Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata wasichana 15 katika nyumba iliyopo maeneo ya Ukonga, waliokuwa tayari kusafirishwa kwenda Oman kufanya kazi za ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Simon Sirro, alisema wasichana hao walikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa toka kwa msiri kuwa kuna mtu amewaweka wasichana kwa ajili ya kuwasafirisha.
Sirro alisema Polisi walifuatilia na kufika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakuta katika nyumba ya Hadija Mohamed (40) wakiwa wamegawanywa katika vyumba viwili.
Alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa mwanamke huyo anashirikiana na mwenzake Salma Habibu (43) mkazi wa Temeke kuwatafutia masoko nchini Oman na wao ni mawakala wanaoletewa kutoka mikoani na kuwapokea kwa ajili ya kuwasafirisha.
Aidha alisema watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Pia ametoa onyo kwa watu wenye tabia hiyo kuacha, kwani wasichana hao wakifikishwa nje ya nchi hufanyiwa vitendo vya kikatili na unyanyasaji.
0 comments:
Post a Comment