MAELEZO YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/21
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma, kupokea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21. Wasilisho hili ni kwa mujibu wa Kanuni ya 97 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja amani na utulivu.
2. Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya Kwanza ni Tathmini ya Mwenendo wa Hali ya Uchumi; Sehemu ya Pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2020/21; na Sehemu ya Tatu ni Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
3. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Aidha, mapendekezo haya yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Katika kipindi hicho cha utekelezaji wa mpango, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
4. Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kipindi cha mwaka 2016 hadi mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka. Ukuaji huu ulichochewa na sekta ya ujenzi kufuatia kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za maji; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuimarika kwa shughuli za habari na mawasiliano; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Pato la Taifa umechangia kuongezeka kwa ajira 6,032,299, ambapo ajira 1,975,723 ni kutoka sekta rasmi na ajira 4,056,576 ni kutoka katika sekta isiyo rasmi.
5. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mojawapo ya malengo ya Serikali ya awamu ya Tano ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Moja ya nyenzo za kutekeleza lengo hilo ni kuzikwamua kaya masikini kutoka katika lindi la umasikini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Serikali imesaini mkataba na Washirika wa Maendeleo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 883.31.
6. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja wa wastani wa asilimia 4.4 kati ya mwaka 2016 na mwaka 2019. Kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020 mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.7 ambao uko ndani ya lengo la ukomo la mfumuko wa bei wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia 5. Mwenendo wa mfumuko wa bei nchini kwa mwaka 2019 uliendelea kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja kutokana na upatikanaji mzuri wa chakula, utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia na utekelezaji na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti.
7. Mheshimiwa Mwenyekiti, ujazi wa fedha umeendelea kukua kwa kasi kulingana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Katika mwaka 2019, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka na kufikia shilingi bilioni 28,313.1 kutoka shilingi bilioni 25,823.5 mwaka 2018, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.6, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.5 mwaka uliotangulia. Ukuaji huo unadhihirisha kuwepo kwa fedha za kutosha kuendesha shughuli za uchumi na kuongezeka kwa uwezo wa sekta ya kibenki kutoa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ujenzi na madini.
8. Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka na kufikia shilingi bilioni 19,695.4 mwaka 2019, kutoka shilingi bilioni 17,726.8 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 11.1, likilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.9 mwaka 2018. Ukuaji huo unaenda sambamba na muendelezo wa utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwenye uchumi, na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini. Aidha, kuimarika huko kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kumechangiwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu, ikiwemo kuboresha matumizi ya mfumo wa taarifa za wakopaji na kusimamia utekelezaji wa maadili bora kwa watumishi wa sekta ya kibenki katika kutoa mikopo.
9. Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida. Sekta hiyo pia imeendelea kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha unaowezesha kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Katika kipindi kilichoishia Desemba 2019, mtaji wa sekta ya kibenki uliongezeka na kufikia shilingi bilioni 4,102.7 kutoka shilingi bilioni 3,800.3 mwezi Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.0. Kiasi hiki cha mtaji wa msingi ni sawa na asilimia 16.8 ya rasilimali za benki ikilinganishwa na kiwango cha chini cha kisheria cha asilimia 10.0. Aidha, sekta ya kibenki ilipata faida ya shilingi bilioni 394.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 221.9 kutoka faida ya shilingi bilioni 122.6 iliyopatikana mwaka 2018. Amana za sekta ya kibenki zimekua na kufikia shilingi bilioni 23,807.0 mwaka 2019 kutoka shilingi bilioni 22,226.5 mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.1. Ongezeko hilo linaashiria kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi ikiwemo mikopo.
10. Mheshimiwa Mwenyekiti, ukwasi kwenye sekta ya kibenki umeendelea kuwa katika viwango vya juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 na kufikia asilimia 32.4 mwezi Desemba 2019. Aidha, rasilimali katika sekta ya kibenki ziliongezeka na kufikia shilingi bilioni 33,067.4 kutoka shilingi bilioni 30,374.0 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.9. Vile vile, ubora wa rasilimali za sekta ya kibenki uliimarika kama inavyodhihirishwa na kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu kutoka asilimia 10.7 Desemba 2018 hadi kufikia asilimia 9.8 ya mikopo yote Desemba 2019. Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupunguza uwiano wa mikopo chechefu ili kufikia lengo la asilimia 5. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na, kuzitaka benki na taasisi za fedha kuboresha usimamizi katika utoaji mikopo; kutekeleza mpango kazi wa kupunguza uwiano wa mikopo chechefu kwa benki zilizokuwa na uwiano mkubwa; na matumizi ya lazima ya taarifa za wakopaji zilizo kwenye kanzidata ya wakopaji kabla ya utoaji wa mikopo.
11. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi wengi wakiwemo waliopo vijijini, Benki Kuu imeruhusu benki kutoa huduma za kibenki kupitia kwa mawakala. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibenki kwa njia hii ambapo hadi kufikia Desemba 2019, benki 21 zilikuwa zinatoka huduma hiyo kwa kutumia mawakala ikilinganishwa na benki 17 zilizokuwa zinatoa huduma hiyo Desemba 2018. Aidha, Desemba 2019 kulikuwepo na mawakala 28,358 nchi nzima ikilinganishwa na mawakala 18,827 waliokuwepo Desemba 2018, likiwa ni ongezeko la asilimia 50.6. Kiasi cha amana kilichowekwa kwenye benki kupitia mawakala wa benki kilifikia shilingi bilioni 5,464.9 Desemba 2019 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 3,402.7 kilichokuwepo Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 60.6 wakati kiasi cha amana kilichochukuliwa kwenye benki kupitia mawakala kilifikia shilingi bilioni 1,833.1 Desemba 2019 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,051.1 Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 74.4.
12. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2019, riba ya amana ya mwaka mmoja ilifikia wastani wa asilimia 8.78 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 8.80 mwaka 2018. Aidha, riba za mikopo zilipungua kufikia wastani wa asilimia 16.97 mwaka 2019 kutoka asilimia 17.43 mwaka 2018. Vile vile, riba ya mikopo ya mwaka mmoja imepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.69 kutoka asilimia 18.25.
13. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2019, nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,623.0, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 2,204.6 mwaka 2018. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi, hususan, bidhaa asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu na bidhaa za viwandani. Kwa kiasi kikubwa, nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje yalifidiwa na mitaji mikubwa ya moja kwa moja na mikopo kutoka nje ya nchi.
14. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mauzo ya bidhaa na huduma nje, yalikuwa dola za Marekani milioni 9,712.6, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,398.3 mwaka 2018. Thamani ya mauzo ya bidhaa zisizo asilia iliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 4,236.6 mwaka 2019 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 3,209.3 zilizopatikana mwaka uliotangulia. Matokeo haya yalichangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji dhahabu sambamba na ongezeko la bei katika soko la dunia. Vilevile, mauzo ya bidhaa asilia yaliongezeka hadi dola za Marekani milioni 829.9 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani milioni 772.1 mwaka 2018, kutokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa za korosho, kahawa na pamba.
15. Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ilikuwa dola za Marekani milioni 10,984.8, sawa na ongezeko la asilimia 7.7 kutoka dola za Marekani milioni 10,197.8 mwaka 2018. Ongezeko hili lilichangiwa na uagizaji wa malighafi pamoja na mashine sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, barabara na uzalishaji umeme.
16. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2019, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,567.6, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.4. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kuwa na akiba ya kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4, ikiwa pia ni juu ya lengo lililokubalika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.
17. Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019. Hali hii ilitokana na utekelezaji mzuri wa sera ya fedha na ya kibajeti, pamoja na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje. Aidha, utulivu huo wa shilingi ya Tanzania ulichangiwa pia na hatua zilizotekelezwa na Benki Kuu katika kuhakikisha uwazi na utaratibu mzuri wa ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini. Utulivu wa thamani ya shilingi umechangiwa pia na utulivu wa mfumuko wa bei kubaki katika viwango vya chini hali iliyopelekea kuwa na utofauti mdogo wa mfumuko wa bei kati ya Tanzania na washirika wake wa biashara. Katika kipindi hicho, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,299.8 katika soko la fedha la jumla ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,275.4 mwaka 2018.
18. Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwezi Novemba 2018. Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo inaipa Benki Kuu nguvu na wajibu wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha (Microfinance Service Providers) waliogawanywa katika madaraja manne yaani benki za huduma ndogo za fedha (microfinance banks); watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana (nondeposit taking microfinance service providers); vyama vya akiba na mikopo (Savings and Credit Cooperative Societies); na vikundi vya kijamii (community microfinance groups).
19. Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki Kuu kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (Tanzania Cooperative Development Commission) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Local Government Authorities) imeanza utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha ikiwemo kusajili watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote. Aidha, Benki Kuu inashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika kuutekeleza mpango wa elimu kwa umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Public Awareness Programme on Microfinance Policy, Law and Regulations). Sheria na Kanuni hizi mpya zitasaidia kuimarisha mfumo wa taarifa za wakopaji, kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma ndogo za fedha ikiwemo riba kubwa na ukusanyaji wa madeni usiozingatia maadili. Sheria na Kanuni hizi pia zitasaidia kuongezeka kwa huduma jumuishi za fedha na elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wanaotumia huduma hizo.
20. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, itaendelea kutekeleza na kusimamia sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea kuwa imara, jumuishi na endelevu.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2019/20 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA
2020/21
A. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2019/20
21. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2019/20 jumla ya shilingi trilioni 12.25 zilitengwa kugharamia miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 9.74 zilikuwa fedha za ndani na shilingi trilioni 2.51 ni fedha za nje. Hadi Januari 2020, jumla ya shilingi trilioni 6.22 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo sawa na asilimia 71.9 ya lengo la shilingi trilioni 8.67. Aidha, Serikali imetumia shilingi trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana na mikopo iliyotumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni: mradi wa maji Arusha; mradi wa maji Ruvu chini; mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi, mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga; upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar; Mradi wa Kuboresha Huduma katika mji wa Zanzibar; Mradi wa Serikali Mtandao Awamu ya Pili Zanzibar; ujenzi wa Jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere; ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga na Mwanza; ukarabati wa reli ya kati; na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
22. Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio makubwa sana yamepatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2016/17 hadi Januari 2020 chini ya utawala wa Rais Magufuli na Serikali yake ya CCM. Naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla baadhi ya mafanikio ya kujivunia kama ifuatavyo:
(i) Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 75 na kwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 25. Hadi Septemba 2019, mradi huu umezalisha takribani ajira 13,117. Aidha, zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7 zimetolewa kwa wazabuni na makandarasi wa ndani 640. Jumla ya shilingi trilioni 2.96 zimetumika kugharamia mradi huu zikijumuisha shilingi bilioni 237.5 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(ii) Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - Mw 2,115: kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel) wenye urefu wa mita 147.6 kuelekea kwenye mtaro wa chini kwa chini wa kuchepua maji na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja ambapo utekelezaji wa mradi wote umefikia asilimia 10.74. Jumla ya shilingi trilioni 1.28 zimetumika kugharamia mradi huu ikijumuisha shilingi bilioni 200.7 ambazo zimetolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020. Mradi huu umezalisha ajira zipatazo 3,074 na kutoa fursa kwa makandarasi wa kampuni 10 za Kitanzania;
(iii) Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Serikai imeendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya 11 ambapo ndege nane (8) mpya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu
(3) yamefanyika ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400; kuongezeka kwa idadi ya vituo vya safari za ndani kufikia 13 na nje kufikia sita (6) ambavyo ni Hahaya (Comoro), Entebbe (Uganda), Bujumbura (Burundi), Mumbai (India), Lusaka (Zambia) na Harare (Zimbabwe). Aidha, Serikali imekamilisha ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA); na kugharamia mafunzo ya marubani (110), wahandisi (127) na wahudumu (125). Hadi Septemba 2019, mradi huu umezalisha ajira 436;
(iv) Miradi ya Umeme: Shughuli zilizotekelezwa ni: kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Makambako – Songea ambapo shilingi bilioni 160.1 zimetumika; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 63 na shilingi bilioni 219.4 zimetumika katika kipindi cha Julai 2016 hadi Januari 2020; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA ambapo jumla ya vijiji 8,641 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia 70.4. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020, jumla ya shilingi trilioni 1.53 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu ikijumuisha shilingi bilioni 207.2 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020; kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I Extension – (MW 185) ambapo ufungaji wa mitambo yote minne (4) umeanza; na kuendelea na upanuzi (upgrade) wa njia ya msongo wa KV 132 kutoka Kinyerezi I hadi kituo cha kupoza umeme cha Gongo la Mboto ambapo utekelezaji umefikia asilimia 85; na kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Rusumo (MW 80) ambao umefikia asilimia 60 na shilingi bilioni 9.4 zimetolewa kugharamia mradi huu;
(v) Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama vijijini na mijini ambapo utekelezaji wa miradi 875 unaendelea ikijumuisha miradi 802 ya maji vijijini na miradi 73 ya maji mijini ambapo miradi 75 ya maji vijijini imekamilika. Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na: mradi wa maji Arusha; mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe, ambapo katika mji wa Same utekelezaji umefikia asilimia 73 na Mwanga asilimia 38 na ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji umefikia asilimia 81; na mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega – Tabora – Igunga (km 290.7) umekamilika. Aidha, ulazaji wa mabomba ya matawi umefikia asilimia 86 na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mijini na vijijini umefikia asilimia 98.6. Hivyo, utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini kufikia asilimia 64.8, katika miji ya mikoa asilimia 84, Dar es Salaam asilimia 85 na katika miji midogo asilimia 64. Jumla ya shilingi bilioni 146.7 zimetolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(vi) Miradi ya Afya: Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo 540 vya kutolea huduma za afya ikijumuisha vituo vya afya 361, hospitali za halmashauri za wilaya 71, hospitali za zamani 9 na zahanati 99 ambapo watumishi 477 wameajiriwa na kupangwa kwenye vituo hivyo. Aidha, Serikali imefanikisha ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa katika hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), Burigi - Geita, Mwananyamala – Dar es Salaam na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika hospitali ya Taifa Muhimbili. Vile vile, madaktari 646 wamegharamiwa mafunzo ya kibingwa kwenye fani mbalimbali katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi; na kukamilika kwa nyumba 320 za watumishi wa sekta ya afya. Katika mwaka 2019/20 vituo vya afya 133 vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 64.64; na katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020 jumla ya shilingi trilioni 3.01 zimetumika kugharamia huduma za afya ikijumuisha shilingi bilioni 14.5 zilizotumika kununua mashine ya Positron Emmission Tomography (PET scan) kwa ajili ya hospitali ya Ocean Road;
(vii) Miradi ya Elimu: mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia; kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja pamoja na hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana nchini ambapo jumla ya shilingi bilioni 371.2 zimetolewa kugharamia shughuli hizo; na shilingi bilioni 9.1 zimetolewa kugharamia ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa shule za msingi. Aidha, kupitia programu ya EP4R yamenunuliwa magari 39 na kusambazwa katika vyuo vyote vya ualimu vya Serikali, kukamilika kwa taratibu za ununuzi wa magari 65 kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora wa shule pamoja na magari matano (5) na Malori mawili (2) kwa ajili ya Baraza la Mitihani la Taifa. Elimumsingi Bila Ada: Serikali imeendelea kugharamia posho ya madaraka kwa walimu wakuu; fidia ya ada kwa wanafunzi 1,874,331 na ruzuku ya uendeshaji wa shule ambapo shilingi bilioni 145.6 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada;
(viii) Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III): Serikali imendelea na utekelezaji wa mkakati wa uwezeshaji wa kaya maskini kiuchumi, ambapo kwa sasa inatekeleza Awamu ya III ya TASAF. Jumla ya kaya 1,067,041 zenye wanakaya 5,130,001 zimetambuliwa na kuandikishwa katika vijiji na mitaa 9,627 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 32,248 zenye wanakaya 169,999 katika shehia 204 za Zanzibar na ruzuku ya fedha shilingi bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya hizo, shilingi bilioni 935.94 ni kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar. Kazi nyingine zilizofanyika ni: kutekelezwa kwa miradi 8,384 ambayo imezalisha ajira za muda kwa kaya zipatazo 230,738 katika Halmashauri 42 Tanzania Bara na kaya 14,555 katika miradi 251 kwa Zanzibar; kuundwa kwa vikundi vya kuweka akiba 16,366 vyenye wanachama 226,050 kwenye halmashauri 44 Tanzania Bara ambavyo vimeweka akiba ya shilingi bilioni 2.5 na kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.13. Aidha, vikundi 1,957 vyenye wanachama 27,398 Zanzibar vimeweka akiba ya shilingi bilioni 1.1 na shilingi milioni 628.0 zimekopeshwa. Vile vile, miradi 47 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji Tanzania Bara na miradi 8 katika sekta za elimu na afya kwa Zanzibar imekamilika.
(ix) Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Katika sekta ya Kilimo zimezalishwa na kusambazwa tani 10 za mbegu mpya za mpunga kwa wakulima 3,050; kusambazwa mbolea tani 492,394.2 katika mikoa yote ya Tanzania Bara; kununuliwa na kuhifadhiwa tani 3,841.9 za mahindi kupitia wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA); na kuzalisha miche 3,692,780 ya kahawa na kusambaza mbegu bora za korosho zitakazozalisha miche 6,647,760. Mifugo: baadhi ya mafanikio ni pamoja na kuendelezwa kwa mashamba matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya Paranex ya kuogesha mifugo; na kukarabatiwa kwa majosho 1,129 na utoaji wa chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Jumla ya shilingi milioni 892.9 zilitolewa kugharamia miradi hiyo ikijumuisha shilingi milioni 154.7 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020. Uvuvi: mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na upandikizaji wa vifaranga 18,700 na uzalishaji wa vifaranga 15,041,401 vya samaki; kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya uvuvi; kupungua kwa uvuvi haramu kwa asilimia 80 kwa maji baridi na asilimia 100 kwa uvuvi wa milipuko katika mwambao wa Bahari ya Hindi; kununuliwa kwa mtambo wa automatic identification system wenye uwezo wa kuona meli zinazoingia na kuvua katika ukanda wa uchumi wa bahari kuu; na kuongezeka kwa uvunaji wa samaki (maji ya asili) kutoka tani 448,400 hadi tani 470,309.23;
(x) Uendelezaji wa Viwanda: kazi zilizotekelezwa ni upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani) ili kuongeza uzalishaji ikiwemo magari ya zimamoto; kufutwa na kupunguzwa kwa ada na tozo 54 ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji; kuzinduliwa na kuanza uzalishaji katika viwanda saba (7) ambavyo ni kiwanda cha Pipe Industries Co. Limited (Dar es Salaam), kiwanda cha chai cha Kabambe (Njombe), kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd (Mikindani – Mtwara), kiwanda cha 21st Century Food and Packaging (Dar es Salaam), kiwanda cha kusaga mahindi cha kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited – MeTL (Dar es Salaam), kiwanda cha bidhaa za plastiki cha Plasco Pipelines Co. Ltd (Dar es Salaam), kiwanda cha kupakia na kuhifadhi parachichi - Rungwe Avocado (Mbeya) na kiwanda cha kuchakata parachichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta (KUZA Afrika). Aidha, jumla ya tani 4,254.1 za korosho zilibanguliwa kupitia viwanda 17 na kuwezesha kuzalishwa kwa fursa za ajira za moja kwa moja 4,066.
Kwa kipindi cha mwaka 2016/17 - 2019/20, jumla ya viwanda vikubwa 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410 vilianzishwa.
(xi) Madini: Serikali imepitia na kurekebisha sera, sheria na mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini ambapo marekebisho hayo yamewezesha kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); kuanzishwa kwa masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini; na kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; na kukamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Mpango wa Utunzaji wa Mazingira. Katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi Februari 2020, jumla ya shilingi trioni 1.18 zilikusanywa kutokana na maduhuli kwenye sekta ya madini, sawa na wastani wa shilingi bilioni 294.41 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 142.53 tu kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2010/11 hadi 2014/15. Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa asilimia 106.6. Mfaninkio haya ni matokeo ya hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha sekta ya madini ili kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake;
(xii) Ujenzi wa Barabara na Madaraja: Katika ujenzi wa Barabara shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na wilaya ambapo hadi Desemba 2019 mtandao wa barabara kuu umefikia km 8,671 na mtandao wa barabara za mikoa km 1,808; barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19) umefikia asilimia 63; na ujenzi wa Ubungo Interchange ambao umefikia asilimia 65. Madaraja: Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa mita 3,200 na upana wa mita 28.45 ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 61.4 yamefanyika; ujenzi wa daraja jipya la Selander unaendelea na umefikia asilimia 25; ujenzi wa madaraja yafuatayo ya Mfugale na Mlalakuwa (Dar es Salaam), Magufuli katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti (Singida), Mara (Mara), Ruhuhu (Ruvuma), Msingi (Singida), Lukuledi (Lindi) na Kavuu (Katavi). Aidha, ujenzi unaendelea wa madaraja ya Mangara (Manyara) asilimia 94, New Wami (Pwani) asilimia 35; na Kitengule (Kagera) asilimia 42. Jumla ya shilingi trilioni 3.60 zimetolewa katika kipindi cha Novemba 2015 hadi Januari 2020 kugharamia miradi ya barabara na madaraja ikijumuisha shilingi bilioni 703.6 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(xiii) Ujenzi wa Meli na Vivuko: mafanikio yaliyopatikana ni kukamilika kwa ujenzi wa meli mpya ya MV Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika Ziwa Nyasa; kuendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji umefikia asilimia 52 na ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 80; ukarabati wa meli ya MV Victoria umefikia asilimia 75 na MV Butiama asilimia 70; awamu ya kwanza ya upanuzi wa maegesho ya Magogoni - Kigamboni imekamilika; jengo la abiria na ofisi ya kivuko cha Lindi – Kitunda limekamilika na kukabidhiwa; vivuko vya MV Kigamboni, Kigongo – Busisi na MV Utete pia vimekamilika na tunaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vya Nyamisati - Mafia (asilimia 28), Bugolora - Ukara (asilimia 40), Chato - Nkome na Kayenze Bezi (asilimia 98); shughuli nyingine ni kununuliwa kwa kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 170 (Magogoni - Kigamboni); kuendelea na ukarabati wa vivuko vya MV Sengerema (asilimia 70) na MV Misungwi (asilimia 20). Jumla ya shilingi bilioni 81.5 zimetumika kugharamia ujenzi na ukarabati wa meli na vivuko ikijumuisha shilingi bilioni 38.8 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(xiv) Viwanja vya Ndege: Jengo la III la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere lilikamilika na kuanza kutumika ambapo shilingi bilioni 722.1 zimetumika kugharamia mradi huu; ujenzi na uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Mwanza umefikia asilimia 99.5; uboreshaji wa kiwanja cha Nachingwea umekamilika; ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34) unaendelea. Jumla ya shilingi bilioni 10.9 zilitolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020 kugharamia miradi hiyo;
(xv) Uendelezaji wa Bandari: ujenzi wa gati Na.1, 2, 3 na gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) katika bandari ya Dar es Salaam umekamilika ambapo meli yenye uwezo wa kubeba magari 6,000 imehudumiwa; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika bandari ya Mtwara umefikia asilimia 60; na ukarabati wa gati namba 2 na kuongeza kina cha bandari ya Tanga unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 60;
(xvi) Ukarabati wa Reli: Serikali imendelea na ukarabati wa reli ya kati ikijumuisha njia ya reli, madaraja na ujenzi wa makalavati kwa vipande vya Dar es Salaam – Ngerengere (km 145) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 89.14, Ngerengere - Kilosa (km 138) asilimia 59.43, Kilosa - Itigi (km 343) asilimia 82.57 na Itigi - Isaka (km 344) asilimia 82.05; ukarabati wa reli ya Tanga – Arusha (km 439) umeendelea ambapo ukarabati wa kipande cha reli ya Tanga – Moshi (km 353) umekamilika na kuanza kusafirisha abiria na mizigo; na ukarabati wa kipande cha Moshi – Arusha (km 86) umeendelea kwa kubadili reli na mataruma, kurejesha madaraja na makalavati, kukarabati stesheni na kufungua mifereji ya maji ya mvua ambapo utekelezaji umefikia asilimia 90;
(xvii) Rada za Kuongozea Ndege na za Hali ya Hewa: miundombinu ya rada, na ufungaji wa mitambo umekamilika, majaribio ya mitambo kwa rada za kuongozea ndege za kiraia yanaendelea katika viwanja vya ndege vya JNIA, KIA na Mwanza; malipo ya ununuzi wa Rada tatu (3) za hali ya hewa zitakazofungwa Mtwara, Mbeya na Kigoma yamefanyika kwa asilimia 90. Jumla ya shilingi bilioni 17.8 zimetolewa kugharamia miradi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2016/17 hadi Januari 2020;
(xviii) Miradi ya Mahakama: Serikali imekamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu Kigoma na Mara, majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi Manyara, Simiyu na Geita na majengo ya mahakama za wilaya za Longido, Chato, Bukombe, Bariadi, Njombe, Ruangwa, Kilwa, Chunya na Kondoa; ujenzi wa nyumba nne (4) za Majaji (Kigoma 2 na Musoma 2) umekamilika; na tunaendelea na ukarabati mkubwa wa Mahakama Kuu Sumbawanga. Jumla ya shilingi bilioni 28.6 zimetolewa kugharamia miradi hiyo ikijumuisha shilingi bilioni 3.5 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;
(xix) Udhibiti wa Uhalifu na Utoaji Haki: Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kushirikiana na wadau, imeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri ya Mahakama kutaifisha jumla ya kilo 398.145 za Dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 32.30 zilizokuwa zinatoroshwa. Madini mengine yaliyotaifishwa ni madini ya bati na madini vito aina ya Almasi, Tanzanite, Amethyst, Rhodolite, Blue Sapphire, grossularite, Tsavorite, Green Garnet, Spessartite, Cintrine, Grossular, Supphire, Spinel, Ruby, Tourmaline na Acuamarine. Jumla ya thamani ya madini yote pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa ni shilingi bilioni 42.27. Aidha, shilingi bilioni 17.22 zimetaifishwa kutoka kwa wahalifu mbalimbali na kuwekwa kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery iliyoko Benki Kuu ya Tanzania. Vile vile, jumla ya shilingi bilioni 13.52 zimelipwa kutoka kwa washitakiwa waliokiri makosa yao (plea bargain) ya ukwepaji kodi. Hivyo, hadi Januari 2020 jumla ya shilingi bilioni 73.0 zililipwa kutokana na makosa mbalimbali. Pamoja na fedha hizo, Serikali imepata amri ya kutaifisha nyumba 24 , magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6,894, Jahazi 1, XRF mashine mbili (2) za kupima ubora wa madini.
Kadhalika, katika kusimamia utawala wa sheria, washtakiwa (mahabusu) 2,812 wamefutiwa kesi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika zoezi la ukaguzi wa magereza na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu.
(xx) Kanda Maalum za Kiuchumi: Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo (SEZ): kumefanyika uwekezaji wa viwanda 11 ambavyo ni Seif for Tobacco Trade Limited, Fujian Hexingwang Industry Company Limited, Siparcoci International Limited, Hua Teng Metalugical Company Limited, Wegmar Paking Limited, Jambo Food Products Limited, Phiss Tannery Limited, Tube Limited, Ramky Tanzania Limited, Tanfroz Limited, na Africa Dragon Enterprises Limited. Kati ya viwanda hivyo, viwanda viwili (Africa Dragon Enterprises Limited na Phiss Tannery Limited) vimekamilika na kuanza uzalishaji na kutoa ajira 120 za moja kwa moja na ujenzi wa viwanda 9 unaendelea. Vile vile, andiko la uendelezaji na makisio ya gharama za kuweka miundombinu wezeshi katika eneo lililolipiwa fidia limekamilika. Eneo Maalum la Uwekezaji Kigoma: shughuli zilizotekelezwa ni kukamilika kwa upembuzi yakinifu na Mpango Kabambe wa uendelezaji wa eneo (Master Plan) na ugawaji wa viwanja kwa ajili ya wawekezaji; kazi nyingine ni kuendeleza miundombinu kwa kufungua barabara zenye jumla ya km 28.46 na kuweka alama za mipaka 106; kupatikana kwa kampuni tatu zitakazowekeza katika ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa jua (Next Gen Solowazi Limited), ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki
(Third Man Limited) na ujenzi wa ghala na kiwanda cha kuchakata zao la michikichi (SGC Investment Limited);
(xxi) Kuhamia Dodoma: Watumishi 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma; ujenzi wa awali wa Ofisi za Serikali katika mji wa Serikali, Mtumba umekamilika; maandalizi ya ujenzi wa majengo ya ofisi awamu ya pili na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami (km 40) katika mji wa Serikali Mtumba unaendelea;
(xxii) Biashara Ndogo: Serikali imesajili wajasiriamali wadogo milioni 1.55 ambapo jumla ya shilingi bilioni 31.02 zimepatikana. Mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya wajasiriamali waliosajiliwa ni pamoja na Dar es Salaam (asilimia 11.6), Arusha (asilimia 6.4), Mwanza (asilimia 5.3) na Mbeya (asilimia 5.2); na
(xxiii) Mafunzo kwa Vitendo: yametolewa mafunzo ya uanagenzi (miezi sita) kwa vijana 5,875 katika vyuo 17 nchini; mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa elimu ya juu 2,297 mahali pa kazi katika fani mbalimbali ambapo kati ya hao wahitimu 890 wameajiriwa katika kampuni na taasisi mbalimbali na wengine kujiajiri; kuwagharamia vijana 100 mafunzo kuhusu kilimo cha kisasa nchini Israeli; na kutolewa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kupitia watathmini kutoka vyuo vya ufundi visivyomilikiwa na VETA (asilimia 65), watathmini kutoka vyuo vya VETA (asilimia 31) na watathmini kutoka maeneo ya kazi hususan Viwandani (asilimia 3). katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020 shilingi bilioni 10.5 zimetolewa kugharamia mafunzo hayo.
23. Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio ya kishindo yanayoonekana nchini kote na yamepatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi . Hivyo, napenda kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Waheshimiwa Wabunge wote waliopigia kura ya NDIYO bajeti ya Serikali na Watanzania wote kwa kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi kulikopelekea mafanikio haya ya kihistoria kwa kipindi kifupi cha miaka minne tu. Asiye na mwana aeleke jiwe!
B. MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21
24. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni:
(i) Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili inalenga kujenga viwanda vinavyotumia kwa wingi malighafi zinazopatikana nchini zikiwemo za kilimo, madini na gesi asilia ili kukuza mnyororo wa thamani. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia, Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi na Kongane za Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu. Aidha, Mpango utaweka mkazo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo na zana za kilimo na uvuvi, huduma za ugani na utafiti, uimarishaji wa malambo na majosho, ujenzi wa maghala na upatikanaji wa masoko ya mazao na mifugo ndani na nje ya nchi;
(ii) Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma za maji safi na salama. Shughuli za miradi zitakazotekelezwa ni pamoja na kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha huduma ya maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ununuzi na usambazaji wa dawa, ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini, kuimarisha huduma za ubora wa maabara za maji, kuboresha huduma za maji mijini na vijijini na kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi;
Vile vile, katika Awamu ya Tatu, kipindi cha pili cha TASAF (2020-2023) itakayotekelezwa kwenye Halmashauri zote 185 na Wilaya zote 11 za Zanzibar itatumia kiasi cha shilingi trilioni 2.032. Asilimia 60 ya fedha hizo sawa na shilingi trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takriban 30,000 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania bara na shehia 388 Zanzibar.
Miradi hiyo itahusu sekta za afya (sh. bilioni 121.736), elimu (sh. bilioni 365.209), maji (sh. bilioni 585.937), barabara (sh. bilioni 49.668) na mazingira (sh. bilioni 96.416). Kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini ambapo ajira milioni 1.2 zitazalishwa na kuwapatia walengwa ujuzi pamoja na stadi za kazi.
(iii) Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na
Uwekezaji: Miradi itakayotekelezwa inalenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, barabara, madaraja, viwanja vya ndege na bandari) na ununuzi na ukarabati wa ndege, meli na vivuko pamoja na uanzishwaji wa Kanda Maalumu za Kiuchumi. Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; na kuendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Nchini; na
(iv) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango: Eneo hili linalenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za utekelezaji wa Mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango; kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha
kwa maandalizi, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya miradi; na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji. Vile vile, Serikali itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/21
A. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20
25. Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, iliyoidhinishiwa ina jumla ya shilingi trilioni 33.11, ikijumuisha shilingi trilioni 20.86 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
26. Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mapato ya ndani yalitarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05. Kati ya mapato hayo, Serikali ililenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 19.10, mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 3.18, na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 765.5. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, mapato ya ndani yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 11.87, sawa na asilimia 92.3 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 12.86 katika kipindi hicho. Kati ya makusanyo hayo, mapato yanayokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa ni shilingi trilioni 10.62, sawa na asilimia 96.9 ya makadirio ya shilingi trilioni 10.96 katika kipindi hicho.
27. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa kukusanya mapato ya kodi umeimarika na kufikia asilimia 96.9 ya lengo ikilinganishwa na ufanisi wa asilimia 88.6 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, sawa na ukuaji wa asilimia 16.6. Sababu za ongezeko la mapato yaliyokusanywa na TRA ni pamoja na: kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya walipakodi; wananchi kuhamasika kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu wezeshi ya barabara na umeme. Sababu nyingine ni kuendelea kuongezeka kwa uwazi katika usimamizi wa sheria za kodi, maboresho ya huduma kwa mlipakodi, usimamizi wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki hususan kwenye sekta ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, kuendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kuwashirikisha kikamilifu na kuwaelimisha ipasavyo wale wote ambao wamekuwa wakibainika kukwepa kodi.
28. Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato ya kodi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza makusanyo zaidi. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na: kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kodi; kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti unatumika ipasavyo; kuendelea na utoaji wa elimu kwa mlipakodi na dhana ya “Ukinunua Dai Risiti na Ukiuza Toa Risiti”; kuendelea kuongeza kasi katika utatuzi wa pingamizi za kodi; kuendelea kusimamia matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki (ETS) katika bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa, na kupitia nyaraka za walipakodi kwa lengo la kufanya usuluhishi wa kodi walizolipa kwa kujikadiria wao wenyewe ikilinganishwa kiasi halisi walichopaswa kulipa kwa mujibu wa Sheria.
29. Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yasiyo ya kodi yaliyokusanywa na
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali yalikuwa shilingi bilioni 835.3. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilikusanya shilingi bilioni 412.6, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio ya shilingi bilioni 457.4 kwa kipindi hicho.
30. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla ya shilingi trilioni 1.58, sawa na asilimia 95.2 ya makadirio ya shilingi trilioni 1.66. Kiasi hicho kimeongezeka kwa asilimia 46.6 ikilinganishwa na kiasi kilichopokelewa Julai 2018 hadi Januari 2019. Ongezeko hilo linatokana na utekelezaji madhubuti wa Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo -
DCF pamoja na kuongezeka kwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
31. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Januari 2020, Serikali imefanikiwa kukopa shilingi trilioni 3.04 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 100.9 ya lengo la shilingi trilioni 3.01. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 2.23 zilitumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na shilingi bilioni 806.8 zilitumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Mwenendo wa upatikanaji wa fedha kutoka soko la ndani umeimarika kutokana na: Kuongezeka kwa ukwasi kwenye benki za kibiashara; Serikali kuendelea kutoa matangazo ya minada ya dhamana za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki katika kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali.
32. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Januari 2020, kiasi cha shilingi trilioni 1.82 sawa na dola za Marekani milioni 800 kimepatikana kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo (Trade and Development Bank-TDB) kiasi hicho ni asilimia 98.3 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 1.85 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara. Aidha, kiasi kilichobaki cha dola za Marekani milioni 200 kinatarajiwa kupatikana kutoka benki hiyo. Vile vile, Serikali imesaini mikataba minne (4) ya mkopo wa dola za Marekani milioni 1,460.0 (takribani shilingi trilioni 3.33) ambao unaratibiwa na Standard Chartered Bank ambapo asilimia 68.0 ya mkopo huo ni kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo (Export Credit Agency - ECA).
33. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi kwa mwaka 2019/20, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 20.86 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi yenye jumla ya shilingi trilioni 18.27 (ikijumuisha fedha za Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kiasi cha shilingi trilioni 1.20), sawa na asilimia 94.1 ya lengo la shilingi trilioni 19.41. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 12.05 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 97.6 ya lengo la shilingi trilioni 12.34 na shilingi trilioni 6.22 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 71.9 ya lengo la shilingi trilioni 8.67. Aidha, Serikali imetumia shilingi trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana na mikopo iliyotumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni: mradi wa maji Arusha; mradi wa maji Ruvu chini; mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi, mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga; upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar; Mradi wa Kuboresha Huduma katika mji wa Zanzibar; Mradi wa Serikali Mtandao Awamu ya Pili Zanzibar; ujenzi wa Jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere; ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga na Mwanza; ukarabati wa reli ya kati; na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
34. Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa bajeti katika kipindi kilichobakia unatarajiwa kufikia malengo yaliyopangwa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itahakikisha kuwa mfumo wa usimamizi wa Mashine za Kielektroniki za kutolea risiti unatumika ipasavyo ili kuziba mianya ya uwezekano wa kugushi risiti; na kuendelea na kampeni za kuhamasisha utumiaji sahihi wa mashine hizo na dhana ya “Ukinunua dai risiti na ukiuza toa risiti”. Vile vile, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa Mafungu yote kwa kuwianisha mapato na matumizi na kipaumbele kitakuwa katika mahitaji yasiyoepukika pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati.
B. SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/21
35. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kuweza kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati. Katika kufanikisha azma hii, sera za mapato kwa mwaka 2020/21 zitajielekeza kwenye maeneo yafuatayo: kuendelea kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi; kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari pamoja na upanuzi wa wigo wa kodi; kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA; kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji; kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania – DCF; na kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu na mikopo inayotolewa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo.
36. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Sura 439, Sheria ya Fedha za Umma Sura 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 na Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410. Lengo kuu ni kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mingine muhimu. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la uzalishaji wa madeni ya Serikali.
C. Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2020/21
37. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, jumla ya shilingi trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21 yamezingatia mahitaji halisi ya ugharamiaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ulipaji wa mishahara na deni la Serikali pamoja na utekelezaji wa vipaumbele vingine vya Taifa. Mapendekezo ya kiwango na ukomo yanajumuisha: mapato ya ndani ya shilingi trilioni 24.07 sawa, na asilimia 69.0 ya bajeti yote; mikopo ya ndani shilingi trilioni 4.90; mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 3.04 na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi trilioni 2.87, sawa na asilimia 8.2 ya bajeti yote.
38. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 21.98 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.90 za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote. Bajeti ya maendeleo inajumuisha shilingi trilioni 10.16 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.8 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 2.74 fedha za nje. Matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
39. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2020/21 ni kama ilivyo katika Jedwali lifuatalo:
HITIMISHO
40. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/21 unazingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini na uongozi thabiti wa Mheshimwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii. Aidha, bajeti ya mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezajiwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Hivyo, bajeti hii itaendelea na utekelezaji wa maeneo makuu manne yaliyoainishwa katika Ilani ambayo ni: Kuondoa umaskini; kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana; kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma; na kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao.
41. Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kugharamia shughuli za Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika miradi ya maendeleo. Lengo kuu ni kupata thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
42. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu, mwezi Oktoba mwaka huu tutafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo. Napenda kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania wote washiriki uchanguzi huu muhimu na wazingatie umuhimu wa kuendelea kudumisha amani ya nchi yetu. Kila anayehusika atekeleze wajibu wake kulingana na nafasi yake tukianzia kwa viongozi wa madhehebu ya dini, wagombea wa nafasi mbalimbali, wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama, wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya habari na hata waangalizi wa kimataifa watakaokuwepo nchini wakati huo. Napenda kuwahakikishia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi utazingatia haki na utafanyika kwa usalama, amani na utulivu wa hali ya juu.
43. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.