Wednesday 31 January 2024

WALIOPATA ELIMU YA USALAMA BARABARANI DODOMA WATOA SHUKRANI KWA AMEND, USWIS

...

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

SHIRIKA la AMEND Tanzania ambalo linajihusisha na utoaji wa elimu ya usalama barabarani limepongezwa na maofisa usarishaji maarufu bodaboda katika Jiji la Dodoma kwa kuwapatia elimu ya usalama barabarani masuala ya kutoa elimu ya usalama barabarani.

Elimu hiyo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda iliyotolewa shirika hilo imetolewa kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania ambapo lengo ni kuliwezesha kundi hilo kuepushwa na ajali za barabarani kwa kupatiwa elimu ya usalama barabarani ikiwemo kutambua alama za barabarani na kufuata sheria zilizopo.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa mahojiano maalumu , madereva hao wa bodaboda waliokuwa wakitoa elimu ya usalama barabarani kwa wenzao ambao walikuwa hawajafikiwa na mafunzo hayo wamesema wanaishukuru Amend Tanzania na Ubalozi wa Uswisi nchini kwa kuwapatia mafunzo hayo.


Nuhu Toyi ambaye ni balozi wa mafunzo ya usalama barabarani na Ofisa Usafirishaji katika Jiji la Dodoma ambaye kituo chake ni UDOM amesema alibahatika kupata mafunzo na yamemsaidia kuendesha chombo chake kwa kujiamini bila kusababisha ajari.

“Pongezi za dhati ziende kwa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania hususan kitengo cha afya kinachofadhiliwa na miss Vivian kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la vijana wa bodaboda wengi ni vijana ambao tupo kati ya umri wa miaka 25.


"Kazi hii wengi tumekuwa tukiifanya kwa mazoea na hatuna elimu kwahiyo wengi tumekuwa ni waathirika wa kusababisha au kusababishiwa ajali kwasababu ya kukosa elimu barabarani lakini ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania umeona itakuwa ni vyema kama vijana hawa ambao ni taifa la kesho na nguvu kazi ya taifa wasiweze kudhuulika na ajali," amesema Toyi.
Kwa upande wake Ofisa Usafirishaji, Laurenti Mayowa amesema alikuwa haelewi alama za barabarani lakini kupitia mafunzo hayo wamepokea kutoka shirika la Amend Tanzania kwani limekuja kitofauti katika kutoa mafunzo yao kwani wamefundishwa kwa nadharia pamoja na vitendo.

“Tulipata mafunzo mazuri sana kwenye swala la uendeshaji wa pikipiki lakini pia tumeweza kufundishwa namna ya kutumia barabara lakini pia namba ya kutumi vyombo vyetu, kwa kweli mafunzo yalikuwa mazuri.

"Nimejifunza mambo mengi na mazuri na kabla ya mafunzo nilikuwa sielewi kwamba barabarani nilikuwa naendesha hovyo hovyo tu na baada ya mafunzo nashukuru mpaka sasaivi nime elewa na tulikuwa wengi sana tukifundishwa awamu kwa awamu nafikiri bodaboda takriban 230 au 250 kwa Dodoma hapa na sasahivi wame elimika”, amesema Mayowa.

Ameongeza alama za barabarani ilikuwa ni changamoto kwa madereva wengi , walikuwa wanaziona lakini wanashindwa kuzitumia kama ipasavyo na walidhani ni michoro tu lakini baada ya mafunzo waliweza kuelewa aina za michoro na alama zinazotumiwa barabarani.

“Tulifundishwa kuna alama za onyo, alama za amri, kuna alama za maelekezo kwahiyo yote haya tumefundishwa pia nimefundishwa alama nyengine ambazo nilikuwa sizielewi vizuri kama alama za michoro juu ya sakafu ya barabara hizo nazo nilikuwa sizielewi nilikuwa naona tu michoro na sielewi maana yake na baada ya elimu nimeelewa vizuri”, amesema Mayowa.


Aidha amesisitiza kwa maafisa usafirishaji kubadilika na kuwa na mahudhurio mazuri ya mafunzo yanayotolewa na shirika la AMEND Tanzania kwasababu yanafundishwa kwa vitendo pamoja na kutii sheria za barabarani.


“Tumefundishwa dereva kujihami kwahiyo wale ambao hawajapata mafunzo hawawezi kuelewa na kutii sheria akiwepo barabarani na anaweza kusababisha ajari kwasababu anakuwa hana uelewa wowote lakini vigumu kujilinda anapotumia chombo chake”,Mayowa.
Naye afisa usafirishaji kutoka kituo cha Ndasha,Ally Rashid Ally amesema kuwa bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyengine na imeteka soko kubwa la ajira kwa vijana kwenye upataji wa kipato na awali haikupewa thamani kama zilivyo biashara nyingine.

Amesema wamekuwa na madereva usafirishaji wengi lakini baadhi yao kwenye kundi hilo hawana elimu ya kutosha ya barabarani na kutambua alama zilizomo.

Ally amesema elimu iliyotewa ni msaada mkubwa kwa maafisa usafirishaji mkoani Dodoma kwani wengi wao wamekuwa na nidhamu iwapo wanatumia vyombo vyao barabarani na changamoto za ajari na vifo vimeweza kuepukika kutokana na maarifa waliopokea kutoka kwa wakufunzi kupitia shirika la AMEND Tanzania.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger