VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) leo imeivua nguo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) bungeni.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeeleza kwamba, Serikali ya CCM ina ufundi wa kupanga mipango mingi lakini haina uwezo wa kutekeleza na kwamba, kinachofanywa ni kudanganya wananchi.
Moja ya mambo yanayoonekana kukera upinzani ni pamoja na Serikali ya CCM kutotoa fedha za miradi kwa wakati jambo linalosababisha kukwama kwa mipango iliyopangwa.
Hayo yamesema na Wilfred Lwakatare wakati akitoa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo mjini Dodoma kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
“Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitengewa fedha iliyokuwa imeombwa na kupitishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2015/2016. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikuweza kuzifahamu, fedha zilizotengwa hazikuweza kutolewa kama ambavyo ilipangwa na kusababisha kukwama kwa mipango iliyokuwa imepangwa kufanyika,” amesema.
Lwakatare amesema, sababu ya kutotolewa fedha za miradi mapema na kwa wakati ni kitendo cha Serikali ya CCM kupanga mipango mingi kila mwaka na kwamba utekelezaji wake umekuwa duni.
“Mtiririko mkubwa na ahadi na mipango chungu nzima niliyoitaja na nyingine niliyoiacha ambayo ilipangwa na kuahidiwa na Wizara kutekelezwa katika kipindi cha Bajeti ya mwaka 2015/2016, utekelezwaji wake ndicho kinapaswa kuwa kipimo pekee cha utendaji wa Wizara hii,” amesema.
Amesema, serikali haina budi kutoa fedha za kutosha kwenye wizara hiyo kwa kuwa, ina majukumu mengi hasa kutokana na ongezeko la wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma zitolewazo na wizara hiyo.
“Majukumu ya Wizara hii ni makubwa na kuna ongezeko la wananchi waliowengi wanaohitaji huduma zaidi kutoka Wizarani.
“Katika mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, wizara imetengewa fedha ndogo zaidi ukilinganisha na fedha zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 ambacho ni kiasi cha shilingi 72,356,901,000/=ukilinganisha na kiasi cha shilingi 61,827,711,000/ kwa mwaka wa fedha 2016/2017,”amesema.
Lwakatare amesema kuwa bajeti iliyotengwa haitakidhi mahitaji ya wizara ya ardhi hasa kwa fungu dogo lililotengwa kwa ajili ya matumizi mengine(OC) na kwamba fungu hilo halitoshi kusimamia mipango ya maendeleo.
“Kwa jinsi bajeti ilivyotengwa ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa hali hii ni kuonyesha kujikwaa kabla ya safari kuanza. Fungu la OC ambalo limetengewa kiasi cha Tshs. 2,548,492,000 pekee ni dogo mno kuweza kusimamia mipango ya maendeleo,” amesema.
Amesema, licha ya fungu la matumizi mengine kugeuzwa kichaka cha kuendeshea ufisadi, ubadhirifu na matumizi yasiyo na tija, serikali inatakiwa kuendelea kutoa fungu hilo kwa kuwa miradi ya maendeleo husimamiwa na kuratibiwa na fungu hilo.
“Ni kweli kuwa kipindi cha nyuma fungu hili limekuwa likitumika kama kichaka cha kuendeshea ufisadi, ubadhirifu na matumizi yasiyo na tija. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa inapofikia hata kmaeneo muhimu yakanyimwa fungu hili, swali linabaki kwamba hiyo pesa inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo itasimamiwa na kuratibiwa vipi?” amehoji.
0 comments:
Post a Comment