Raza: Tuache utoto tujadili Katiba
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza ametaka wajumbe wenzake kuheshimiana bila kujali wingi au uchache wa wajumbe kwenye makundi yao, kama kweli wana dhamira ya dhati ya kutunga Katiba.
Akizungumza na gazeti hili, Raza alisema mwenendo
wa Bunge siyo mzuri na hauleti picha nzuri kwa mamia ya wananchi ambao
wanategemea wapatiwe Katiba bora itakayoondoa tatizo yao.
“Tupo hapa tunalipwa kwa siku Sh.300,000 na
tunajua huku nyuma kuna maelfu ya wananchi wetu hawana hata Sh.1000 ya
chakula, halafu tunakaa hapa tunafanya vurugu na kuacha kusikilizana
hata katika hoja za msingi? Nadhani hatuwatendei haki wananchi,” alisema
Raza.
Alisema hakuna asiyejua matatizo ya wananchi.
Kinachotakiwa sasa ni kukaa na kuanza kupitia Rasimu ya Katiba, hasa
baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba
kuiwasilisha bungeni.
Sarungi: Sikubaliani na rasimu mpya
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Maria Sarungi amepinga
utaratibu wa kuwasilishwa tena bungeni mabadiliko ya Kanuni ambayo
yataibua upya vurugu na hivyo vikao vya Bunge kuendelea kuahirishwa.
Sarungi kuwa kanuni ambazo
zilipitishwa kwa Azimio la Bunge Machi 11, zilitokana na kazi kubwa
iliyofanyika, ikiwepo vikao vya maridhiano.
“Tulikaa karibu mwezi mmoja kupitisha kanuni hizi
tena kwa maridhiano. Watu walikaa bungeni hadi usiku. Iweje leo hata
bado hatujaanza kuzitumia walete mabadiliko?” alihoji.
Alisema kitendo cha kurejesha mijadala ambayo
tayari ilipitishwa na Bunge ni kutaka kuibaua tena vurugu bungeni na
hivyo kupoteza fedha za umma.
“Nadhani Watanzania wanajionea watu ambao
wanakwamisha Bunge. Hapa kuna matumizi mabaya ya fedha. Kama tulipitisha
kila kitu wenyewe iweje leo walete tena mambo yale yale upya,” alisema
Sarungi.
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Rispa Miguma kutoka kundi la wateule 201 wa Rais, amesema kwa anayoyaona bungeni, hawezi hata siku moja kutamani kuwa mwanasiasa.
Mjumbe: Wanasiasa wamenisikitisha
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Rispa Miguma kutoka kundi la wateule 201 wa Rais, amesema kwa anayoyaona bungeni, hawezi hata siku moja kutamani kuwa mwanasiasa.
Alisema anachojifunza kutoka kwa wanasiasa
wanaoshiriki Bunge la Katiba kinamsikitisha kutokana na kugeuza chombo
hicho kuwa uwanja wa siasa badala ya mahala pa kuzungumzia masilahi ya
taifa.
“Badala ya kuangalia kitu ambacho wananchi walio
nje ya Bunge wanataka, mnatumia jina la wananchi, Watanzania eti
wamewatuma wakati hata kuzungumza nao wengine hamzungumzi nao,” alisema.
Miguma alitoa ujumbe wa maneno ya Mungu dhidi ya wanaotuhumiana kuhusika na vitendo vya rushwa katika shughuli hiyo akisema:
“Huu ni ujumbe kwa kundi la 201 hasa kwa wale
ambao wanahusika. Ujumbe wenu kwanza ni huu hapa, kwanza kabisa
usimshuhudie jirani yako uongo, pili inunue kweli na wala usiiuze, tatu
afichaye kosa atafuta kupendwa.”
Bunge livunjwe tukawaombe radhi wananchi- Mjumbe
Dodoma. Mivutano katika Bunge la Katiba imemchukiza mmoja wa
wajumbe wa chombo hicho, Michael Laizer ambaye amemshauri mwenyekiti
wake, Samuel Sitta amwombe Rais kuvunja Bunge.
Laizer pia amewataka wajumbe wenzake kurudi katika
maeneo yao ili wakaombe radhi kwa Watanzania kutokana na ufujaji wa
fedha unaotokana na kuwepo kwao kwenye vikao vya Bunge.
“Mwenyekiti narudia tena kama watu hawataki uamuzi
huu, nakushauri andika barua kwa Mheshimiwa Rais ili aje alivunje Bunge
na twende makwetu,” alisema Laizer.
Laizer alilishutumu Bunge hilo kuendelea kutafuna
fedha wakati watu wengine wanaishi maisha magumu zaidi kiasi cha
kushindwa kupata hata mlo mmoja kwa siku.
Alipinga muda ambao wametumia wajumbe hao kwa
ajili ya kujadili masuala ya kanuni pekee bila hata ya kufikia uamuzi,
akisema ndoto yake ni kuwa hadi wiki hii waanze kuchambua vifungu vya
katiba.
Aidha alisema watu wenye umri mkubwa kama yeye (Laizer) wanaogopa kuchangia hoja kutokana na tabia ya kuzomeana.
Vurugu zawa kero Dodoma
Dodoma. Kitendo cha kuahirishwa mara kwa mara kwa vikao vya
Bunge la Katiba kimewakera baadhi ya wakazi wa Mji wa Dodoma ambao sasa
wanapendekeza chombo hicho kivunjwe.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wakazi hao
walisema kuwa vurugu za bungeni zimewachosha na kuwafanya wakose hamu ya
kuangalia au kusikiliza mijadala.
Katibu wa uchumi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT)
mkoani Dodoma, Mary Chihoma alisema kwa hali ilivyo sasa, haya ni
matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
“Hatuwezi kusema ni mtu mmoja ndiye ambaye
anastahili kubeba lawama hizo. Hawa wote wanatakiwa kulaumiwa moja kwa
moja kwani wanakula kwa wasichokifanyia kazi,” alisema Chihoma.
Mwanasiasa huyo alitoa wito kwa wajumbe hao kumwogopa Mungu na kurudi kwenye mjadala wa msingi wa kutunga Katiba.
0 comments:
Post a Comment