Monday, 12 January 2026

BILIONI 6.7 KUBORESHA AFYA YA MAMA NA MTOTO KAHAMA

...

 







UJENZI WA JENGO LA GHOROFA TATU WAFUNGUA ENZI MPYA YA HUDUMA ZA AFYA MANISPAA YA KAHAMA


Na Neema Nkumbi, Kahama


Manispaa ya Kahama inaendelea kuandika historia mpya katika sekta ya afya baada ya kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la kisasa la mama na mtoto lenye thamani ya shilingi bilioni 6.7, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, kupunguza vifo vya mama na mtoto, pamoja na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.


Mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na halmashauri hiyo kupitia mapato ya ndani ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zinazoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha huduma za afya nchini.


Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amesema mazingira mazuri ya kiutendaji yaliyoanzishwa na serikali yameiwezesha halmashauri hiyo kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali.


Amesema mafanikio hayo yamechochea utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na sekta nyingine za kijamii, huku sekta ya afya ikipewa kipaumbele kikubwa kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa jamii.


"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazingira mazuri ya utendaji, Kupitia ongezeko la mapato ya ndani na usaidizi wa Serikali Kuu, tumeweza kuanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto lenye gharama ya shilingi bilioni 6.7 hadi kukamilika kwake," amesema Kibetu.


Ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unaendelea vizuri chini ya mkandarasi SUMA JKT, huku halmashauri ikiendelea kusimamia utekelezaji wake kwa karibu ili kuhakikisha linakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyopangwa.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Baraka Msumi, amesema jengo hilo la ghorofa tatu litakapokamilika litakuwa kituo kamili cha huduma za mama na mtoto, kikitoa huduma zote muhimu chini ya paa moja.


Amesema huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma kwa mama mjamzito, wajawazito wanaosubiria kujifungua, wodi za kujifungulia, wodi za akina mama waliokwisha kujifungua kwa uangalizi, pamoja na wodi maalum kwa akina mama wanaopata changamoto baada ya kujifungua.


"Kutakuwa pia na wodi ya uangalizi maalum (ICU), chumba cha upasuaji, wodi za watoto, wodi za watoto wanaohitaji uangalizi maalum, ICU ya watoto, ofisi za madaktari, ukumbi mdogo wa mikutano pamoja na vyumba vya wauguzi kwa ajili ya kupumzika," amesema Dkt. Msumi.


Ameongeza kuwa jengo hilo litakuwa na uwezo wa kulaza zaidi ya wagonjwa 70 kwa siku kwani Kwa mujibu wa takwimu za hospitali hiyo, zaidi ya wajawazito 700 hujifungua kila mwezi, hali inayosababisha msongamano mkubwa wa wagonjwa, jambo litakalopungua kwa kiasi kikubwa baada ya kukamilika kwa jengo hilo.


Dkt. Msumi ametoa wito kwa akina mama wajawazito kutumia vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo karibu na makazi yao, akitaja Kituo cha Afya Kagongwa na Kituo cha Afya Nyasubi ambavyo vina uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, X-ray na ultrasound, huku rufaa ikitolewa pale inapohitajika kwenda Hospitali ya Manispaa.


Akizungumza kuhusu maendeleo ya ujenzi, Mhandisi kutoka kampuni ya SUMA JKT, Elihakimu Royal, amesema mradi unaendelea vizuri na hakuna changamoto yoyote inayokwamisha utekelezaji wake.


Amesema mkandarasi huyo amejiandaa kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa, akitoa shukrani kwa Serikali na uongozi wa Manispaa ya Kahama kwa imani waliyoionesha kwa kampuni hiyo.


Ujenzi wa jengo la mama na mtoto Manispaa ya Kahama unaakisi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika sekta ya afya, inayolenga kujenga jamii yenye afya bora, inayopata huduma za afya zilizo jumuishi, za kisasa na kwa gharama nafuu.


Mradi huo pia unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan lengo namba 3 la kuhakikisha afya njema na ustawi kwa watu wa rika zote, kwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.


Wananchi wa Manispaa ya Kahama wameelezwa kunufaika moja kwa moja na mradi huo mara utakapokamilika, huku wito ukitolewa kwa jamii kushirikiana na serikali katika kutunza miundombinu ya afya ili idumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger