Tuesday, 13 January 2026

WANAOSEMA 'SAMIA MUST GO' AKITOKA UNAMUWEKA NANI PALE? - CLEMENCE MWANDAMBO

...
MWANAMITANDAO maarufu Clemence Mwandambo (maarufu kama Baba Yenu Mwandambo), ameweka wazi msimamo wake thabiti wa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa anathamini kazi kubwa inayofanywa na kiongozi huyo wa nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha Jambo TV, Mwandambo amewashangaa watu wanaopitisha kampeni za "Samia Must Go," akibainisha kuwa madai hayo hayana mashiko na yanashindwa kutoa mbadala wa uongozi thabiti uliopo sasa.

"Namkubali Rais Samia na Kazi Yake" Mwandambo, ambaye anafahamika kwa kutoa maoni yake bila uoga, amesema mapenzi yake kwa Rais Samia yanatokana na utendaji wake uliotukuka. Amesisitiza kuwa hawezi kuwa sehemu ya kundi linalopiga kelele za kutaka Rais aondoke madarakani bila sababu za msingi.

"Ninampenda Rais Samia... kama mtu, na kazi yake ninaithamini. Mimi ninamkubali. Siwezi kusema na vijana wanaosema 'Samia must go'. Wanaosema 'Samia must go', sawa akitoka unaweka nani pale? Pale ataenda kukaa mtu mwingine, sio wewe unayepiga kelele," alisema Mwandambo kwa kusisitiza.

Kada Mzalendo Mwenye "Roho ya Upinzani" 

Licha ya kuwa na kadi ya CCM tangu enzi za utawala wa Hayati Dkt. John Magufuli, Mzee Mwandambo amejipambanua kama mzalendo wa nchi ambaye hatangulizi chama mbele ya ukweli. Amefafanua kuwa ana "karoho ka upinzani" ndani yake ambako hukitumia kupinga mambo yasiyo sawa kwa maslahi ya nchi.

"Nina kadi ya Chama cha Mapinduzi, lakini karoho ka upinzani kamo. Mimi ni mzalendo wa nchi na sio mzalendo wa chama. Nikiona jambo halipo sawa, siwezi kukaa kimya, nitalipinga," alieleza kada huyo ambaye video zake zimekuwa zikivuta hisia za wengi mtandaoni.

Mwandambo ametoa rai kwa wanasiasa nchini kuacha tabia ya "uchifu" na kujiona hawawezi kuambiwa ukweli. Amesema amekuwa akitumia video zake kama njia ya kufikisha sauti ya wananchi kwa kuwa hayupo kwenye mfumo (system) wa maamuzi serikalini, lakini anasikitishwa na baadhi ya viongozi kuona maoni tofauti kama kiburi.

"Kwa bahati mbaya sana, tuna wanasiasa machifu. Hawataki kusikia wazo kinyume na wanavyofikiri. Ukitoa wazo tofauti wanakuona una kiburi. Mimi nikipaza sauti kupitia simu labda naweza kusikika, lakini wamekuwa hawaamini maoni yangu," aliongeza.

Msimamo huu wa Mzee Mwandambo umepokelewa na wengi kama alama ya ukomavu wa kisiasa, ambapo mwanachama wa chama tawala anakuwa na ujasiri wa kumuunga mkono kiongozi wake (Rais) huku akiendelea kuwa mlinzi wa haki na mshauri wa dhati kupitia kukosoa pale inapobidi.


 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger