sh milioni 132, lakini kiuhalisia manufaa ni zaidi ya hapo," alisema.

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai alisema ni dhahiri kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika chuo hicho cha Moshi kwa sababu wanafunzi watakwenda kunufaika na kumaliza masomo yao wakiwa na ujuzi bora.

“Ni kwamba serikali ilifanya mabadiliko ya sheria ya madini na kutunga sheria mbalimbali zinazoendaa na sheria hiyo lengo kusisitiza makampuni yanayochimba madini kutekeleza mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

“GGML wamekwenda mbele zaidi kwani wangetakiwa kufanya hivyo katika eneo la Geita lakini wamekuja hadi Moshi, hawa ni watu wazuri sana ndio maana nasema wanahitaji kupongezwa sana,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai (kushoto) akimpongeza Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo (katikati) kwa msaada wa zana za ufundishaji wa masuala ya madini zilizotolewa na kampuni hiyo kwa Chuo cha VETA Moshi. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai (kushoto) akipokea nyaraka mbalimbali kutoka kwa Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo (kulia) ambazo zinahusu zana za ufundishaji wa masuala ya madini zilizotolewa na kampuni hiyo kwa Chuo cha VETA Moshi.
Mmoja wa wanafunzi wanaopata mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA- Moshi akitumia moja ya zana zilizotolewa na kampuni ya GGML kwa chuo hicho kwa ajili ya kuboresha mbinu za ufundishaji kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya madini.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger