Kura mchanganyiko Bunge la Katiba
Kwa ufupi
Mjumbe Vuai Ali Vuai alisema, wamefikia maridhiano
hayo, ili kuwezesha kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwani kila
upande uliendelea kutetea msimamo wake hata katika kikao cha maridhiano.
Dodoma.Wajumbe wa Kamati ya
Maridhiano jana walinusuru Bunge Maalumu la Katiba kuvunjika, baada ya
kukubaliana kutumika kwa utaratibu wa upigaji kura wa wazi na siri kama
ilivyopendekezwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Wajumbe hao walitangaza uamuzi huo bungeni
kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika kamati ndogo ya maridhiano
iliyofanyika jana asubuhi baada ya kushindwa kuafikiana katika kikao cha
awali kilichofanyika juzi kuanzia saa 3:00 usiku hadi usiku wa manane
ili kunusuru kukwama kwa Bunge hilo.
Kabla ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta alisema juzi usiku walikutana hadi usiku wa manane baada ya
hapo, walikabidhi kamati ndogo yenye mchanganyiko wa wajumbe kutoka
Kamati ya Kanuni na Kamati ya Maridhiano.
“Baada ya kukamilisha kazi, wajumbe wa kamati
ndogo watatoa taarifa hapa ambao ni John Mnyika, Profesa Ibrahimu
Lipumba, Vual Ali Vual na Askofu Donald Mtetemela,”alisema Sitta.
Akitoa taarifa ya maridhiano hayo, kwa niaba
Freeman Mbowe, Mjumbe John Mnyika alisema, alianza kwa kunukuu kitabu
kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere, mwaka 1962 chenye ujumbe mahususi kwa
Chama cha TANU akisema ujumbe huo kwa sasa ni sahihi kwa watu wengi na
taasisi ikiwamo CCM.
Mnyika pia alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) hawana nia yoyote ya kuvuruga mchakato wa katiba kama ambavyo
imeelezwa katika siku za karibuni na viongozi, kwani wazo la kutaka
Katiba Mpya imekuwa ni kilio chao cha muda mrefu.
Naye Profesa Lipumba alisema suala ambalo tumekuwa
tukisimamia kwa muda mrefu suala ambalo lina utata, kati ambao
wanapenda kura za uwazi na wale wa siri.
Alisema: “Tuliletewa mchanganyiko wa uwazi na
siri, lakini maana yake ni kura ya uwazi, wenzetu wamekuwa na msimamo
mkali hata hili la kufanya uamuzi ilikuwa tufanye kwa siri, lakini hata
hivyo hawakukubali.”
“Tulifanya uamuzi ili tusonge mbele, basi
tulipendekeza upigaji kura wa kuamua tupige kura kwa mfumo wa siri,
lakini pia wenzetu walikataa,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema kwa kuzingatia kutokwama kwa zoezi la kuanza kujadili rasimu, wameamua kukubali kutokubaliana.
“Ili kusonga mbele tunahitaji kusonga mbele tuanze
kujadili Katiba, natoa wito kwa wenzangu wa chama tawala kwa kuwa mpo
wengi mnadhamana kubwa, ni vyema mkawa na utaratibu wa kuwasikiliza
wachache,” alisema.
Mjumbe Vuai Ali Vuai alisema, wamefikia maridhiano
hayo, ili kuwezesha kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwani kila
upande uliendelea kutetea msimamo wake hata katika kikao cha maridhiano.
0 comments:
Post a Comment