Kesi ya kwanza ya ugonjwa wa Corona (Covid-19) imeripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku virusi hivyo hatarishi vikiendelea kusambaa katika maeneo mbali mbali duniani.
Wizara ya Afya ya Kongo DR imesema mtu anayeshukiwa kuwa na ugojwa huo ni raia wa Ubelgiji aliyeingia nchini humo siku chache zilizopita, na kwamba kwa sasa amewekwa chini ya uangalizi maalumu hospitalini katika jijini la Kinashasa.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Morocco imetangaza habari ya kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Corona katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Taarifa ya wizara hiyo imesema, aliyeaga dunia kwa Corona ni mwanamke aliyekuwa na umri wa 89, raia wa nchi hiyo ambaye alikuwa anaishi Italia na alirejea nchini humo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari.
Burkina Faso hapo juzi pia ilitangaza kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Corona na kuingia katika orodha ya nchi chache za chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika kuripoti kesi za ugonjwa huo; nchi zingine zikiwa ni Senegal, Togo, Cameroon, Afrika Kusini, na Nigeria.
Nchi kadhaa za kaskazini mwa Afrika kama Tunisia, Algeria, Morocco na Misri zimeripoti visa kadhaa vya ugonjwa huo ulioibukia nchini China mwishoni mwa Disemba mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment