Thursday, 28 October 2021

HII HAPA ORODHA YA VIWANJA VYA NDEGE HATARI ZAIDI DUNIANI

...

Usafiri wa ndege ni usafiri pendwa na watu wengi kwa sababu ya kutumia muda mfupi safarini, huduma, mazingira na safari nzima mara nyingi huwa ya raha ukilinganisha na usafiri kama wa basi ama treni kwa nchi za Afrika.

Pamoja na uzuri wa ndege, usalama wa viwanja inavyotumia ni jambo linaloangaziwa sana.

Utafiti uliowahi kufanywa unaonyesha kwamba wakati wa kupaa ama kutua kwa ndege, kitakwimu ni hatari zaidi ukilinganisha na wakati mwingine wowote ikiwemo ndege ikiwa katikati ya safari angani. Kwa mujibu wa mtandao wa biashara wa businessinsider asilimia 49 ya ajali zote mbaya za ndege zimetokea wakati ndege zikiwa ziko katika harakati za mwisho mwisho za kutua na asilimia 14% zikiwa katika harakati za kupaa. Pamoja na sababu zingine za kiufundi za ndege husika na hali ya hewa, hali ya viwanja vya ndege huwa msingi wa usalama wa safari za ndege. Ifuatayo ni orodha ya viwanja 8 hatari zaidi vya ndege duniani.


8: Juancho E. YrausquinAirport (Uholanzi)

Uwanja wa ndege wa Juancho E. Yrausquin

Uwanja huu unapatikana katika kisiwa cha Saba huko Uholanzi, unafahamika kama kiwanja chenye njia fupi zaidi ya ndege duniani, yenye urefu wa mita 396 tu, ni kama urefu wa viwanja vinne vya mpira wa miguu.

Kwa sababu ya kuzungukwa na miamba mikubwa iliyopo mwanzo wa njia na mwisho wa njia ya kutua na kupaa kwa ndege, inafanya utuaji na upaaji wa ndege kuwa wa mashaka wakati wote. Mbali na hilo uwanja huu una miteremko mikali inayopunguza ufanisi wa ndege hasa kwenye kutua.


7: Wellington Airport (New Zeeland)

Nchi ya New Zealand ni moja ya nchi zenye milima na hali ya hewa tata ya upepo kutokana na ukaribu wake na kuzungukwa na milima na bahari. Uwanja wa ndege wa Wellington una njia moja tu yenye inayotumika na ndege wakati wa kutua na kupaa yenye urefu wa mita 2,500 na ambayo inaanzia majini na kuishia majini. Kwa maana inapoanzia kuna bahari na inapoishia kuna bahari. Uwanja huu umepewa jina la utani la uwanja wa ndege wa 'Upepo' kutokana na upepo mkali uliopo.

Mbaya zaidi, ili kufika katika eneo la uwanja kuna upepo mkali unatokana na milima iliyo umbali kiasi kutoka baharini kwa upande wa pili. Marubani wengi wanaeleza kuwa ni uwanja mgumu na hatari wakati wa kutua kwa ndege.

6: The Princesa JulianaAirport (Uholanzi)

Uwanja huu unapatikana katika kisiwa cha San Martín, karibu na fukwe ya umma ya Maho, Uholanzi ambapo watu wanaoogelea, hulazimika kuhimiliki upepo mkali na kumwagiwa michanga wakati ndege inapotua kwenye uwanja huo. Ili kutua na kupaa ndege hizo hupita katika anga la chini kabisa, karibu na vichwa vya watu.

Ni uwanja unaochukua abiria zaidi ya milioni 1.8 kwa mwaka, huku kukiwa na ndege zaidi ya 170 zinazofanya kazi kwa siku kupitia mashirika ya ndege zaidi ya 30 yanayotoa huduma kwenye uwanja huo.

5: ParoAirport (Bhutan)

Paro Airport

Ni marubani 17 tu wanaruhusiwa kutua katika uwanja huu wa ndege. Hata kama una uzoefu wa namna gani, si rahisi kutua katika uwanja huu. Marubani hawa wamepewa vibali maalumu kwa sababu ya hali ilivyo katika uwanja huu.

Ndege huruhusiwa kutua mchana tu tena kwa uangalifu mkubwa na kujiridhisha sana, kutokana na hali ya hewa kwenye eneo hilo lenye milima. Mawingu huathiri sana marubani wakati wa kutua.

Kwa mujibu wa mtandao wa simpleflying.com yapo mashirika mawili tu yanayoruhusiwa kutoa huduma ya usafiri wa ndege ikiwemo la taifa Royal Bhutan lenye ndege tano.

Awali uwanja huu ulijengwa kama kituo cha helkopta za Jeshi la India kwa niaba ya serikali ya kifalme ya Bhutan.


4: Courchevel Airport (Ufaransa)

Uwanja wa ndege wa Courchevel

Uwanja huu uko juu ya milima ukiwa na njia yenye urefu wa mita 518 inayojumuisha mteremko. Hakuna taratibu za utuaji zinazofahamika ikiwemo taa za kuongoza kutokana na hali ya hewa na milima iliyopo. Uzoefu hutumika zaidi kusaidia ndege kutua kwenye uwanja huo.


3: Cristiano Ronaldo (Madeira) Airport - Santa Cruz (Ureno)
Uwanja wa ndege wa Madeira

Madeira ndiko iliko asili ya mchezaji wa Machester United, Christiano Ronaldo na kwa kumpa heshima kijana wao, nahodha wa taifa hilo na mchezaji nyota kuwahi kutokea Ureno, uwanja huu kwa sasa unaitwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Christiano Ronaldo.

Uwanja huu umezungukwa na vilima vingi, hali inayopelekea kuwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya mara kwa mara. Ukiacha njia nyembamba ya ndege iliyopo ni moja ya maeneo yenye upepo mkali hasa futi chache kutoka ardhini unaokuja ghafla na kusababisha kuwa moja ya viwanja hatari vya ndege duniani.

Novemba 19, 1977, ndege aina ya Boeing 727-282 iliyokuwa inafanya safari zake kutoka Brussels kwenda Madeira ilianguka, baada ya kupitiliza kwenye njia ya ndege na kuanguka kwenye fukwe na kulipuka. Upepo na hali mbaya ya hewa ilikuwa chanjo na kusababisha abiria 131 kati ya 164 kupoteza maisha. Na baada ya ajali hii, Mamlaka za Ureno ziliongeza urefu wa njia hii, pamoja na hilo bado unasalia kuwa miongoni mwa viwanja vya ndege hatari zaid duniani.


2: ToncontinAirport (Honduras)

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toncontin

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toncontin huko Tegucigalpa , ambao tangu mwaka 1934 umekuwa ukipokea wasafiri zaidi ya 800,000 kwa mwaka. Uwanja huu upo karibu na milima na una njia ama barabara nyembamba inayotumika na ndege wakati wa kutua na kupaa.


Hali ya hewa katika eneo hili huendana na baridi pamoja na ukungu mzito, kutokana na hali hii, uwepo wa milima na wembamba wa njia ya ndege husababisha mazingira magumu ya ndege hasa wakati wa kutua. Rubani anapaswa kupaisha ndege haraka kwa sababu ya milima, vinginevyo ni rahisi kuigonga milima ama nyumba za watu ambapo kuna makazi mengi ya watu karibu na uwanja huo.

Zaidi ya ajali 10 zimerekodiwa kutokea Toncontin, ajali mbaya zaidi ni ile iliyotokea Oktoba 1985, wakati ndege moja ya abiria ilipogonga milima ikiwa kwenye harakati za kutua na kusababisha vifo vya watu 131.


1: Tenzin-Hillary Airport (Nepal)

Uwanja wa ndege wa Tenzin-Hillary

Uwanja wa ndege wa Tenzin-Hillary umezungukwa na miteremko mikali na milima mingi. Njia yake ya ndege ina urefu wa mita 526 ambapo mwanzo kuna ukuta na mwisho wa njia kuna korongo kubwa

Kwa mujibu wa mtandao wa Forbes mwaka 2019 uwanja huu ulitajwa kuwa hatari zaidi duniani.

Hatari ya uwanjani huu, ni ufupi wa njia yake, korongo na kuzungukwa na milima. Rubani akikosea kidogo hakuna namna ataweza kukwepa madhara yatakayotokea.

Hali ya hewa katika milima ya Himalaya karibu na uwanja huu, haitabiriki, ghafla tu inaweza kukawa na ukungu, mvua ama barafu na kufanya utuaji wa ndege kuwa wa hatari. Ni kawaida sana katika uwanja huu safari kuahirishwa, na hasa ndege zinazotoka mji wa Kathmandu.

Mara nyingi mchana kunakuwa na mawingu mazito na ndege nyingi zinalazimika kuwa na ratiba ya kusafiri alfajiri.

Moja ya ajali inayokumbukwa zaidi kutokea ilikuwa mwaka 2008 wakati ndege ya shirika la ndege la Yeti(Flight 103) ilipobamiza milima na kusababisha vifo vya abiria wote 16. Aliyepona alikuwa rubani pekee.

CHANZO - BBC
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger