Friday, 13 May 2016

Chadema Waungana na CUF Kutomtambua Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza rasmi kutoitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inayoongozwa na Dk Ali Mohamed Shein. 

Mbali na kutoitambua Serikali hiyo, chama hicho kimesema leo kitatoa mkakati mzito wa namna ya kushughulikia suala la matangazo ya Bunge la Kumi na Moja kutoonyeshwa moja kwa moja (live) na televisheni.

Msimamo huo ulitangazwa kwa waandishi wa habari jana mjini Dodoma katika kikao cha pamoja kati ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, manaibu wake wawili, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar). 

Pia walitoa taarifa juu ya mambo yanayojadiliwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu (CC) kinachofanyika chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. 

Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Mwalimu alisema chama hicho hakitampa ushirikiano Dk Shein. 

“Kikao maalumu cha Kamati Kuu ya Chadema kilichoketi Jumatatu, tumefikia msimamo wa kutoitambua Serikali ya SMZ. Msimamo wa Maalim Seif Shariff Hamad ndiyo msimamo wetu,” alisema. 

Maalim Seif aliwania urais Zanzibar kupitia CUF katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta matokeo yake na kutangaza uchaguzi wa marudio ambao mgombea huyo na chama chake walisusia. 

“Hatutatoa ushirikiano kwa SMZ na katika kikao cha leo (jana) cha CC tutawasilisha azimio hilo.Hali ya kisiasa Zanzibar ni mbaya mbaya sana. Wazanzibari wanaelekea kununa,” alisema Mwalimu. 

Mwalimu alisema hawatafanya maandamano Zanzibar lakini hali itakuwa mbaya zaidi kwani Wazanzibari wengi wanaelekea kununa na kwamba hilo litasababisha hali mbaya zaidi.

“Hali ya Zanzibar si nzuri kama CCM wanavyoeleza.  Watu hawazikani, hawatembeleani tumerudi kulekule kama mwaka 1995 kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema. 

Mashinji alisema kikao hicho cha kamati kuu kitapokea taarifa kutoka kwa wabunge wa Chadema, kuhusu Bunge kutoonyeshwa ‘live’ na athari zake kwa wananchi. 

“Uhuru wa wananchi kupata habari litajadiliwa kwa kina. Sasa hivi Bunge letu liko gizani tunapata habari za kupapasa tu. Tutatoka na mkakati kabambe wa kushughulikia suala hili,” alisema.

Akizungumza hatua hiyo iliyochukuliwa na Bunge, Mnyika alisema kinachoonekana sasa ni kama chombo hicho kimetekwa na Serikali na hilo litatolewa tamko zito rasmi leo na Mbowe mwenyewe.

“Kuna mambo makubwa tuki- yawekea mkakati huwa Serikali inasalimu amri. Tunataka kutoka kwenye huu mkwamo ili Bunge lionyeshwe live,”alisema. 

Januari 27, Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitangaza Serikali kusitisha matangazo hayo ya moja kwa moja kama njia ya kubana matumizi. 

Waziri huyo aliliambia Bunge matangazo hayo yatarushwa vipande muhimu vya mijadala usiku katika kipindi maalumu cha Leo katika Bunge ambacho kitarushwa saa nne za usiku uamuzi ambao ulipingwa vikali ndani na nje ya Bunge. 

Leo, Nape atawasilisha bajeti ya wizara yake bungeni ambako mjadala mzito unaotarajiwa kulitikisa Bunge ni suala hilo la kutoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni. 

Wadau wa habari wamepiga kambi mjini hapa kujaribu kuishawishi Serikali na Bunge kubadili msimamo huo
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger