Tuesday, 10 May 2016

SUKARI:KILO 622,000 ZAKAMATWA MOROGORO,RC DODOMA AAGIZA TANI 154 ZIUZWE KWA WANANCHI

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Suala la uhaba bandia wa sukari limeendelea kuitikisa nchi, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi nzuri baada ya kuwatia nguvuni wafanyabiashara wengine, waliohodhi bidhaa hiyo kinyume cha sheria huku ikiwamo kukamata kilo 622,000 za mfanyabiashara Haruni Zakaria mkoani Morogoro.

Mwishoni mwa wiki, mfanyabiashara huyo anayemiliki Kampuni ya Al Naeem, alikutwa akiwa ‘ameficha’ tani 4,579.2 za bidhaa hiyo katika maghala yake yaliyoko Tabata, Dar es Salaam. 
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wachunguzi wa taasisi hiyo na wa Jeshi la Polisi, walifanya ukachero wao katika maghala ya kampuni hiyo yaliyopo Mbagala na Tabata, Mei 5, mwaka huu.

Lakini siku chache baada ya kunasa sukari hiyo, kikosi kazi cha Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoa wa Morogoro kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Kebwe Steven Kebwe kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari, kimebaini kiasi cha kilo 622,000 za sukari zilizofichwa katika maghala mbalimbali yaliyomo mkoani humo. 
Dk Kebwe amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei kuweka ulinzi kwenye maghala hayo yaliyokutwa yameficha sukari hiyo na kuhakikisha inauzwa kwa bei elekezi, iliyowekwa na serikali kwa wananchi.

Pia alimwagiza kuwafikisha wafanyabiashara walioficha sukari hiyo mahakamani mara moja na kumsaka mfanyabiashara Sadick Yassin ambaye alifunga duka lake wakati wa ukaguzi na kutokomea kusipojulikana.

Mali ya Zakaria wa Dar
Akizungumza jana, Dk Kebwe alisema sukari hiyo imebainika kuwa ni mali ya mfanyabiashara mmiliki wa Kampuni ya Al Naeem Enterprises na kuhifadhiwa katika maghala mbalimbali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero (K1) tani 429, Kiwanda cha Sukari Kilombero (K2) tani 135 na katika Manispaa ya Morogoro tani 58.4, jumla kuwa ni tani 622.4

“Nimeunda kikosi kazi cha kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari katika maghala yao katika ukaguzi wa awali, jumla ya tani 622.4 za sukari zimebainika kwenye maghala mbalimbali na sukari yote iliyobainika ni mali ya Al-Naeem Enterprises na tayari maghala hayo yenye sukari yapo chini ya ulinzi wa vyombo vya dola,” alisema.

Licha ya kumwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kuweka ulinzi katika maghala hayo na kusimamia sukari hiyo inauzwa kwa bei elekezi ya serikali, pia alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakiki iwapo sukari hiyo imelipiwa kodi ya serikali.

Dk Kebwe pia aliwataka wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo, kutoa taarifa za wafanyabiashara au watu walioficha sukari ili hatua zichukuliwe mara moja dhidi yao. 
Kabla ya kuweka msimamo wa Serikali ya Mkoa dhidi ya wafanyabiashara dhalimu, Dk Kebwe na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa walifanya ziara ya kushtukiza ya kuhakiki upya maghala ya wafanyabiashara wa maduka ya jumla katika Manispaa ya Morogoro.

Katika ghala la Kampuni ya Sukari Kilombero lililipo mjini Morogoro lilikuwa na tani 58.4 za sukari ambayo ni mali ya Al Naeem Enterprises.
Msimamizi wa ghala hilo, Robert Charles alimfahamisha Mkuu wa Mkoa na timu yake kuwa sukari hiyo ipo kwa muda wa mwezi mmoja sasa baada ya kununuliwa na mfanyabiashara huyo kutoka kiwandani Kilombero.

Alisema sukari tani 58.4 iliyokutwa ndani ya ghala hilo ni mali ya mfanyabiashara Zakaria aliyeinunua kutoka kiwandani Kilombero na kuihifadhi hapo akisubiri kusafirishwa na kuwauzia wanunuzi wa jumla. 
Baadhi ya wauzaji wa maduka ya jumla waliokaguliwa na timu ya Mkuu wa Mkoa, Thabit Islam na Hassan Binzoo walisema hali ya upatikanaji wa sukari katika kipindi hiki ni mgumu kutokana na kuadimika ghafla.

Dar yanaswa nyingine
Katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, zimekamatwa tani 2,700 za sukari zikiwa zimefichwa katika ghala moja eneo la Mbagala. 
Akitoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Paul Makonda, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Photidas Kagimbo alisema sukari hiyo imekamatwa baada ya Rais kutoa agizo la kuwabaini wale wote walioficha sukari na kusababisha wananchi kuteseka kupata bidhaa hiyo.

Kagimbo alisema licha ya kukamatwa kwa sukari hiyo Manispaa hiyo bado inaendelea na msako ili kuwabaini na wafanyabiashara wengine waliohodhi bidhaa hiyo.

Msako mkali Kahama
Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Polisi imefanya upekuzi katika baadhi ya maghala ya kuhifadhia sukari na kuwabaini baadhi ya wafanyabiashara wanne wanaojihusisha na kazi hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Michael Nyange alisema wamefanya ukaguzi katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari, ambayo ni ya wafanyabiashara John Hango (walikuta mifuko miwili ya kilo 50), Nyorobi Kisabu (hakuna kilichokutwa), Mshaka Kaziro (hakuna kilichopatikana) na Alex Magina (mifuko 40, yenye kilo 50 kila mfuko). Alisema kazi hiyo itakuwa endelevu.

RC Dodoma aagiza iuzwe
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ameagiza tani 154 kuuzwa kwa wananchi kwa bei elekezi, huku akiwataka wafanyabiashara ambao bado wameficha sukari kuitoa mara moja kabla rungu halijawashukia.

Takukuru kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa walikamata na kuzifungia tani 154 za sukari katika ghala la mfanyabiashara Haidary Gulamali na sasa Rugimbana ametoa agizo la kufunguliwa kwa ghala hilo ili litoe huduma kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa akiwa amefuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa alisema wameamua kufungua ghala na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambao wanauhitaji mkubwa kwa sasa wa sukari.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger