Watu saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera, wakituhumiwa kuwaua wanandoa wawili kwa kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao, chanzo kikidaiwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 14 mwaka huu saa saba usiku katika Kijiji cha Mabale, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo.
Alisema kuwa wakati wanandoa hao wakiwa wamelala, mlango wa nyumba yao ulivunjwa na kuvamiwa na kundi la watu ambao hawakufahamika na kuanza kuwakata kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na kusababisha kupoteza maisha papo hapo.
Aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Elizeus Rubanie (35) na mke wake, Juliana Joseph (28).
"Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na baadhi ya wanaukoo kwa muda mrefu, uliotokana na kuachiwa eneo alilokuwa akiishi na babu yake, aliyehama kwa shinikizo la wanajamii waliomtuhumu kuwa ni mwizi," alidai.
Kamanda Malimi alidai kuwa baada ya babu huyo kuhama na kumwachia eneo hilo mjukuu wake, baadhi ya wanajamii waliungana na baadhi ya ndugu kwenye ukoo huo, hasa shangazi wawili wa marehemu, na kuanza kumsakama marehemu na familia yake na kumtolea vitisho.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Sophia Joseph (45), Joseph Magambo (47), Alphonce Karoli (37), Martine Makabe (36), Alex Leopord (44), Salvatory Mwiliza (38) na Aloyce Leopord (45).
Kamanda Malimi alidai upelelezi bado unaendelea ili kubaini watu wote waliohusika na tukio hilo, na kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment